Pato aomba kusafirisha mwili wa mrembo aliyeangukia kwenye volkano

Muktasari:
Mrembo Juliana Marins, 26, alipanda kwenye mlima wenye kilele cha futi 1,000 katika mlima wa Rinjani huko Indonesia na kujikuta akiangukia kwenye shimo lenye volkano na kujikuta akikwama huko kwa siku kadhaa kabla ya kupoteza maisha.
LONDON, ENGLAND: STAA wa zamani wa Chelsea, AC Milan, Villarreal na timu ya taifa ya Brazil, Alecandre Pato, amejitolea kutoa msaada wa kusaidia familia iliyompoteza binti yao aliyepoteza maisha baada ya kuanguka kwenye shimo lenye volkano wakati alipokuwa kwenye michezo kuvuka na kamba kwenye milima.
Mrembo Juliana Marins, 26, alipanda kwenye mlima wenye kilele cha futi 1,000 katika mlima wa Rinjani huko Indonesia na kujikuta akiangukia kwenye shimo lenye volkano na kujikuta akikwama huko kwa siku kadhaa kabla ya kupoteza maisha.
Timu ya waokoaji ilipambana kunusuru maisha yake, lakini hadi wakati wanamfikia mrembo huyo, tayari zilikuwa zimeshapita siku nne na kukutwa akiwa amepoteza maisha kutokana na majeraha. Aliangukia kwenye shimo hilo Jumamosi na mwili wake uliotolewa Jumatano.
Na sasa, straika wa zamani wa The Blues, Pato - alijitolea kugharimia gharama zote za kusafirisha mwili wa mrembo huyo hadi kwao Brazil.

Hakufahamika mapema kama familia ya mrembo Juliana imekubali kupokea ombi hilo la Pato kujitolea kusafirisha mwili wa mpendwa wao kutoka Indonesia hadi Brazil.
Familia hiyo kwa hasira tayari imetoa taarifa yake ya kukosoa vikali muongoza watalii aliyekuwa na mrembo wao Juliana alifanya makosa, huku wakipeleka lawama pia kwa waokoaji.
Dada wa Juliana, mrembo Marianna aliiambia Fantástico, Juliana aliachwa na mwogoza watalii na alipochoka alihitaji kupumzika. Kitu kilichokuwa kikifanyika kwenye milima hiyo ni kuvuka kwa kamba kutoka shimo moja kwenda jingine.
Marianna alisema: “Waliendelea tu, mwogoza watalii alimtelekeza.”

Mrembo Juliana alikuwa mmoja kati ya watalii watano waliokwenda kwenye milima hiyo, huku mwongoza watalii, aliyekuwa akiwaongoza ni mmoja tu.
Familia hiyo pia imezilaumu mamlaka za Indonesia kwa kushindwa kufanya jitihada za haraka za uokoaji, kama wangemfikia Julian kwa wakati pengine wangenusuru maisha yake.
Walisema: “Juliana alitelekezwa na timu ya uokoaji. Kama wangemfikia mapema ndani ya saa saba, basi Juliana angekuwa hai. Alihitaji huduma ya ziada. Tutatafuta haki kwa sababu anastahili.”

Mrembo Juliana alitokea kwenye jiji la Rio de Janeiro na alikuwa akiishi kwenye kitongoji cha Niterói. Alihitimu elimu ya matangazo na alikuwa akifanyakazi kama mnenguaji wanaodansi kwa kutumia mtalimbo.
Katika klipu iliyovunja moyo ya wengi ambayo ilipostiwa na rafiki yake, Federica, mrembo Juliana alionekana akitasamu wakati wakiwa kwenye kambi kabla ya kuangukia kwenye shimo hilo la volkano. Mabinti hao wawili walikuwa wakifurahia muonekano wa eneo waliokuwa, mawingu yalikuwa yametanda karibu yao kabisa.
Kwenye kipande hicho cha video, mrembo Federica alisema: “Hii viu ni matata, unaweza kuona ilivyo tamu.” Na Juliana alijibu: “Ndio, tumefika hapa kwa ajili ya hili, nimefurahi!”.

Wakati mrembo alipokuwa bado anatafutwa na timu ya uokoaji, dada yake, mrembo Mariana, alisema: “Tuliambiwa Juliana alihamaki kwa sababu hakujua cha kufanya, hilo likasababisha kuanguka. Baada ya muongoza watalii kuona amechelewa kurudi, alienda kumtazama na kugundua ameanguka chini zaidi.”
Straika Pato, 35, ambaye alistaafu soka 2023 na kuanza kazi ya uchambuzi wa soka, Novemba mwaka jana, alifunga mabao 10 katika mechi 27 alizochezea timu ya taifa ya Brazil kati ya 2008 na 2013.

Aliichezea Chelsea mara mbili mwaka 2016 – lakini alifunga kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Aston Villa. Katika maisha yake ya soka, Pato alizichezea pia AC Milan ya Italia na Villareal ya Hispania.