Nigeria yapata pigo, kabla ya kuivaa Msumbiji
Muktasari:
- Nigeria ikipenya, robo fainali itamva mshindi kati ya Algeria au DR Congo.
NDOTO ya Nigeria ya kutwaa taji la nne la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) imepata pigo baada ya Cyriel Dessers na Ryan Alebiosu kuumia.
Alebiosu, beki wa Blackburn Rovers aliyecheza mechi yake ya kwanza akiwa na timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles dhidi ya Uganda na kuonyesha kiwango kizuri, akicheza dakika zote 90 akichukua nafasi ya Bright Osayi-Samuel, huku Nigeria ikipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya The Cranes.
Hata hivyo, licha ya uchezaji wake mzuri, alipata jeraha la kuchanika mguuni na kulazimika kuwahishwa hospitalini. Hali yake ya kushiriki mechi zilizobaki za mashindano bado haijulikani, wakati kikosi cha Eric Chelle kikijiandaa kukabiliana na Msumbiji katika hatua ya 16 Bora wikiendi hii.
Kwa upande mwingine nyota wa Panathinaikos, Cyriel Dessers naye pia yuko shakani kutokana na jeraha la paja. Anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi (scan) ili kubaini uzito wa jeraha hilo na kama ataweza kuendelea na mashindano.
“Ni vigumu kucheza. Huu ni mchezo wake wa kwanza barani Afrika, kwenye AFCON. Nimefurahishwa na alichokifanya, lakini nina wasiwasi kidogo kwa sababu ana jeraha,” amesema Chelle na kuongeza;
“Walipofunga bao, alipata jeraha kubwa sijui neno sahihi kwa Kiingereza, lakini alilazimika kwenda hospitalini. Mguu wake ulikuwa umechanika. Nimefurahishwa na uchezaji wake leo (jana) na kwa sasa nina machaguo mengi.”
Nigeria ikipenya, robo fainali itamva mshindi kati ya Algeria au DR Congo.