OLE WENU! Amorim awapiga mkwara mastaa Man Utd
Muktasari:
- Amorim ambaye bado hajapata kibali cha kazi England, aliwasili Manchester wiki hii ambapo kwa siku chache zilizopita amekutana na wafanyakazi wengine na kutembelea miundombinu ya timu hiyo ikiwemo sehemu za kufanyia mazoezi pamoja na Uwanja wa Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA mpya wa Manchester United, Mreno Ruben Amorim amewachana wachezaji wenye umri wa mdogo katika timu hiyo akisema hawana kisingizio kulingana na na umri wao akiwataka wawe tayari kuipa timu kitu inachostahili wakati wote wanapokuwa uwanjani.
Amorim ambaye bado hajapata kibali cha kazi England, aliwasili Manchester wiki hii ambapo kwa siku chache zilizopita amekutana na wafanyakazi wengine na kutembelea miundombinu ya timu hiyo ikiwemo sehemu za kufanyia mazoezi pamoja na Uwanja wa Old Trafford.
Kocha huyo aliulizwa kuhusu wachezaji vijana waliopo katika timu kwa sasa ambao ni pamoja na Kobbie Mainoo, Alejandro Garnacho, Amad Diallo, Leny Yoro na Rasmus Hojlund waliotwishwa imani kubwa na mashabiki wanaoamini wana vipaji vikubwa, lakini tangu kuanza kwa msimu huu hawajaonyesha kiwango bora wakikwamishwa na vitu mambo mbalimbali ikiwemo majeraha.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu alipowasili Manchester, Amorim alisema: "Sitaki kusema tunahitaji muda kwa sababu tuna wachezaji vijana wengi. Naamini wako tayari. Wako tayari kukabiliana na mahitaji ya kuichezea Manchester United. Wanapaswa kuwa tayari kwa sababu wako hapa.
"Tunajua itachukua muda na tutajaribu kushinda mechi kwenye huo muda. Ni lazima tuanze bila visingizio, bila kufikiria kwamba hawawezi kucheza hivi. Hii haiko akilini mwangu. Wataanza siku ya kwanza na wazo la kushinda bila kujali umri. Hilo ndilo lengo."
Amorim alisaidia wachezaji wengi vijana kuonyesha uwezo alipoiongoza Sporting Lisbon na anatarajiwa kufanya hivyo pia akiwa na Man United.
Kocha huyo pia alisema moja kati ya mambo ambayo anataka kuanza nayo ni kuhakikisha timu inakuwa na utambulisho na staili ya uchezaji inayoeleweka, jambo ambalo lilikuwa likilalamikiwa halikuwepo wakati wa Erik ten Hag.
"Tunajua tunahitaji muda, lakini tunapaswa kushindana na muda. Na maana ya kushinda muda ni kushinda mechi. Lakini jambo muhimu kwangu ni utambulisho.
"Hivyo, tangu siku ya kwanza tutaanza na utambulisho wetu. Bila shaka tutajiandaa kwa mechi, lakini tutazingatia sana aina ya uchezaji wetu, jinsi ya kucheza, jinsi ya kushambulia."