Rekodi yaipa Yanga ahueni CAFCL
Muktasari:
- Matokeo hayo yanaifanya Yanga kurudia historia ya kupoteza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi, kama ilivyokuwa katika misimu ya 2023/24 na 2024/25, baada ya kuvunja mwenendo huo msimu uliopita kwa kuanza na ushindi dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco.
YANGA imeanza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuchapwa bao 1-0 na MC Alger ya Algeria, katika mchezo ambao ilitawala umiliki wa mpira lakini ikashindwa kutumia nafasi zake, kabla ya Soufiane Bayazid kuipa timu yake ushindi kwa bao la dakika ya 90.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kurudia historia ya kupoteza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi, kama ilivyokuwa katika misimu ya 2023/24 na 2024/25, baada ya kuvunja mwenendo huo msimu uliopita kwa kuanza na ushindi dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Yanga ilimiliki sehemu kubwa ya mchezo, lakini ilishindwa kupata bao baada ya kukutana na MC Alger iliyocheza kwa nidhamu kubwa ya ulinzi na kufunga mianya iliyokuwa ikitumiwa na wenyeji kutengeneza mashambulizi.
MC Alger ilionekana kuwa na mpango wa kuizuia Yanga kwa kujaza wachezaji wengi nyuma, huku ikiiacha timu hiyo kucheza kwa uhuru katika eneo lake na sehemu kubwa ya kiungo. Hata hivyo, ilipofika katika nusu ya uwanja wa wapinzani, Yanga ilikosa mbinu za kupenya.
Hali hiyo iliifanya Yanga kuwa na umiliki mkubwa wa mpira bila kuonyesha ubunifu wa kutosha katika eneo la mwisho la ushambuliaji. Mashambulizi mengi yalikwama kabla ya kufika kwenye maeneo ambayo yangeweza kuleta hatari kwa lango la MC Alger.
Takwimu za mchezo hadi dakika ya 69 zilionyesha Yanga ilikuwa na asilimia 68 ya umiliki wa mpira dhidi ya asilimia 32 za MC Alger, lakini tofauti hiyo haikuzaa matunda kwa wenyeji. Takwimu za mwisho zilionyesha umiliki wa asilimia 67.2 kwa Yanga dhidi ya 32.8 za MC Alger.
Katika mashuti, Yanga ilipiga saba dhidi ya manne ya MC Alger, huku wenyeji wakielekeza manne langoni na wapinzani wao moja. Hata hivyo, pamoja na kutawala takwimu hizo, Yanga ilishindwa kupata bao na hatimaye kulipa gharama ya kutotumia nafasi zake.
Kipigo hicho kinaendeleza rekodi ya Yanga kuanza vibaya hatua ya makundi katika misimu mitatu kati ya minne iliyopita.
Msimu wa 2023/24, ilianza kwa kuchapwa mabao 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria, Novemba 24, 2023, lakini ilirejea nyumbani na kupata suluhu ya 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wake wa pili.
Katika mchezo wake wa tatu, Yanga ilitoka suluhu ya 1-1 ugenini dhidi ya Medeama ya Ghana, kabla ya kupata ushindi wa kwanza wa kundi hilo kwa kuichapa timu hiyo mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano.
Baadaye iliendelea kupambana na kumaliza nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi nane, nyuma ya Al Ahly iliyokuwa na pointi 12.
Msimu wa 2024/25, Yanga ilianza tena kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan, Novemba 26, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Hata hivyo, ilijibu kipigo hicho kwa kupata sare ya 1-1 ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wake wa pili, kabla ya kuichapa timu hiyo mabao 3-1 nyumbani katika mchezo wa nne.
Katika msimu huo, Yanga ilipambana hadi mchezo wa mwisho wa kundi, ilipotoka suluhu ya dhidi ya MC Alger nyumbani, lakini matokeo hayo hayakutosha kuifikisha robo fainali. Ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi nane, nyuma ya Al Hilal iliyokuwa na pointi 10 na MC Alger iliyokusanya tisa.
Hata hivyo, msimu wa 2025/26 Yanga ilivunja mwenendo wa vipigo vya mechi za ufunguzi kwa kuanza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco,
Novemba 22, 2025, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Prince Dube
Kwa maana hiyo, katika misimu minne ya karibuni ya hatua ya makundi, Yanga imeshinda mchezo mmoja na kupoteza mitatu ya ufunguzi. Rekodi hiyo inaonyesha kuwa licha ya kuanza kwa ushindi msimu uliopita, safari hii imerejea kwenye mwenendo wa kupoteza mchezo wa kwanza.