Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man United kila siku afadhali ya jana

MAN UTD Pict

Muktasari:

  • Hali hiyo imeongeza presha kwa kocha Mauricio Pochettino, ambaye anakabiliwa na kazi kubwa ya kurekebisha safu ya ulinzi ambayo imekuwa ikishindwa kuzuia wapinzani kupata mabao kwa urahisi.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inaendelea kuzama katika wakati mgumu baada ya kuchapwa mabao 4-0 nyumbani na Brentford, matokeo yaliyozidisha wasiwasi kuhusu hatma ya timu hiyo katika Ligi Kuu England.

Kipigo hicho kimeifanya United kufikisha mabao 25 iliyofungwa katika mechi nane za mashindano yote tangu ilipolazimishwa sare ya 1-1 na Leeds United Oktoba 18, huku katika mechi zake nne zilizopita pekee ikiruhusu mabao 14.

Hali hiyo imeongeza presha kwa kocha Mauricio Pochettino, ambaye anakabiliwa na kazi kubwa ya kurekebisha safu ya ulinzi ambayo imekuwa ikishindwa kuzuia wapinzani kupata mabao kwa urahisi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Liverpool, Pochettino alipoulizwa kuhusu udhaifu wa safu yake ya ulinzi, alikwepa kujadili mwenendo wa timu hiyo kwa ujumla, akisema angeweza kuzungumzia tu mambo yaliyotokea tangu alipoanza kazi ndani ya klabu.

Hata hivyo, wiki moja baadaye, baada ya United kufungwa tena mabao manne na Brentford, suala hilo liliibuka upya.

Alipoulizwa namna ya kutatua tatizo hilo, kocha huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur, Paris Saint-Germain na Chelsea amesema suluhisho ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Alieleza kuwa wanahitaji kuboresha muunganiko kati ya wachezaji, kuendelea kufanya mazoezi, kuchambua video za mechi na kutafuta mbinu sahihi zitakazowasaidia kurejesha uimara wa timu.

Pochettino alikiri kuwa hali ilivyo sasa ni ngumu kuliko alivyotarajia, lakini akasisitiza kuwa ni lazima waikubali hali halisi na kutafuta namna ya kutoka hapo.

MAN 01

Hata hivyo, tatizo la United si idadi ya mabao inayofungwa pekee, bali pia kushindwa kuhimili presha baada ya kuruhusu bao la kwanza.

Katika mchezo dhidi ya Brentford, kama ilivyokuwa katika mechi nyingine za msimu huu, United ilionekana kuwa na vipindi vizuri vya mchezo, lakini ilishindwa kutumia nafasi zake na kujikuta ikipoteza kutokana na makosa ya kujilinda.

Kocha wa Brentford, Keith Andrews, alieleza kuwa moja ya maendeleo muhimu kwa timu yake ni uwezo wa kupokea pigo ndani ya mchezo, kusimama tena na kuendelea kupambana bila kuruhusu tukio moja kuathiri mwenendo mzima wa timu.

Huo ni uwezo ambao United imekuwa ikikosa katika kipindi hiki.

Pochettino alikiri kuwa bao la kwanza walilofungwa dhidi ya Brentford lilikuwa rahisi kuzuilika, lakini lilipatikana na kubadilisha kabisa mwenendo wa mchezo.

Amesema baada ya kufungwa, wachezaji walionekana kupoteza utulivu, hali iliyochangia kushuka kwa kiwango na kuathiri kujiamini kwao.

Kocha huyo alisisitiza umuhimu wa wachezaji kubaki pamoja, kusaidiana na kuendelea kupambana licha ya changamoto wanazokutana nazo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo, Pochettino ameongeza kuwa timu inahitaji kuboresha maeneo mengi na si kutegemea suluhisho moja pekee.

Amesema wakati mwingine timu inaweza kuboresha mambo mbalimbali, lakini matokeo yasiwe mazuri mara moja, jambo linalofanya juhudi hizo zisionekane kuwa na thamani kwa watu wanaopima kila kitu kwa matokeo.

Alifafanua kuwa katika soka, timu inaweza kufanya mambo yasiyo sahihi na kupata matokeo mazuri, lakini inapokuwa kwenye kipindi kigumu, hata inapojaribu kurekebisha makosa, hulazimika kusubiri hadi juhudi hizo zianze kuzaa matunda.


MAN 02

SHIDA ZAIDI YA UWANJANI

Mbali na matokeo mabaya, United inakabiliwa pia na changamoto za uongozi na uhusiano wake na mashabiki.

Katika mchezo dhidi ya Brentford, maandamano ya mashabiki wanaopinga umiliki wa klabu yaliendelea, huku nyimbo za kumuunga mkono aliyekuwa kocha Michael Carrick na kumkosoa mkurugenzi wa soka Jason Wilcox zikisikika uwanjani.

Baada ya United kufungwa bao la nne, mashabiki waliokuwa karibu na jukwaa la viongozi walielekeza hasira zao kwa Wilcox na Ofisa Mtendaji Mkuu, Omar Berrada. Hali hiyo iliendelea hata baada ya filimbi ya mwisho.

Katika jukwaa hilo walikuwepo pia Sir Alex Ferguson na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, David Gill, ambao walishuhudia hali ya klabu ambayo wakati wao ilipitia kipindi cha mafanikio makubwa.

