Chelsea yafuta posti ya Enzo kisa mashabiki wa England
Muktasari:
- Katika mchezo huo uliochezwa Atlanta, England ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Anthony Gordon na kuonekana kuwa njiani kutinga fainali.
MIAMI, MAREKANI: CHELSEA imejikuta kwenye wakati mgumu baada ya mashabiki wake kuishambulia vikali klabu hiyo kufuatia kuchapisha picha ya Enzo Fernandez akishangilia bao lake dhidi ya England katika nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Katika mchezo huo uliochezwa Atlanta, England ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Anthony Gordon na kuonekana kuwa njiani kutinga fainali.
Hata hivyo, Enzo Fernandez aliisawazishia Argentina dakika za mwisho kwa shuti kali lililomshinda kipa Jordan Pickford, kabla ya Lautaro Martinez kufunga bao la ushindi kwa kichwa kufuatia krosi ya Lionel Messi na kuipeleka Argentina fainali kwa ushindi wa mabao 2-1.
Baada ya bao hilo, akaunti rasmi ya Chelsea kwenye mitandao ya kijamii ilichapisha picha ya Enzo akishangilia, ikiandika:”Enzo Fernandez” ikisindikizwa na emoji ya mlipuko.
MASHABIKI WACHAFUKA
Chapisho hilo liliibua hasira kali kutoka kwa mashabiki wengi wa Chelsea, hasa wale wa England, ambao waliona halikufaa kwa klabu ya England kusherehekea bao lililoiondoa timu yao ya taifa. Mmoja wa mashabiki aliandika:
“Kwa kweli? Sisi ni klabu ya England. Hili ni kosa kubwa kutoka kwa klabu yangu.”
Mw ingine amesema:”Kwa nini klabu ya England ichapishe hili wakati Enzo amefunga dhidi ya England?”
Mashabiki wengine walihoji kuwa Chelsea imeendelea kuonyesha kutokuwa na uelewa wa hisia za wafuasi wake.
Mmoja aliandika:”Mnaonekana hamuelewi kabisa mashabiki wenu siku hizi.”
CHELSEA YAFUTA CHAPISHO
Kutokana na wimbi kubwa la malalamiko, Chelsea iliamua kulifuta chapisho hilo muda mfupi baadaye.
Hatua hiyo ilikuja baada ya maelfu ya mashabiki kuendelea kukosoa uamuzi wa idara ya mitandao ya kijamii ya klabu hiyo.
ENZO BADO GUMZO
Mbali na sakata hilo, mustakabali wa Enzo Fernandez Chelsea umeendelea kuwa gumzo baada ya kiungo huyo kukiri siku za nyuma kuwa anatamani kuishi nchini Hispania, huku akihusishwa na uhamisho wa kwenda Real Madrid.
Kauli hizo ziliwahi kumletea adhabu ya ndani ya klabu mapema mwaka huu.
Hata hivyo, kocha mpya wa Chelsea, Xabi Alonso, amesema wazi kuwa anataka Enzo abaki Stamford Bridge na kuwa sehemu muhimu ya kikosi chake msimu ujao.
Katika mchezo huo wa nusu fainali, mmiliki mwenza wa Chelsea, Todd Boehly, alikuwepo uwanjani akishuhudia mechi hiyo akiwa amevaa jezi ya timu ya taifa ya England, jambo lililoongeza uzito wa mjadala uliofuatia baada ya chapisho la Chelsea.