Newcastle yakubali yaishe, yamgeukia Nicolas Jackson
Muktasari:
- Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya klabu hiyo, Jackson ameibuka kuwa chaguo la haraka kutokana na sifa zake za kiuchezaji na uzoefu alionao wa muda mfupi katika Ligi Kuu England.
MABOSI wa Newcastle United imepanga kumgeukia mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Senegal, Nicolas Jackson, mwenye umri wa miaka 24, baada ya kuona Manchester United ina nafasi kubwa zaidi ya kushinda vita ya kumsajili straika wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, 21, katika dirisha hili.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya klabu hiyo, Jackson ameibuka kuwa chaguo la haraka kutokana na sifa zake za kiuchezaji na uzoefu alionao wa muda mfupi katika Ligi Kuu England.
Newcastle United inapanga kufanya mabadiliko makubwa kwenye safu ya ushambuliaji kwa ajili ya kuziba pengo la Alexander Isak ambaye anaweza kutua Liverpool wakati wowote kutokana na majadiliano yanayoendelea
Katika msimu msimu uliopita, Jackson alicheza mechi 44 kwenye mashindano yote Ulaya na baadhi ya mechi za Klabu Bingwa ya Dunia nchini Marekani akiwa na Chelsea na kufunga mabao 17 pamoja na kutoa pasi tano za mabao.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2033, lakini Chelsea inadaiwa kuwa tayari kumuuza ikiwa itapokea ofa inayoanzia Pauni 55 milioni ili ianze maisha bila huduma ya mchezaji huyo.
Jackson alijiunga na Chelsea akitokea Villarreal 2023 kwa dau la Pauni 32 milioni ambapo alisaini mkataba wa miaka minane kuichezea timu hiyo. Chelsea inatajwa kulazimika kumuuza ili kuweka sawa vitabu vya masuala ya matumizi ya kifedha.
Rafael Leao
TOTTENHAM Hotspur imemuongeza winga wa AC Mian na timu ya taifa ya Ureno, Rafael Leao, 26, katika orodha ya wachezaji ambao inataka kuwasajili dirisha hili ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji. Mbali ya Leao, Spurs pia ilikuwa inahusishwa na staa wa Real Madrid, Rodrygo, 24. Mkataba wa wa Leao unatarajiwa kumalizika 2028 sawa na ule wa Rodrygo.
Bobby Clark
KKIUNGO wa Liverpool, Bobby Clark, 20, yupo mbioni kujiunga na Derby County kwa mkopo wa msimu mzima. Clark alionyesha uwezo mkubwa kwenye timu ya vijana ya Liverpool chini ya miaka 21 na pia alicheza mechi sita za kikosi cha wakubwa. Liverpool imekubali kumtoa kwa mkopo ili apate nafasi ya kucheza mara kwa mara. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani.
Mads Bidstrup
KIUNGO wa kimataifa wa Denmark, Mads Bidstrup, 24, ambaye alicheza mechi 30 akiwa na RB Salzburg msimu uliopita anatajwa kuwa katika rada za Nottingham Forest kwenye dirisha hili. Bidstrup ana mkataba hadi Juni 2026 na amekuwa akizivutia timu mbalimbali za EPL kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupokonya mipira.
Brandon Williams
BEKI wa zamani wa Manchester United, Brandon Williams, 24, ambaye kwa sasa yupo huru hana klabu tangu aachwe msimu wa 2023/24. Hull City na Stoke City zimeonyesha nia ya kumchukua, huku zikiamini anaweza kurejea katika kiwango bora baada ya majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu. Msimu wa mwisho alicheza mechi 17 za michuano yote.
Douglas Luiz
NOTTINGHAM Forest imepanga kuwasiliana na wakala wa kiungo wa Juventus, Douglas Luiz, 27, ambaye anahusishwa kutaka kurejea England ambako timu kibao zinahitaji huduma yake. Luiz ambaye alijiunga na Juventus kwa dau la Pauni 42 milioni, anahusishwa na Manchester United pamoja na Everton. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029. Msimu uliopita alicheza mechi 27 za michuano yote.
Malick Thiaw
NEWCASTLE United inamtazama beki wa kati wa AC Milan, Malick Thiaw, 23, na tayari imeshatuma wawakilishi kwenda Italia kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Milan juu ya nyota huo wa kimataifa wa Ufaransa. Thiaw ana mkataba na Milan hadi 2027, lakini Newcastle iko tayari kutoa hadi Pauni 35 milioni kama ada ya uhamusho ili kumpata.
Giovanni Leoni
LIVEPROOL imemuweka katika rada beki wa kati wa Parma, Giovanni Leoni, 18, ambaye aling’ara katika Ligi Daraja la Kwanza akiwa na timu hiyo msimu uliopita. Leoni ambaye ni sehemu ya kikosi cha Italia cha wachezaji wenye umri chini ya miaka 21, mkataba wake na Parma unamalizika 2027. Parma inahitaji Pauni 30 milioni ili kumuuza Leon alicheza mechi 32 msimu uliopita.