Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arsenal vs Man City mambo matano kuamua mechi, mbio ubingwa

Muktasari:

  • Arsenal na Manchester City zitakutana kwa mara ya kwanza katika mechi ya ushindani msimu huu kwenye pambano ambalo limekuwa bila shaka, miongoni mwa mechi kubwa zaidi za soka la England linapokuja suala la kuamua hatima ya ubingwa.

LONDON, ENGLAND: MACHO yote yatakuwa kwa Arsenal na Manchester City, leo Jumapili zitakapokutana katika Uwanja wa Emirates kwenye Ligi Kuu England, na hapa tunaangazia baadhi ya simulizi muhimu kabla ya mchezo huo.

Arsenal na Manchester City zitakutana kwa mara ya kwanza katika mechi ya ushindani msimu huu kwenye pambano ambalo limekuwa bila shaka, miongoni mwa mechi kubwa zaidi za soka la England linapokuja suala la kuamua hatima ya ubingwa.

Mchezo huo unaonekana kuwa na hali tofauti kidogo kutokana na sakata la nje ya uwanja linaloikabili City, ambalo limekuwa likizungumziwa sana, pamoja na uwezekano wa klabu hiyo kupewa adhabu. Hata hivyo, mambo hayo yatakuwa mbali na mawazo ya wachezaji wote pindi mechi itakapoanza. Kabla ya pambano hilo la vigogo, tumebainisha mambo matano muhimu yanayopaswa kuzingatiwa.


KWA MAN CITY USHINDI LAZIMA

Hali haionekani kuwa nzuri kwa City, sivyo? Weka kando tuhuma 114 ambazo klabu hiyo imekutwa na hatia nazo, ingawa inaendelea kupinga madai hayo na kukata rufaa, pamoja na adhabu yoyote inayoweza kuikabili ambayo ina uwezo wa kuharibu msimu wake na pengine hata misimu inayofuata. Hata ukitazama msimu huu pekee, bila kuhusisha uwezekano wa kukatwa pointi, hali inazidi kuwa mbaya.

Tangu Enzo Maresca ashinde mechi saba za kwanza za Ligi Kuu England na kuanza kwa kasi kubwa katika kipindi cha baada ya Pep Guardiola, City imeporomoka. Ilipoteza mechi tatu zilizofuata kabla ya kupata sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Fulham mwishoni mwa wiki iliyopita. Katika Ligi ya Mabingwa katikati ya wiki, ilionekana kuwa kivuli cha timu iliyokuwa bora wiki chache zilizopita, huku bao la kusawazisha la Rayan Cherki dakika za mwisho likiiokoa na kuipa pointi moja nyumbani dhidi ya Napoli.

Sasa City iko pointi sita nyuma ya Arsenal na inaonekana kupoteza mwelekeo kwa kasi. Kwa mujibu wa Opta, ina nafasi ya asilimia 10.1 pekee ya kuifikia Arsenal na kutwaa ubingwa. Nafasi za Arsenal zinakadiriwa kuwa asilimia 74.4.

Kwa sasa Arsenal ni timu yenye nguvu zaidi, jambo linaloonekana pia katika utabiri huo ambao unaipa City nafasi ya asilimia 22.2 pekee ya kushinda mechi ya leo Jumapili. Tangu msimu wa 2021/22, hii ndiyo nafasi ndogo zaidi ambayo City imewahi kupewa ya kushinda mechi ya ligi.

Hata hivyo, huhitaji hilo kujua kwamba Arsenal ina uwezekano mkubwa wa kushinda. Haijafungwa katika mechi tano kati ya sita zilizopita dhidi ya City, ndiyo timu inayofanya vizuri zaidi kwa sasa na ndiyo bingwa wa Ligi Kuu England.

Ili msimu huu uwe na ushindani wa kuwania ubingwa, City inabaki kuwa matumaini makubwa ya mashabiki wasioegemea upande wowote, hasa ikiwa itaepuka kukatwa pointi. Hata kama haitapambana kikamilifu kuwania taji, bila kupata matokeo mazuri leo, huenda mbio za ubingwa zikawa zimeisha kwa timu nyingine kabla ya Novemba kumalizika, hasa ikizingatiwa Arsenal iliifunga Liverpool Anfield mapema mwezi huu.

Je, timu nyingine zitaweza kurejea ikiwa Arsenal itashinda hapa? Inawezekana kabisa zisifanikiwe. Hilo linaweka shinikizo kubwa kwa City kupata matokeo.

NDO MCHEZO WA HAALAND?

Kwa kuzingatia umuhimu wa mabao yake katika mafanikio ya timu, haishangazi kuona kwamba Erling Haaland anaposhuka kiwango cha ufungaji, kwa viwango vyake mwenyewe, City nayo inaporomoka.

Man City haijashinda mechi yoyote kati ya nne zilizopita za ligi na bao lake la mwisho katika ligi lilifungwa kwenye mchezo wa kwanza wa mfululizo huo ilipofungwa 2-1 na Aston Villa. Kukaa mechi tatu bila kufunga bao siyo jambo la kutisha sana na siyo mara ya kwanza kwa Haaland kufanya hivyo. Lakini unapokuwa umezoea kumuona akifunga kwa urahisi ni vigumu kutotambua hata kipindi kifupi cha ukame.

