Mahakama yamkomalia Hakimi
Muktasari:
- Mahakama ya juu zaidi ya Ufaransa, Court of Cassation, imekataa rufaa ya Hakimi, 27, aliyekuwa akipinga uamuzi wa mahakama ya rufaa wa kumfikisha katika Mahakama ya Jinai ya Hauts-de-Seine kujibu tuhuma hizo.
PARIS, UFARANSA: BEKI wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Morocco, Achraf Hakimi, ameshindwa katika hatua yake ya mwisho ya kisheria dhidi ya uamuzi wa kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma za kumbaka mwanamke mwaka 2023.
Mahakama ya juu zaidi ya Ufaransa, Court of Cassation, imekataa rufaa ya Hakimi, 27, aliyekuwa akipinga uamuzi wa mahakama ya rufaa wa kumfikisha katika Mahakama ya Jinai ya Hauts-de-Seine kujibu tuhuma hizo.
Uamuzi huo wa mwisho unamaanisha kuwa Hakimi sasa atasubiri kesi yake kusikilizwa katika mahakama ya jinai, baada ya awali kuamriwa kufikishwa mahakamani Februari mwaka huu.
Hakimi amekanusha tuhuma hizo tangu zilipoibuka na amesisitiza kuwa hana hatia.
Wakili wake, Fanny Colin, aliiambia AFP kuwa tuhuma dhidi ya mteja wake “hazijachunguzwa” na Mahakama ya Cassation, akieleza kuwa ushahidi wa upande wa utetezi utawasilishwa hadharani wakati wa kesi.
Colin pia amesema Hakimi, ambaye “hana cha kuficha”, ameshirikiana kikamilifu na polisi pamoja na mamlaka za mahakama tangu uchunguzi ulipoanza na ataendelea kufanya hivyo wakati wa kesi.
Kwa upande mwingine, wakili wa mwanamke aliyefungua malalamiko, Rachel-Flore Pardo, amesema uamuzi wa kumfikisha Hakimi mahakamani unaonyesha uzito wa hoja zilizotolewa na mahakama ya rufaa.
Pardo amesema mteja wake amedhamiria kupata haki baada ya mchakato wa kisheria uliodumu kwa miaka kadhaa.
Tukio hilo liliripotiwa Februari 2023, wakati mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 24 alipokwenda polisi katika eneo la Val-de-Marne, kusini-mashariki mwa Paris, na kudai kuwa Hakimi alimbaka.
Kwa mujibu wa chanzo cha polisi kilichonukuliwa wakati huo, mwanamke huyo amesema alikutana na Hakimi kupitia Instagram Januari 2023, kabla ya kwenda nyumbani kwake kwa teksi iliyoagizwa na mchezaji huyo.
Alidai kuwa alipofika nyumbani kwa Hakimi, mchezaji huyo alimbusu na kumshika bila ridhaa yake kabla ya kumbaka.
Mwanamke huyo alidai alifanikiwa kumsukuma Hakimi na kumtumia ujumbe rafiki yake, ambaye baadaye alifika kumchukua.
Siku chache baadaye, Hakimi alishtakiwa kwa tuhuma za ubakaji.
Kesi hiyo sasa itaendelea katika mahakama ya jinai, ambako ushahidi wa pande zote mbili utawasilishwa na kuchunguzwa kabla ya uamuzi wa mwisho kutolewa.