Endrick: Naweza kuondoka Januari
Muktasari:
- Nyota huyo wa Brazil aliingia akitokea benchi na kusaidia Madrid kufanya mabadiliko makubwa ya matokeo baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-1. Kichwa chake kilizaa nafasi iliyomruhusu Carlos Espí kufunga bao muhimu, kabla ya Endrick kusawazisha kwa kichwa akitumia kona ya Arda Güler. Antonio Rüdiger alifunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza.
MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Endrick, amesema yuko tayari kuondoka klabuni hapo katika dirisha dogo la usajili la Januari ikiwa italazimu, licha ya kuonyesha kiwango bora katika ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Roma.
Nyota huyo wa Brazil aliingia akitokea benchi na kusaidia Madrid kufanya mabadiliko makubwa ya matokeo baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-1. Kichwa chake kilizaa nafasi iliyomruhusu Carlos Espí kufunga bao muhimu, kabla ya Endrick kusawazisha kwa kichwa akitumia kona ya Arda Güler. Antonio Rüdiger alifunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza.
Endrick alisema anachukulia mambo siku moja baada ya nyingine, akisisitiza kuwa yuko tayari kufuata yatakayojiri kuhusu maisha yake ya soka.
“Nikitakiwa kuondoka Januari, nitaondoka; nikitakiwa kubaki, nitabaki. Nitafanya kile ambacho Mungu ataweka moyoni mwangu,” alisema.
Mshambuliaji huyo pia alimshukuru kocha José Mourinho kwa kumwamini na kuzungumza naye kwa uwazi. Alisema licha ya kuthamini msaada wa kocha huyo, jukumu lake kubwa ni kupigania mafanikio ya Real Madrid.
Endrick, aliyerejea baada ya kipindi cha mkopo katika klabu ya Lyon ya Ufaransa, amekuwa na nafasi ndogo ya kucheza msimu huu, hali iliyochochea uvumi kuhusu uwezekano wa kuondoka. Mkataba wake na Madrid unatarajiwa kumalizika Juni 2030, huku AC Milan na Roma zikitajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazomfuatilia.
BENJAMIN PAVARD
INTER imeingiza Euro milioni 8.897 kutokana na bonasi na asilimia za mauzo ya wachezaji waliotoka klabuni hapo. Mapato hayo yanahusisha Marcelo Brozovic, Benjamin Pavard, Lucien Agoume, Vagiannidis na Michele Di Gregorio. Taarifa za fedha zinaonyesha kiasi hicho kimechangia mapato ya klabu, yaliyovuka zaidi ya euro milioni 500 msimu wa 2025/26.
RIYAD MAHREZ
AL-SHAMAL ya Qatar imetangaza kumsajili winga wa Algeria, Riyad Mahrez, aliyekuwa Al-Ahli Saudi. Mahrez amejiunga bure baada ya mkataba wake kuvunjwa mwishoni mwa msimu uliopita. Al-Shamal ni klabu ya tano katika maisha yake ya soka, baada ya Le Havre, Leicester City, Manchester City na Al-Ahli, akiwa na mataji mengi makubwa.
JADON SANCHO
GETAFE ya Hispania inachunguza uwezekano wa kumsajili Jadon Sancho, aliyemaliza maisha yake Manchester United. Kocha Jose Bordalas anavutiwa na uwezo wa winga huyo, lakini mshahara anaoutaka wa euro milioni nne ni kikwazo. Getafe inatafuta suluhisho, ikiwamo bonasi za kiwango cha mchezo au mkataba mfupi unaokubalika kwa pande zote kwa sasa.
DION BELJO
MANCHESTER United, Tottenham na Everton zinafuatilia mshambuliaji wa Dinamo Zagreb, Dion Beljo, kabla ya dirisha la Januari. Mshambuliaji huyo wa Croatia amefunga mabao 12 katika mechi 14 zilizopita, yakiwamo 10 kwenye mechi saba za ligi. Brentford, Chelsea na City Football Group pia zinatajwa kumfuatilia kuelekea dirisha la Januari ujao hivi.
EMIL AUDERO
JUVENTUS ilimfikiria kipa Emil Audero wakati wa dirisha la usajili la majira ya joto, lakini dili halikukamilika kwa sababu mbalimbali. Audero alisema alikuwa akisubiri chaguo huku akiendelea na mazoezi. Kipa huyo alilinganisha Juventus ya 2016/17 na Inter ya 2023/24, akisema Juve ilikuwa bora kibinafsi, lakini Inter kama timu kwa ujumla.
ALEX SCOTT
BOURNEMOUTH iko tayari kumuuza kiungo Alex Scott Januari, lakini inataka pauni milioni 100 na haitaki kupunguza nguvu ya kikosi ikiwa itakuwa kwenye vita ya kushuka daraja. Chelsea na Liverpool zinaongoza mbio za kumsajili. Chelsea iliwahi kutoa Pauni milioni 60, lakini ofa hiyo ilikataliwa. Scott kwa sasa anauguza jeraha la paja.
PAUL POGBA
PAUL Pogba anaweza kuhamia Ligi ya Marekani, MLS, baada ya kuachana na Monaco msimu huu. Ripoti zinasema amependekezwa kwa klabu kadhaa, zikiwamo DC United, Inter Miami ya Lionel Messi na New York City. Hakuna mazungumzo rasmi yaliyoanza, huku kiungo huyo akitafuta klabu itakayomsaidia kurejea uwanjani baada ya misukosuko ya soka.
ERLING HAALAND
REAL Madrid inaendelea kufuatilia hali ya mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, ikisubiri nafasi ya kumsajili. Ripoti zinasema klabu hiyo ina uhusiano na familia pamoja na mawakala wa Mnorway huyo. Madrid pia inafuatilia kesi ya City kuhusu madai ya kuvunja kanuni za fedha za Ligi Kuu England na kuchukua hatua.
JJ GABRIEL
REAL Madrid inaongoza mbio za kumsajili kinda wa Manchester United, JJ Gabriel, mwenye miaka 16, baada ya kuomba kusitisha usajili wake. Mshambuliaji huyo amekasirishwa na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza. PSG, Bayern Munich na Barcelona pia zimewasiliana na wawakilishi wake, huku Madrid ikiamini inaweza kumshawishi kuhamia Hispania hivi karibuni.