Hii ni mara ya nane kwa Haaland kucheza mechi tatu au zaidi za Ligi Kuu bila kufunga bao. Hata hivyo, ni mara mbili tu zilizopita ambapo amekaa mechi nne bila kufunga, na hajawahi kwenda zaidi ya hapo.

Lakini kama kuna mchezo unaoweza kumfufua Haaland ni huu… mipambano ya wachezaji binafsi na uhasama kati yao siyo mambo yanayopewa uzito mkubwa kama ilivyokuwa zamani. Hata hivyo, pambano kati ya Haaland na Gabriel Magalhaes huenda likawa mfano wa karibu zaidi wa hali hiyo katika ligi hiyo kwa sasa. Wamekuwa na mipambano mikali katika miaka michache iliyopita. Hata hivyo, mara chache Arsenal na Gabriel wameweza kumzuia Haaland kabisa, kwani mshambuliaji huyo wa Norway amefunga katika mechi zote isipokuwa mbili kati ya nane alizocheza dhidi ya Gunners kwenye Ligi Kuu England.

Mara ya mwisho Haaland na Gabriel kukutana uwanjani ilikuwa katika Kombe la Dunia 2026, Norway ilipocheza dhidi ya Brazil, na mshambuliaji huyo wa kati wa City alishinda pambano hilo kwa kiwango cha wazi. Alimpita Gabriel na kufunga bao la kwanza la Norway dakika ya 79. Kisha akapiga shuti kali na kufunga bao la pili akiwa nje kidogo ya eneo la penalti, baada ya mabeki wawili wa kati wa Brazil kumpa muda na nafasi.

Haaland anajitaka sana yeye mwenyewe na wenzake. Kushindwa na Gabriel hakutamfurahisha, na bila shaka atakuwa na hamasa ya kuhakikisha hilo halijirudii.


ARSENAL INAANZA KUTOKUWA SALAMA

Arsenal ni mabingwa wa ushindi wa bao moja, na mara nyingi hushinda kwa matokeo ya 1-0, kama wimbo wao maarufu unavyosema.

Ushindi wao dhidi ya Hull City kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa ulikuwa wa 34 wa mabao 1-0 katika Ligi Kuu England chini ya Mikel Arteta. Hilo, pengine bila kushangaza, ni zaidi ya timu nyingine yoyote tangu Mhispania huyo achukue jukumu la kuinoa.

Katika mechi 11 za mwanzo za msimu huu pekee, Arsenal imepata ushindi wa 1-0 mara nne, pamoja na ushindi mwingine miwili wa 2-1. Hakuna timu katika miaka ya karibuni iliyoweza kulinda ushindi wa bao moja kwa ufanisi kama Arsenal hii, hasa kwa sababu inaruhusu wapinzani kupata nafasi chache sana.

Baada ya kupata bao la kuongoza, Arsenal ni hodari wa kuwazuia wapinzani wake wasikaribie lango lake. Inapokuwa mbele, huruhusu nafasi zenye thamani ya ndogo zaidi kufungwa kwa kila dakika 90, kiwango kilicho chini ya wakati inakuwa sare (0.77) au inapokuwa nyuma (1.1).

Hiyo ni rekodi ya pili kwa ubora katika ligi, nyuma ya Tottenham Hotspur (0.35), ambayo imecheza kwa muda wa saa tatu na nusu pungufu ikiwa mbele ya wapinzani wake kuliko Arsenal. Siyo jambo la ajabu kuona Gunners ikipata bao la kuongoza na wapinzani wake kushindwa hata kulikaribia lango.

Lakini, katika wiki iliyopita, Arsenal imepoteza uongozi dhidi ya Newcastle United na Borussia Dortmund. Katika mechi zake mbili zilizopita, imeonekana kuwa dhaifu kidogo na kwa namna isiyo ya kawaida inapokuwa mbele. Baada ya kuruhusu mabao, ilikaribia kupoteza mechi zote mbili. Newcastle iliongoza 2-1 kabla ya Arsenal kusawazisha, huku Dortmund ikiona bao la Jobe Bellingham likifutwa kwa sababu ya kuotea.

Hata kwa Arsenal hii, uongozi wa bao moja unaanza kuonekana kutokuwa imara sana. Kwa hiyo, ikipata bao la kuongoza leo Jumapili, huenda inapaswa kutafuta la pili au zaidi.


RAYA VS KEPA

Mashabiki wa Arsenal huenda walikuwa na hofu kubwa David Raya alipoumia bega katika mchezo dhidi ya Newcastle mwishoni mwa wiki iliyopita. Hofu hiyo iliongezeka zaidi baada ya picha zake kuonekana akiwa amefungwa mkono kwa kitambaa maalumu.

