Michael Carrick atamani dili Man United
Muktasari:
- Carrick, ambaye aliwahi kuwa kapteni wa timu ya taifa ya England, aliajiriwa mwezi uliopita kama mbadala wa Ruben Amorim, ili kuiongoza timu hadi mwisho wa msimu.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa mpito wa Manchester United, Michael Carrick sasa yuko kwenye mchakato wa kuwa kocha rasmi wa mashetani wekundu hao.
Carrick, ambaye aliwahi kuwa kapteni wa timu ya taifa ya England, aliajiriwa mwezi uliopita kama mbadala wa Ruben Amorim, ili kuiongoza timu hadi mwisho wa msimu.
Baada ya kuajiriwa kwake, mabosi wa Man United walitaka akae kwa muda wakati mchakato wa kumsaka kocha wa kudumu wa kuchukua nafasi ya Amorim, ukiendelea.
Hata hivyo, Carrick ameanza kazi yake kwa kishindo kikubwa, akikusanya pointi 13 kati ya 15 pamoja na kuifunga Manchester City na Arsenal.
Kiwango hicho kimewafanya mabosi wa United kufikiria upya mipango yao, huku gazeti la The Sun likiripoti kuwa Carrick sasa yuko kwenye orodha ya makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kupewa mikoba.
Viongozi wa viunga vya Old Trafford wamevutiwa sana na utulivu wa Carrick pamoja uwajibikaji anaouonyesha ikiwa ni pamoja na kujitolea kwake kwenye akademi ya vijana na Man United.
Carrick alisafiri safari ya maili 300 kwenda Oxford katikati ya wiki ili kutazama timu ya vijana ya United waliokuwa wakicheza mechi ya FA Youth Cup.
Man United ilikuwa na orodha ya makocha wengi, lakini baadhi wanaonekana kukataa akiwamo kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, ambaye amesaini mkataba wa kuendelea kuifundisha timu hiyo hadi mwaka 2028.
Roberto De Zerbi naye alikuwa akihusishwa na nafasi hiyo, lakini kwa sasa hapewi nafasi kubwa kupata ajira hiyo kama ilivyo kwa kocha Crystal Palace, Oliver Glasner.
Akizungumza mapema wiki hii, Carrick alithibitisha kuwa anatamani kupewa mkataba wa kudumu: "Si mimi ninayeamua nitakaa muda gani hapa, lakini napenda kuwa hapa na nikiwa hapa nitatoa kila nilicho nacho. Daima napanga mipango ya muda mrefu kwa manufaa ya klabu."