Pale Arsenal! Gyokeres anaomba asisti tu
Muktasari:
- Straika Gyokeres, 27, amewasili Arsenal kwa ada ya Pauni 63.7 milioni wikiendi iliyopita, wakati aliposaini mkataba wa miaka mitano.
LONDON, ENGLAND: WAPINZANI wa Arsenal kwa msimu ujao, kazi mnayo. Unajua kwa nini, straika mpya wa miamba hiyo ya Emirates, Viktor Gyokeres baada ya kutua, amekuwa na ombi moja tu kutoka kwa nahodha wa kikosi na kiungo mchezeshaji, Martin Odegaard, alipomwambia: “Nataka asisti tu”.
Straika Gyokeres, 27, amewasili Arsenal kwa ada ya Pauni 63.7 milioni wikiendi iliyopita, wakati aliposaini mkataba wa miaka mitano.
Kuwasili kwa straika huyo kumemaliza mchakato wa Arsenal wa kusaka straika mpya kwa muda mrefu na Kocha Mikel Arteta sasa anaamini amemaliza tatizo lililokuwa likiikabili timu yake msimu uliopita.
Gyokeres alifunga mabao 97 katika mechi 101 alizochezea Sporting Lisbon na kumfanya awe mmoja wa mastraika matata kabisa Ulaya kwa sasa.
Lakini, anachohitaji mkali huyo wa zamani wa Coventry City ni kupewa pasi za kutosha, hasa akimpa kazi kiungo Odegaard kuhakikisha anampa asisti.
Katika video iliyopostiwa kwenye chaneli ya mitandao ya kijamii ya Arsenal, Gyokeres alionekana akisoma barua kutoka kwa nahodha wa miamba hiyo.
“Kama kuna kitu chochote unataka au msaada wowote, we nipigie kelele,” hivyo ndivyo ilivyosomeka sehemu ya meseji ya Odegaard kwa straika huyo.
“Zile asisti tafadhali, hiyo itakuwa safi,” alijibu Gyokeres.
Kisha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 aliendelea kusoma, akisema: “Nasubiri kwa hamu kufanya kazi pamoja na kupata mafanikio msimu huu. Kila la heri, Martin.”
Straika huyo wa kimataifa wa Sweden alikutana na Odegaard kwa mara ya kwnaza Jumapili iliyopita, alipowasili Singapore kutazama mechi ambayo Arsenal iliichapa Newcastle 3-2. Odegaard alifunga bao la ushindi, wakati alipopiga mkwaju wa penalti dakika 84.
Mechi ijayo, Arsenal itakipiga na mahasimu wao wa Londo, Tottenham huko Hong Kong, Alhamisi. Gyokeres anaweza kuanza kuitumikia Arsenal katika mechi hiyo ya kirafiki, lakini kwa kukosa utimamu wa mechi kunaweza kumchelewesha kuonekana uwanjani akiwa na uzi wa Arsenal.
Kocha Arteta hakufuta uwezekano wa Gyokeres kutocheza mechi hiyo, aliposema: “Sawa, tutafikiria kwa sababu bado hajafanya mazoezi na wenzake tangu alipocheza mechi ya mwisho Sporting ilipochukua ubingwa.
“Hivyo, tutamfanyia utafiti wa kina, alifanyiwa vipimo vyote na kila kitu kipo vizuri, lakini atalazimika kufanya haraka kuwa fiti kwa ajili ya mechi na hilo ndilo jambo muhimu. Hivyo, hatutamzuia, tunamhitaji haraka iwezekanavyo.”
Kama atacheza, Gyokeres ataonekana na jezi Namba 14 mgongoni, ambayo iliwahi kuvaliwa na gwiji Thierry Henry. Mechi yake ya kwanza ya kimashindano itakuwa dhidi ya Manchester United kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England, itakayopigwa wikiendi ya Agosti 17.