Nigeria, Ghana zalambwa kufuzu AFCON 2027
Muktasari:
- Nigeria ilikubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Guinea-Bissau, huku Ghana ikipoteza kwa mabao 4-2 dhidi ya Gambia.
ACCRA, GHANA: MABINGWA wa zamani Nigeria na Ghana zimeanza vibaya raundi ya pili ya mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 baada ya kupokea vipigo.
Nigeria ilikubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Guinea-Bissau, huku Ghana ikipoteza kwa mabao 4-2 dhidi ya Gambia.
Wenyeji Guinea-Bissau walianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 15 kupitia Franculino, kabla ya Mahamadou Balde kuongeza la pili dakika ya 66.
Alvaro Djalo alifunga bao la tatu katika muda wa nyongeza na kuhitimisha ushindi huo mkubwa wa wenyeji.
Licha ya kipigo hicho, Nigeria imebaki katika nafasi ya pili kwenye Kundi L ikiwa na pointi tatu, wakati Guinea-Bissau ikiongoza ikiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zake mbili.
Tanzania na Madagascar, ambazo zilitoka sare ya bao 1-1 Jumanne, zinashika nafasi ya tatu na nne mtawalia, kila moja ikiwa na pointi moja.
Katika Kundi C, Gambia ilifanya come back ya kuvutia baada ya kuifunga Ghana mabao 4-2 katika mchezo uliochezwa nchini Ghana.
Ghana ilianza kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya 27 baada ya Ernest Nuamah kufunga kwa mkwaju wa penalti.
Felix Afena-Gyan akaongeza la pili dakika sita baadaye, na kuwapa wenyeji matumaini ya kupata ushindi wao wa kwanza.
Hata hivyo, Gambia ilianza kurejea mchezoni dakika ya 37 baada ya Mohamed Badamosi kufunga penalti na kupunguza pengo.
Omar Colley akaisawazishia Gambia dakika tatu kabla ya mapumziko, kabla ya Ebrima Colley kufunga mabao mawili kipindi cha pili na kuikamilishia timu yake ushindi wa 4-2.
Ushindi huo umeifanya Gambia kuongoza Kundi C ikiwa na pointi sita, huku Ivory Coast ikiwa ya pili kwa pointi sita.
Ivory Coast ilichapa Somalia kwa mabao 2-0.
Timu mbili zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu katika kila kundi zitafuzu kwa Fainali za AFCON 2027, zitakazofanyika kwa pamoja Kenya, Tanzania na Uganda kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.