Zamalek inaharibiwa na uongozi mbovu
Muktasari:
- Akizungumza katika mahojiano na televisheni, kiongozi huyo amesema Zamalek inahitaji mabadiliko ya kiutawala pamoja na msaada wa kimaadili na kifedha kutoka kwa mashabiki wake ili kuvuka kipindi hicho kigumu.
CAIRO, MISRI: KIONGOZI wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Hany Abou Rida, amesema matatizo yanayoikabili Zamalek ya Misri yanatokana zaidi na uongozi na usimamizi mbovu kuliko ukosefu wa vipaji vya wachezaji.
Abou Rida amesema klabu hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na matumizi yake kuwa makubwa kuliko mapato inayoyapata, hali inayozidisha ugumu wa kuendesha shughuli zake.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni, kiongozi huyo amesema Zamalek inahitaji mabadiliko ya kiutawala pamoja na msaada wa kimaadili na kifedha kutoka kwa mashabiki wake ili kuvuka kipindi hicho kigumu.
"Changamoto halisi ya klabu ni uongozi. Kuna malalamiko na kesi nyingi zinazoikabili katika FIFA na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS). Uongozi unahitaji msaada wa kimaadili na kifedha kutoka kwa mashabiki ili kukabiliana na kipindi hiki kigumu," amesema.
Mbali na kuzungumzia hali ya Zamalek, Abou Rida aliipongeza timu ya taifa ya Misri pamoja na kocha wake, Hossam Hassan, kwa kufanikiwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2026.
Amesema safari ya kufuzu haikuwa rahisi kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo kwenye kundi lao, huku kila hatua ikiambatana na matokeo ya kushtukiza.
Amebainisha kuwa hata timu nyingine zenye nguvu barani Afrika, ikiwamo Nigeria, zililazimika kupitia hatua za mchujo ili kutafuta nafasi ya kushiriki fainali hizo.
Pia alimpongeza nahodha wa Misri, Mohamed Salah, akieleza kuwa nyota huyo wa Liverpool ni mfano wa kuigwa kutokana na ukomavu, ari na uwezo wake wa kuwahamasisha wenzake ndani na nje ya uwanja.
"Salah ni mfano halisi wa ukomavu na hamasa, ndani na nje ya uwanja. Ninajivunia sana mafanikio yake," amesema.