Kwa sasa, United inakabiliwa na hatari ya kushuka daraja ikiwa haitabadilisha mwenendo wake haraka. Hatua hiyo itakuwa pigo kubwa kwa klabu hiyo inayotajwa miongoni mwa zenye utajiri mkubwa duniani.

Aliyekuwa kiungo wa timu ya taifa ya England, Danny Murphy, amesema United kwa sasa ipo kwenye vita ya kuwania kubaki Ligi Kuu na haiwezi kukwepa ukweli huo.

Murphy alieleza kuwa kipigo dhidi ya Brentford kilipaswa kuwa somo kubwa kwa Pochettino, hasa kuhusu namna anavyoipanga timu yake inapokabiliana na wapinzani wenye uwezo wa kushambulia kwa kasi.

Amesema United haiwezi kuendelea kucheza kwa kujiachia katika safu ya ulinzi huku ikiruhusu wapinzani kupata nafasi nyingi za kufunga.

Kwa mtazamo wake, Pochettino anapaswa kuweka kando matarajio ya mashabiki kuhusu aina ya soka ambayo Manchester United inapaswa kucheza na kuanza kutumia mbinu zinazolenga kuimarisha ulinzi.

Alisisitiza kuwa timu inahitaji kuwa na wachezaji wengi nyuma ya mpira, kupunguza nafasi kati ya mabeki, kucheza kwa nidhamu na kujenga uimara wa kuzuia mashambulizi.

Kwa mujibu wa Murphy, United inapaswa kuanza kwa kutafuta sare na kutunza lango lake bila kuruhusu mabao ili kurejesha kujiamini kabla ya kufikiria kurejea kwenye soka la kushambulia kwa nguvu.

Alionya kuwa timu hiyo ikiendelea kucheza kwa kushambuliana na wapinzani wake katika hali ya sasa, itaendelea kupoteza mechi.


MAN 04

DENI LAZIDI KUWA KIKWAZO

Pamoja na matatizo ya kiufundi, hali ya kifedha ya Manchester United nayo inazidisha ugumu wa kutafuta suluhisho.

Klabu hiyo inadaiwa zaidi ya pauni1.1 bilioni na ilikopa pauni 10 milioni muda mfupi baada ya kutumia pauni milioni tisa kupata huduma za Pochettino na benchi lake la ufundi kutoka Shirikisho la Soka la Marekani.

Hali hiyo inaonyesha kuwa klabu haiwezi kutegemea dirisha la usajili pekee kutatua matatizo yake.

Pochettino alihoji matarajio ya watu wanaotaka kuona mabadiliko makubwa ndani ya muda mfupi, akieleza kuwa haiwezekani kubadilisha wachezaji 25 au 26 mara moja.

Pia, alikataa kuwatupia lawama wachezaji kwa hali ambayo klabu inakabiliana nayo, akisisitiza kuwa wanahitaji kushirikiana kutafuta suluhisho.

Kwa sasa, United inasubiri kucheza mechi sita zaidi za Ligi Kuu kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa, lakini swali kubwa ni kama itaweza kujinasua kwenye hali hii kabla haijachelewa.

Iwapo Crystal Palace itaifunga Hull City katika mchezo wake wa Jumapili, United inaweza kushuka hadi nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi. Palace pia ilikuwa na nafasi ya kuipita United katika michezo iliyofuata dhidi ya Chelsea na Newcastle.

Kwa klabu yenye historia na mafanikio makubwa kama Manchester United, hatari ya kushuka daraja si jambo la kupuuzwa tena.


MAN 03

TAKWIMU ZINAZOZIDISHA SHAKA

Takwimu za Manchester United katika msimu huu zinaonyesha ukubwa wa tatizo linaloikabili klabu hiyo.

- Imeshindwa kutunza lango lake bila kuruhusu bao katika mechi zake 12 za mwanzo za Ligi Kuu msimu huu, jambo ambalo haikuwahi kulifanya tangu msimu wa 1930/31, ilipomaliza ikiwa mkiani mwa ligi.

- Imekuwa timu ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kuruhusu angalau mabao mawili katika kila kipindi kati ya vipindi saba mfululizo vya mchezo.

- Imefungwa mabao manne au zaidi katika mechi tatu mfululizo za ligi kwa mara ya kwanza tangu Novemba na Desemba 1961.

- Pochettino amekuwa kocha wa pili katika historia ya Ligi Kuu England kupoteza mechi zake mbili za kwanza kwa tofauti ya mabao manne au zaidi, akitanguliwa na Dave Jones aliyefanya hivyo akiwa Wolverhampton Wanderers mwaka 2003.

- Kati ya timu 27 zilizokuwa na pointi nane baada ya mechi 11 katika historia ya Ligi Kuu England, timu 17 zilishuka daraja.

- United ilifungwa mabao 50 ya Ligi Kuu msimu uliopita, lakini haikusajili beki mpya katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

- Mabeki wanne kati ya watano waliotumika na United katika mchezo dhidi ya Brentford walikuwa sehemu ya kikosi kilichofungwa mabao 4-0 na timu hiyo hiyo zaidi ya miaka minne iliyopita.