Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tyson kizimbani kisa njiwa anayezungumza

TYSON Pict

Muktasari:

  • Tyson anatuhumiwa kukiuka mkataba wa udhamini aliotia saini Januari 2024 na kampuni ya Medier Ltd, iliyopanga kumtumia kutangaza jukwaa la kamari la mtandaoni la Rabona.

LONDON, ENGLAND: BONDIA maarufu wa uzito wa juu, Mike Tyson, anakabiliwa na mgogoro wa kisheria wa pauni1.5 milioni (zaidi ya Sh5 bilioni) baada ya kudaiwa kukataa kushiriki katika tangazo lililopangwa kumwonyesha akizungumza na njiwa mkubwa anayeweza kuzungumza.

Tyson anatuhumiwa kukiuka mkataba wa udhamini aliotia saini Januari 2024 na kampuni ya Medier Ltd, iliyopanga kumtumia kutangaza jukwaa la kamari la mtandaoni la Rabona.

Kwa mujibu wa mpango huo, bondia huyo alitakiwa kufanya mahojiano kwa njia ya video na mtangazaji aliyevalia vazi la njiwa mkubwa, kabla ya kumfundisha ndege huyo mchezo wa ngumi.

Hata hivyo, waandaaji wa kampeni hiyo wanadai Tyson alijiondoa baada ya kukubali pambano la maonyesho lililomuingizia dola 15 milioni dhidi ya nyota wa YouTube aliyegeukia ndondi, Jake Paul.

TY 01

Wakili wa Medier, Ali Reza Sinai, ameiambia Mahakama Kuu ya London kuwa Tyson na kampuni yake ya matangazo, Tyrannic, ambayo inadhibitiwa na mkewe, Lakiha Tyson, walipoteza hamu ya kutekeleza mkataba huo baada ya pambano dhidi ya Paul kupangwa.

Kwa upande mwingine, Tyson na kampuni yake wanakanusha tuhuma za kuvunja mkataba, wakidai Medier ndiyo iliyokiuka makubaliano kwanza kwa kumtaka bondia huyo kushiriki kipindi cha burudani kilichoitwa Talking Pigeons.

Kipindi hicho kilipangwa kuwashirikisha watangazaji wanne, mmoja wao akiwa amevalia vazi la njiwa mkubwa. Tyson alitakiwa kuzungumza kwa kufuata maandishi maalumu, kusimulia kumbukumbu za utotoni na kuwafundisha watangazaji hao ndondi kwa kutumia sanamu iliyokuwa na sura ya mpinzani wake wa zamani, Evander Holyfield.

Katika mpango huo, watangazaji wangetumia sanamu hiyo kufanya mazoezi ya kupiga ngumi, kabla ya Tyson kucheza michezo ya kasino kwenye tovuti ya Rabona huku akiendelea kuwasiliana nao kwa njia ya video.

TY 02

Wakili wa Tyson, Amanda Hadkiss, amedai mahakamani kuwa matakwa hayo yalizidi kwa kiasi kikubwa kile ambacho mteja wake alipaswa kufanya chini ya mkataba.

Amesema makubaliano yalihusu kurekodiwa kwa Tyson akicheza michezo ya kasino, ikiwamo mashine za kupangwa matokeo (slots), poka na roulette, au michezo mingine iliyoidhinishwa na kampuni kupitia tovuti yake.

Mahakama imeelezwa kuwa mkataba huo ulihusisha malipo ya jumla ya dola milioni mbili kwa Tyson kupitia kampuni yake ya Tyrannic, yaliyopaswa kulipwa kwa awamu. Kabla ya pande hizo kutengana, Tyson alikuwa tayari amelipwa karibu dola 190,000.

Sinai amedai Tyson na kampuni yake walishindwa kutekeleza matangazo ya moja kwa moja kwa njia ya mtandao kama walivyokubaliana, huku wakikatisha mkataba bila kutoa taarifa inayotakiwa.

Akizungumzia pambano la Tyson dhidi ya Paul, wakili huyo amesema makubaliano ya bondia huyo na mtandao wa Netflix yalikuwa jambo muhimu katika mgogoro huo, akidai Tyson alipoteza hamu ya kuendelea na mkataba wa Rabona.

TY 03

Mahakama imeelezwa kuwa pambano hilo lilipangwa awali kufanyika Julai 20, 2024, lakini likafanyika Novemba mwaka huo, Tyson akipoteza dhidi ya Paul.

Kwa mujibu wa Sinai, Tyson alitarajiwa kuhudhuria mkutano mkubwa wa kampuni za kamari mjini Amsterdam, Uholanzi, kuanzia Julai 16 hadi 19, 2024. Hata hivyo, alidai Tyson na Tyrannic walihofia kushiriki katika shughuli hiyo kungeweza kukinzana na masharti ya mkataba wake wa Netflix na kuathiri mikataba mingine ya udhamini kabla ya pambano dhidi ya Paul.

“Utekelezaji wa mkataba wa huduma ulikuwa usumbufu kwa Tyrannic na Tyson,” amesema Sinai.

Hata hivyo, upande wa Tyson umesisitiza kuwa wajibu wake wa kimkataba ulikuwa kutangaza michezo ya kasino na si kushiriki katika kipindi cha burudani kilichohitaji maigizo na mazungumzo yaliyopangwa mapema.

Mgogoro huo sasa unaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya London, huku pande hizo mbili zikitofautiana kuhusu tafsiri ya masharti ya mkataba na wajibu wa Tyson katika kampeni hiyo.