Palmeiras yatwaa Copa Libertadores
Muktasari:
- Ushindi huo umeendeleza utawala wa klabu za Brazil katika mashindano hayo makubwa zaidi ya klabu Amerika Kusini, ambapo kwa mwaka wa nane mfululizo timu kutoka nchini humo imefanikiwa kutwaa taji hilo.
MONTEVIDEO, URUGUAY: PALMEIRAS ya Brazil imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Amerika Kusini (Copa Libertadores) kwa mara ya tatu ndani ya miaka saba baada ya kuichapa Estudiantes ya Argentina kwa bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Montevideo, Uruguay.
Shujaa wa Palmeiras alikuwa mshambuliaji Ramon Sosa aliyefunga bao pekee la mchezo huo kwa shuti la karibu, akimalizia pasi ya kichwa iliyotengenezwa na Jhon Arias, aliyewahi kuchezea Wolverhampton Wanderers (Wolves).
Ushindi huo umeendeleza utawala wa klabu za Brazil katika mashindano hayo makubwa zaidi ya klabu Amerika Kusini, ambapo kwa mwaka wa nane mfululizo timu kutoka nchini humo imefanikiwa kutwaa taji hilo.
Licha ya kupoteza mchezo huo, Estudiantes ilipata nafasi kadhaa za kusawazisha, lakini ilishindwa kuzitumia.
Mshambuliaji Guido Carrillo, aliyewahi kuchezea Southampton ya England, alikuwa karibu kupata bao kupitia shuti la sarakasi akiwa angani (bicycle kick), lakini kipa Carlos Miguel, aliyewahi pia kuchezea Nottingham Forest, alifanya kazi nzuri ya kuokoa.
Kwa upande wa Estudiantes, kipigo hicho kimewaacha wakisubiri kwa muda zaidi kurejea kwenye ubingwa wa mashindano hayo, ambao mara ya mwisho waliutwaa mwaka 2009.
Wakati huo, Juan Sebastian Veron alikuwa nahodha wa timu hiyo, lakini kwa sasa anahudumu kama rais wa klabu hiyo.
Kwa upande wa Palmeiras, kocha Abel Ferreira ameiongoza timu hiyo kurejea kwenye mafanikio baada ya kupoteza fainali ya msimu uliopita dhidi ya Flamengo.
Sasa kikosi hicho kitaelekeza nguvu kwenye fainali ya Kombe la Brazil dhidi ya Gremio, itakayochezwa mwishoni mwa wiki ijayo.
Sosa, raia wa Paraguay mwenye umri wa miaka 27, aliwahi kuchezea Nottingham Forest msimu wa 2024/25, ambako alifunga mabao matatu katika mechi 23 alizoichezea klabu hiyo, ingawa alianza mchezo mmoja pekee wa Ligi Kuu England.
Ushindi wa Palmeiras unaendeleza historia ya mafanikio ya klabu hiyo katika soka la Amerika Kusini na kuifanya kuwa miongoni mwa timu zenye mafanikio makubwa katika kipindi cha hivi karibuni.