Nigeria yatwaa ubingwa wa dunia U-17
Muktasari:
- Bao la Oluebube Umejiaku katika kipindi cha pili liliamua mchezo huo wa fainali na kuipa Nigeria ushindi dhidi ya Japan, katika pambano lililochezwa jijini Rabat, Morocco.
NIGERIA imeandika historia mpya katika soka la wanawake baada ya kuitandika Japan kwa mabao 2-1 na kutwaa taji la Kombe la Dunia la Wanawake kwa vijana chini ya miaka 17 kwa mara ya kwanza, huku ikiwa nchi ya kwanza ya Afrika kufanikisha hilo.
Bao la Oluebube Umejiaku katika kipindi cha pili liliamua mchezo huo wa fainali na kuipa Nigeria ushindi dhidi ya Japan, katika pambano lililochezwa jijini Rabat, Morocco.
Nigeria ilianza mchezo kwa kasi, ikitengeneza nafasi kadhaa kupitia Awawu Bashiru na Umejiaku, ambao walikaribia kufunga mabao lakini mashuti yao hayakulenga langoni.
Umejiaku aliendelea kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Japan, akipiga kichwa kilichogonga mwamba wa juu wa lango baada ya kipa Kou Kadowaki kushindwa kudhibiti mpira uliopigwa kwenye eneo la hatari.
Nigeria ilipata bao la kwanza kupitia Bashiru dakika ya 39, ambaye alituma mpira uliokuwa ukishuka kuelekea langoni, lakini Kadowaki alishindwa kuudhibiti na kuuruhusu kuingia wavuni.
Baadaye Nigeria iliongeza bao la pili kupitia Umejiaku aliyepokea pasi ndefu ya Esther Stephen, akautuliza mpira kwa mguu wa kushoto kabla ya kumpiga chenga ya juu kipa Kadowaki na kuandika bao lililozidi kuiweka timu hiyo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Japan ilijaribu kurejea mchezoni, lakini ilipata bao lake la kwanza dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika, kupitia Fuki Ito aliyefunga kwa shuti la kwanza baada ya Anri Ito kuurudisha mpira kwa kichwa kutoka kwenye kona.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Umejiaku amesema kile walichokionyesha kwenye fainali hiyo ni maelekezo ya makocha yaliyowasaidia wachezaji kupambana hadi mwisho.
"Ninajisikia vizuri na nina furaha sana. Namshukuru Mungu kwa kila kitu. Ilikuwa mechi ngumu kwetu, lakini maelekezo ya makocha yalitufanya tuinue vichwa vyetu na kukabiliana na kila hali. Tulihitaji kujipa moyo na kutiana nguvu ndani ya uwanja," amesema Umejiaku.
Kwa upande wake, kocha wa Japan, Sadayoshi Shirai, alikiri Nigeria ilikuwa timu yenye nguvu, hasa katika kasi na uwezo wa kutumia nguvu za mwili.
Amesema wachezaji wake walipambana hadi dakika za mwisho licha ya changamoto walizokutana nazo, akiwataka kujivunia safari yao katika mashindano hayo.
"Awali ya yote, lazima niseme Nigeria ilikuwa timu imara sana. Tulielewa uwezo wao, lakini kulikuwa na nyakati walifanikiwa kupenya nyuma ya safu yetu ya ulinzi.
"Hata hivyo, naamini wachezaji wetu walipambana sana hadi mwisho. Nataka wajivunie walichokifanya kwa sababu namna walivyopambana katika Kombe hili la Dunia imeweza kuwatia moyo watu wengi," amesema Shirai.
Safari ya Nigeria hadi kufika fainali haikuwa nyepesi, kwani ilianza kwa kupoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi kwa mabao 2-1 dhidi ya Poland, kabla ya kuifunga Puerto Rico 2-0 na mabingwa watetezi Korea Kaskazini mabao 3-1. Katika hatua ya 16 bora iliiondoa Mexico kwa ushindi wa 2-1, kisha ikavuka robo fainali kwa kuichapa Venezuela bao 1-0 kupitia penalti ya dakika za mwisho.
Katika nusu fainali, Nigeria iliandika historia nyingine baada ya kuifunga Brazil mabao 3-1 na kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kufika fainali ya mashindano hayo, safari iliyofikia kilele kwa kutwaa ubingwa baada ya kuishinda Japan mabao 2-1.