Mhispania huyo amekuwa mchezaji wa kipekee tangu alipojiunga na klabu hiyo kutoka Brentford 2023, akishinda tuzo ya Golden Glove ya Ligi Kuu England kwa misimu mitatu mfululizo. Ni Pepe Reina, Joe Hart na Ederson pekee waliowahi kufikia mafanikio hayo kabla yake.

Uwezo wake wa kuokoa mashuti umekuwa muhimu, lakini pia utulivu wake anapokuwa chini ya presha na uwezo wake wa kupiga pasi. Kwa hiyo, ilipoonekana kuwa huenda ameumia vibaya, wasiwasi haukuwa tu kuhusu uwezo wa Arsenal kuzuia mabao.

Kwa bahati nzuri, Arteta alithibitisha siku chache baadaye kwamba Raya hatafanyiwa upasuaji na angerudi uwanjani hivi karibuni.

Inaonekana hakuna wasiwasi wa muda mrefu kuhusu jeraha hilo, ingawa bado haijafahamika kama Raya atakuwa tayari kuanza mchezo wa Jumapili. Ikiwa hatakuwa tayari, Kepa Arrizabalaga ataendelea kuwa kipa wa kwanza, baada ya kucheza katika sare ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Borussia Dortmund katikati ya wiki.

Kwa upande wa Kepa, amepiga hatua kubwa tangu alipopata wakati mgumu baada ya kujiunga na Chelsea kutoka Athletic Club 2018. Kipindi chake cha mkopo Bournemouth msimu wa 2024/25, kabla ya kujiunga na Arsenal, kilimsaidia kurejesha sifa yake England.

Kwa mfano, makosa yake matatu yaliyosababisha wapinzani kupiga mashuti katika msimu huo yalikuwa machache ikilinganishwa na Raya, aliyefanya makosa tisa. Hata hivyo, ni wazi kwamba Kepa hana ushawishi wala uwezo wa kupiga pasi kama Raya. Kepa alipiga pasi 105 zilizovunja mistari ya wapinzani msimu wa 2024/25, idadi iliyo chini sana ya Raya aliyepiga 193 katika msimu huohuo.

Raya alipiga pasi hizo 269 msimu uliopita, na kwa sasa anashika nafasi ya tatu akiwa na 121 katika msimu huu. Pia Raya ni kiongozi anayeleta utulivu katika safu ya ulinzi na mara nyingi huweka mwelekeo wa Arsenal inapokuwa na mpira. Kukosekana kwake katika mchezo mkubwa kama huu, hasa ikizingatiwa kwamba City hupiga presha ya juu, kunaweza kuwa pigo kubwa kwa Arsenal.


KOSA LA MCHEZAJI KUAMUA MATOKEO?

Wachezaji bora wanaweza kuonekana kuwa watulivu kiasi cha kufanya iwe vigumu kufikiria kwamba wanapata presha yoyote. Hata hivyo, haipaswi kupuuzwa jinsi presha inavyoweza kuwa na mchango mkubwa katika mechi kubwa kama hizi.

Mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu England kati ya timu hizo zimekuwa na mabao sita yaliyotokana moja kwa moja na makosa ya wapinzani. Miongoni mwao ni kosa la Gianluigi Donnarumma lililompa Kai Havertz nafasi ya kufunga bao la kusawazisha la Arsenal katika mchezo wao wa mwisho wa ligi mwezi Aprili. Hata hivyo makosa yameanza kuathiri misimu ya timu zote mbili, ingawa kwa viwango tofauti.

Katika mechi zao nne zilizopita, City imefanya makosa manne yaliyosababisha wapinzani kufunga mabao. Ni timu nne pekee zilizofanya makosa mengi zaidi ya aina hiyo katika msimu mzima kuliko City ilivyofanya katika mechi zake nne za mwisho.

Kwa upande mwingine, kulikuwa na kipindi ambacho makosa yalikuwa yakifafanua na hatimaye kuamua hatima ya Arsenal katika mbio za ubingwa. Msimu huu, karibu ilikuwa imeondoa kabisa makosa ya gharama kubwa katika mchezo wake, hadi wiki iliyopita.

Arsenal ilipopoteza pointi kwa mara ya pili pekee katika msimu wa 2026/27, kwenye sare dhidi ya Newcastle, ilifanya kosa lake la kwanza la gharama kubwa msimu huu. Martin Odegaard alijaribu kupiga mpira kwa mguu, lakini akaukosa wakati wa kurusha mpira kutoka nje ya uwanja, muda mfupi kabla ya Harvey Barnes kufunga bao la kusawazisha. Inaeleweka kwamba kadiri uchovu unavyoongezeka, ratiba ya mechi inavyobana na presha kuongezeka, makosa yanaweza kuanza kujitokeza kwa baadhi ya wachezaji.

Pia haitakuwa jambo la kushangaza ikiwa kosa jingine kubwa litatokea Emirates leo Jumapili. Na kwa kuzingatia tofauti ndogo zinazoweza kuamua matokeo ya mechi kama hii, kosa hilo linaweza kuwa na athari kubwa sana.