Neville ataka kipa mpya Man United
Muktasari:
- Beki huyo wa zamani wa Man United na England, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka kwenye kituo cha Sky Sports, Neville alishinda mataji manane ya Ligi Kuu England alipokuwa Old Trafford chini ya Sir Alex Ferguson.
LONDON, ENGLAND: GARY Neville amesema anaamini Manchester United ina ulazima wa kusajili kipa mpya kama inataka kumaliza ndani ya Top Six kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Beki huyo wa zamani wa Man United na England, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka kwenye kituo cha Sky Sports, Neville alishinda mataji manane ya Ligi Kuu England alipokuwa Old Trafford chini ya Sir Alex Ferguson.
Lakini, Neville, 50, ameweka wasiwasi uwezekano wa Man United kuwa vinara kwenye ligi msimu huu, huku akibainisha kwamba hata nafasi ya kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao itakuwa ngumu kwao kama kocha Ruben Amorim hatasajili kipa mpya kwenye dirisha hili.
Neville alisema: “Kwa United, kumaliza ndani ya nafasi sita za juu itakuwa afya kwao.
“Tumeshaondoka kwenye kusema kwamba Man United inapaswa kushinda ubingwa wa ligi. Huo sio uhalisia kwa sasa. Ninachokifikiria kwa sasa, wanaweza kumaliza namba saba, nane huko ndiko wanakoonekana.
“Lakini, bila ya kucheza soka la Ulaya, wanaweza kumaliza kwenye sita bora kama watakuwa vizuri, kama watapata kipa mpya.”
Man United imekuwa ikihusishwa na kipa wa PSG, Gianluigi Donnarumma, ambaye ataachana na mabingwa hao wa Ulaya, huku miamba hiyo ya Old Trafford ikiwa imetumia karibu Pauni 200 milioni kunasa saini za washambuliaji Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko.
Washambuliaji hao wote watatu wana uhakika wa kuanza kwenye kikosi cha Man United katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal, Jumapili hii. Wakati Man United ikifanya maboresho makubwa kwenye safu ya ushambuliaji baada ya msimu uliopita kufunga mabao 40 tu, lakini shida ya Neville ipo golini, kipa Andre Onana alikuwa na makosa mengi yaliyogharimu kikosi hicho cha Old Trafford kwenye mechi zao za msimu uliopita.