Napoli kutua Old Trafford kwenda kumng'oa straika Hojlund
Muktasari:
- Napoli imepanga kuvamia Man United kumnasa straika huyo endapo kama klabu hiyo ya Old Trafford itaingia kwenye mkwamo wa kifedha na kulazimika kuuza mastaa wake ili kujiokoa.
MIAMBA ya soka ya Italia, Napoli imeripotiwa kujiandaa kwa ajili ya kwenda kupeleka ofa huko Manchester United ili kunasa saini ya straika Rasmus Hojlund kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Napoli imepanga kuvamia Man United kumnasa straika huyo endapo kama klabu hiyo ya Old Trafford itaingia kwenye mkwamo wa kifedha na kulazimika kuuza mastaa wake ili kujiokoa.
Hojlund, 22, alijiunga na Man United kwa ada ya Pauni 72 milioni akitokea Atalanta ya Italia. Kwa maana hiyo, Napoli inataka kumrudisha mkali huyo kwenye kukipiga katika mikikimikiki ya Serie A, mahali ambako alikuwa matata uwanjani na kuwavutia wababe hao wa Old Trafford kwenda kunasa saini yake. Hojlund anakosolewa huko Man United kutokana na kiwango chake kuwa duni na sasa huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea kwa kupigwa bei kutokana na ugumu wa kiuchumi unaoikabili Man United kwa sasa.
Tino Livramento
MANCHESTER City imeripotiwa kuwa kwenye mpango madhubuti wa kunasa saini ya beki wa kulia wa Newcastle United, Tino Livramento, 22, kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Man City ipo kwenye mchakato wa kujenga kikosi, ambapo miamba hiyo ya Etihad imekuwa ikimfukuzia pia beki wa kushoto, Mtaliano Andrea Cambiaso, 25, ili anase saini yake kwenye usajili wa majira ya kiangazi kuifanya timu yao kuwa na kikosi cha kiushindani ndani ya uwanja.
Frenkie de Jong
ARSENAL imeripotiwa kuwa siriazi kwenye mpango wao wa kunasa huduma ya kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong ili kwenda kuboresha kikosi chao cha Emirates kwa ajili ya msimu ujao. Kinachoripotiwa ni kwamba Arsenal ipo tayari kuipa Barcelona ofa ya Euro 75 milioni kwa ajili ya kunasa saini ya kiungo huyo wa Kidachi ili kwenda kuimarisha timu yao kwenye sehemu ya katikati ya uwanja kuwa na nguvu kubwa ya kufukuzia ubingwa msimu ujao.
Mateo Kovacic
ATLETICO Madrid imeripotiwa kuonyesha thamani ya dhati ya kwenda kunasa saini ya kiungo wa Manchester City, Mateo Kovacic kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Staa huyo wa Croatia, mwenye umri wa 30, ambaye aliwahi kuitumikia pia Chelsea, anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji ambao Man City itafikiria kuachana nao wakati dirisha lijalo la usajili litakapofunguliwa kutokana na miamba hiyo ya Etihad kuwa na mpango wa kuleta nyota wapya kikosini.
Yves Bissouma
TOTTENHAM Hotspur imeripotiwa kuwa na mpango wa kumwondoa kwenye kikosi chao kiungo wa Mali, Yves Bissouma, wakati wa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa. Staa huyo mwenye umri wa miaka 28 amekuwa kwenye kiwango bora tangu alipojiunga na Spurs, lakini sasa miamba hiyo ya London inapiga hesabu za kuachana naye wakati dirisha lijalo la usajili litakapofunguliwa mwishoni mwa msimu huu katika kipindi cha majira ya kiangazi huko Ulaya.
Samu Aghehowa
ASTON Villa imeripotiwa kujiandaa na vita kali dhidi ya timu nyingine za Ligi Kuu England, Arsenal, Chelsea na West Ham United katika mchakamchaka wa kufukuzia huduma ya mshambuliaji wa FC Porto, Samu Aghehowa. Fowadi huyo Mhispaniola mwenye umri wa miaka 20 kiwango chake cha soka kimevutia timu nyingi hasa za Ligi Kuu England, ambazo zimekuwa zikichuana kupata saini yake, huku vita kali zaidi ikitarajia kutokea wakati wa dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
Nick Pope
NEWCASTLE United imeripotiwa kwamba itafungua milango kwa ajili ya kusikiliza ofa zinazomhusu kipa wa miamba hiyo ya St James' Park, Nick Pope ili kumpiga bei kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Newcastle inaamini itapata mteja wa kumchukua kipa huyo mwenye umri wa miaka 32 wakati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa huko kwenye ligi za Ulaya. Pope ni moja ya makipa wazuri waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England
Neymar
STAA wa Santos ya Brazil, Neymar ameripotiwa kuwa na mpango wa kurudi kujiunga na timu yake ya zamani ya Barcelona wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Wakala wa mchezaji huyo, Pini Zahavi alisema Neymar, ambaye aliachana na timu ya Al Hilal ya Saudi Arabia na kurudi kwao Brazil kujiunga na timu hiyo ya Santos, aliyowahi kuichezea pia utotoni, atakwenda kukipiga Nou Camp kama mchezaji huru kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.