Palmer, lolote linaweza kutokea
Muktasari:
- Palmer ambaye alisajiliwa na Chelsea katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana akitokea Manchester City kwa Pauni 42 milioni alikosolewa na mashabiki wengi baada ya kiwango chake katika mchezo dhidi ya Everton uliomalizika kwa suluhu ya 0-0.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amesema mchezaji wake, Cole Palmer anatakiwa kufanya vizuri zaidi pale anapokuwa anawekewa mtu mmoja wa kumkaba muda wote wa mchezo, vyenginevyo anaweza akajikuta nje ya kikosi hicho.
Palmer ambaye alisajiliwa na Chelsea katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana akitokea Manchester City kwa Pauni 42 milioni alikosolewa na mashabiki wengi baada ya kiwango chake katika mchezo dhidi ya Everton uliomalizika kwa suluhu ya 0-0.
Mashabiki hao wengi walifunguka kwamba benchi la ufundi la Chelsea linatakiwa limpe pia nafasi kubwa ya kucheza Joao Felix na kumpumzisha Palmer.
Kabla ya mchezo wao wa jana dhidi ya Fulham, Maresca alisema: “(Palmer) Bado anahitaji kuboresha mambo katika nyakati hizo anazokuwa amepangiwa mtu.”
“Ninachukua uamuzi mechi moja baada ya nyingine, huwa naangalia ufungaji wa mabao na msaada ambao mchezaji anatupa sisi kama timu, kwa sasa yeye na Nicolas Jackson, sio tu kufunga mabao bali wanasaidia kwa jinsi tunavyoshambulia, lakini bado anahitaji kubadilika.”
Wakati huohuo, Maresca alisema ataruhusu uuzaji wa wachezaji watakaoomba kuondoka katika dirisha lijalo.
“Kipaumbele kipo kwa mechi ya Fulham. Hatuwazii kuhusu wachezaji wanaotaka kuondoka, lakini ikiwa watagonga mlango na wanataka kuondoka, sitasema, ‘Hapana, lazima uishi hapa’, niwaruhusu kuondoka kwa sababu jambo bora kwa kila mmoja ni kufurahi, hivyo wale ambao hawana furaha wako huru kuondoka.
Kuhusu uwezekano wa Christopher Nkunku kuondoka, Maresca alisema: “Tunampenda Christo, lakini siku zote kutakuwa na ambao hawafurahii.”