Odegaard akiwa bora, Arsenal usipime
Muktasari:
- Msimu uliopita, Arsenal ilibakiwa na mechi mmoja kufikia ndoto ya kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa, licha ya Odegaard kukumbwa na majeraha yaliyopunguza makali ya kiwango chake.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL inaonekana kuwa tayari kukabiliana na kila mtihani msimu huu, huku nahodha wake Martin Odegaard akianza kuonyesha kiwango bora zaidi cha soka lake, jambo linaloongeza matumaini ya klabu hiyo kufanya vizuri katika Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu uliopita, Arsenal ilibakiwa na mechi mmoja kufikia ndoto ya kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa, licha ya Odegaard kukumbwa na majeraha yaliyopunguza makali ya kiwango chake.
Sasa, katika harakati za kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita, ambao waliutumia kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa Ligi Kuu baada ya miaka 24, kocha Mikel Arteta amepata sababu ya kutabasamu baada ya Odegaard, 27, kuanza msimu akiwa katika kiwango bora.
Arsenal ilitawala mchezo dhidi ya Napoli katika mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, lakini ilihitaji ubora wa Odegaard kupata ushindi wa bao 1-0 baada ya kiungo huyo kufunga kwa shuti kali la mguu wa kushoto dakika 15 kabla ya mchezo kumalizika.
Uwepo wa Odegaard katika kiwango hicho unaifanya Arsenal ionekane kuwa na uwezo wa kuvuka vikwazo mbalimbali na kuongeza matumaini ya Arteta kufikia malengo yake.
Msimu uliopita, Odegaard alisumbuliwa na majeraha ya goti na bega yaliyomfanya acheze mechi 36 tu katika mashindano yote, akifunga bao moja na kutoa pasi saba za mabao. Katika Ligi Kuu England alicheza mechi 24 pekee.
Alianza kuonyesha dalili za kurejea kwenye kiwango chake wakati Norway ilipofika robo fainali ya Kombe la Dunia kabla ya kutolewa na England, lakini tangu kuanza kwa msimu huu ameonekana kuwa katika kiwango kingine kabisa.
Odegaard alitoa ishara ya kiwango hicho katika ushindi wa Arsenal wa mabao 3-0 dhidi ya Manchester City kwenye Ngao ya Jamii, akifunga bao la kuvutia baada ya kumkalisha chini kipa Gianluigi Donnarumma kabla ya kutinga mpira wavuni.
Baadaye alifunga katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coventry City, kabla ya kufunga bao la ushindi katika mchezo ambao Arsenal iligeuza matokeo na kuichapa Chelsea 2-1 Uwanja wa Emirates, hivyo kuendeleza mwanzo wa msimu wa ushindi wa asilimia 100.
Katika mchezo huo dhidi ya Chelsea, Odegaard alifunga baada ya kufanya mbio nzuri kuelekea eneo la hatari, akitumia kwa akili ujanja wa Kai Havertz na kisha kumalizia kwa nguvu.
Bao hilo pamoja na lile alilofunga dhidi ya Napoli ni ushahidi wa mchezaji mwenye kipaji kikubwa anayerejea kileleni mwa kiwango chake, akiwa fiti na akicheza katika timu iliyojaa kujiamini kutokana na mafanikio iliyoyapata.
Ushindi dhidi ya Napoli ulikuwa muhimu kwa Arsenal kutokana na michezo migumu inayowasubiri kwenye Ligi ya Mabingwa, ikiwamo dhidi ya Real Madrid na safari ya kwenda kuikabili Bayern Munich.
Namna Arsenal ilivyovunja taratibu ulinzi wa Napoli pia ilionyesha utulivu na ukomavu, licha ya wenyeji hao kutumia mfumo wa kujilinda kwa wingi uliokumbusha falsafa ya kocha mkongwe Max Allegri.
Kwa kila mchezo unaopita, Arsenal inaonekana kuwa timu inayotaka kujenga zaidi juu ya mafanikio ya msimu uliopita.
ODEGAARD AKIWA BORA
Msimu huu, Odegaard anaonekana kucheza kana kwamba ana jambo la kuthibitisha, akifahamu kuwa licha ya Arsenal kupata mafanikio makubwa msimu uliopita, mchango wake binafsi haukuwa katika kiwango alichotarajia.
Mchezaji wa zamani wa Ligi Kuu England, Nedum Onuoha, alisema Odegaard atataka kuwa na mchango mkubwa zaidi katika timu hiyo msimu huu.
"Arsenal bado ina kazi haijamaliza kwenye Ligi ya Mabingwa. Anataka kuwa nahodha wa kwanza wa Arsenal kuinua kombe hilo," alisema Onuoha.
Aliongeza kuwa Arsenal ina nafasi ya kutwaa Ligi ya Mabingwa kutokana na ilivyoonyesha katika misimu miwili iliyopita, lakini uwepo wa Odegaard akiwa katika kiwango bora unaifanya timu hiyo kuwa tishio zaidi.
"Unapokuwa katika kiwango chako bora, timu nayo huwa bora. Toleo bora la Arsenal linatokea Odegaard anapokuwa anasimamia mchezo, kwa sababu wachezaji wengi zaidi hushiriki katika namna wanavyoshambulia," alisema.
Kocha Arteta pia amesisitiza umuhimu wa Odegaard kuwa na ujasiri wa kuamua michezo.
"Hiki ndicho tunachohitaji; wachezaji wenye mtazamo wa kuamua mchezo, kucheza kwa kujiamini na kuendelea kuchukua hatari. Anaingia katika maeneo hayo mara nyingi zaidi katika michezo ya hivi karibuni. Lilikuwa bao la ajabu," alisema Arteta.
Dhidi ya Napoli, Odegaard hakuishia kufunga bao la ushindi pekee, bali pia aliongoza timu kwa juhudi zake uwanjani, akionyesha ubora wa kiuongozi sambamba na kuwa mchezaji aliyeamua matokeo.
Onuoha alisema Odegaard amekuwa sehemu muhimu ya mwanzo mzuri wa Arsenal msimu huu, akimsifu kwa ubunifu wake, hasa upande wa kulia, uwezo wa kulinda mpira na kutafuta pasi za kutengeneza nafasi za mabao, huku pia akitimiza majukumu ya ulinzi.
Odegaard alifanikiwa kufanya kile ambacho baadhi ya wachezaji wenzake walishindwa, baada ya Arsenal kupoteza nafasi kadhaa za wazi kabla ya yeye kuamua mchezo.
Ubora wa Arsenal ulionekana pia katika idadi ya mashuti 26 waliyopiga, ikiwa ni mara ya kwanza tangu takwimu hizo kuanza kutunzwa msimu wa 2003/04 kwa timu hiyo kufikisha idadi hiyo katika mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa. Pia ilikuwa idadi kubwa zaidi ya mashuti ambayo Napoli imewahi kuruhusu katika kipindi hicho.
"Martin anachangia kwa mabao ambayo yanaamua matokeo, na hicho ndicho tunachotaka kutoka kwa wachezaji wetu wa kushambulia; wawe na uwezo wa kuamua," alisema Arteta.
Ligi ya Mabingwa imekuwa taji ambalo Arsenal imeshindwa kulifikia, baada ya kupoteza fainali dhidi ya Barcelona mwaka 2006 na Paris Saint-Germain msimu uliopita.
Hata hivyo, ikiwa Odegaard ataendelea na kiwango hiki bora, matumaini ya Arsenal kuvuka kikwazo hicho na hatimaye kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa yataongezeka kwa kiasi kikubwa.