Neymar agusia kustaafu soka
Muktasari:
- Nyota huyo wa Brazil amekumbwa na majeraha ya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni na amekiri kuwa kwa sasa anaishi “mwaka hadi mwaka” katika hatua hii ya taaluma yake ya mchezo wa soka.
RIO DE JANEIRO, BRAZIL: SUPASTAA, Neymar ameashiria kuwa anaweza kustaafu soka ndani ya miezi michache ijayo.
Nyota huyo wa Brazil amekumbwa na majeraha ya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni na amekiri kuwa kwa sasa anaishi “mwaka hadi mwaka” katika hatua hii ya taaluma yake ya mchezo wa soka.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona na Paris Saint-Germain, mwenye miaka 34, kwa sasa amerejea katika klabu yake ya utotoni ya Santos baada ya kuondoka katika kipindi kilichojaa majeraha nchini Saudi Arabia.
Uhamisho wake wa Pauni 198 milioni alipotoka Barcelona kwenda kujiunga na PSG bado hadi leo ndio ada kubwa zaidi kuwahi kulipwa kwa mchezaji katika uhamisho mmoja.
Kombe la Dunia 2026 linakaribia huku Brazil ikitarajiwa kukutana na Scotland katika hatua ya makundi pamoja na Morocco na Haiti. Neymar anatumaini kung’ara katika jukwaa hilo kubwa zaidi ambalo linaweza kuwa tamati ya safari yake ya kipekee ikiwa kocha Carlo Ancelotti atamchagua na kumjumuisha kwenye kikosi chake.
Akizungumza na CazeTV nchini kwao kuhusu mustakabali wake, Neymar alisema: "Sijui nini kitatokea kuanzia sasa. Huenda ikafika Desemba nikataka kustaafu. Ninaishi mwaka hadi mwaka. Kuna mwaka huu, ambao ni muhimu sana si tu kwa Santos, bali pia kwa timu ya taifa ya Brazil na kwangu mimi pia.”
Majeraha yamekuwa changamoto kubwa kwa Neymar tangu alipoingia katika umri wa miaka 30, akiwa nje kwa vipindi virefu. Anajua kwamba atahitaji kurejea katika kiwango cha asilimia 100 ya utimamu wa mwili ikiwa anataka kutimiza ndoto yake ya kucheza Kombe la Dunia 2026, fainali zitakazofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico majira yajayo ya kiangazi.
Sasa amerejea kutoka kwenye jeraha lake la hivi karibuni na ameeleza hali yake ya sasa, aliposema: “Niliweza kurejea vizuri sana katika mchezo wangu wa mwisho. Nina furaha na nimetulia kwa kurejea nikiwa bora kidogo kuliko nilivyokuwa hapo awali. Kwa hakika, ninahitaji kuongeza kasi na mwendo wa mchezo kidogo zaidi, lakini kwa uvumilivu nitafikia asilimia 100 yangu.”