Kocha Vipers ataka ubingwa Cecafa Kagame Cup
Muktasari:
- Mabingwa hao wa Ligi Kuu Uganda, wameonyesha makali yao katika Kundi A, wakiifunga Garde Républicaine ya Djibouti mabao 3-0 katika mchezo wa ufunguzi, kisha kuitandika Gor Mahia ya Kenya bao 1-0, matokeo yaliyowapa pointi sita na kuwaweka kileleni mwa kundi hilo.
KOCHA wa Vipers SC ya Uganda, Denis Jean Lavagne, amesema kikosi chake kimekuja Rwanda kwa lengo la kutwaa ubingwa wa Kombe la CECAFA Kagame baada ya kuanza vyema kampeni ya mashindano hayo kwa kushinda mechi mbili za kwanza.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Uganda, wameonyesha makali yao katika Kundi A, wakiifunga Garde Républicaine ya Djibouti mabao 3-0 katika mchezo wa ufunguzi, kisha kuitandika Gor Mahia ya Kenya bao 1-0, matokeo yaliyowapa pointi sita na kuwaweka kileleni mwa kundi hilo.
Vipers sasa inajiandaa na mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya APR FC ya Rwanda utakaochezwa Alhamisi hii Julai 30, 2026, ambayo ina pointi tatu.
Sare itawatosha Waganda hao kumaliza vinara wa kundi na kutinga hatua ya nusu fainali, lakini Lavagne amesema hesabu zao si kufuzu pekee bali ni kutwaa taji.
Kocha huyo alisema mwanzo mzuri walioupata umeongeza morali kwa wachezaji, lakini aksisitiza kuwa bado hakuna kilichopatikana kwani mechi ngumu zaidi zinawasubiri kuanzia hatua ya mtoano.
“Ni vizuri kuanza mashindano kwa ushindi. Matokeo hayo yanatupa kujiamini, lakini bado tuna kazi kubwa mbele yetu. Lengo letu ni kupigania ubingwa,” alisema Lavagne.