Mzigo mpya EPL hewani leo!

Muktasari:
- Wakati msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu England ukiwa umemalizika wiki chache tu zilizopita, klabu 20 sasa zitafahamu zitaanza na nani kwenye msimu mpya, ambapo ratiba yake itawekwa hadharani, Jumatano, Juni 18.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England imethibitisha kwamba itaweka hadharani ratiba ya msimu wa 2025/26, leo Jumatano.
Wakati msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu England ukiwa umemalizika wiki chache tu zilizopita, klabu 20 sasa zitafahamu zitaanza na nani kwenye msimu mpya, ambapo ratiba yake itawekwa hadharani, Jumatano, Juni 18.
Liverpool ilinyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita ilipomaliza pointi 10 juu ya timu iliyoshika nafasi ya pili, Arsenal. Na kwenye msimu huo, ulishuhudia timu za Southampton, Ipswich Town na Leicester City zikishuka daraja na kwamba msimu ujao zitakuwa kwenye Championship.
Sunderland, Burnley na Leeds United zimechukua nafasi zao, ikiaminika kwamba zitaonyesha kiwango bora kuliko wenzao walioshuka. Ratiba yao itasoma Jumatano na watajua wataanza na nani na lini.
Maofisa wa kutoka kwenye Ligi Kuu England wamefichua kwamba maandalizi ya ratiba yanachukua miezi sita. Na sakata hilo limefanywa na kampuni moja ya IT ya Ufaransa, Atos, ambayo ipo nje ya jiji la Paris. Kuna mambo kadhaa yalizingatiwa kabla ya uandaaji wa ratiba hiyo. Vitu vilivyozingatiwa ni ratiba ya mechi za kimataifa, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League na Europa Conference League ili kutengeneza ratiba ya Ligi Kuu England, ambayo haitakuwa na mwingiliano. Kingine kilichozingatiwa ni ratiba ya mechi za ligi nyingine za chini. Kingine kilichoangaliwa ni hali ya timu za eneo moja kutakuwa na ratiba ya mechi ya muda unaofanana, ambapo mfano Liverpool na Everton hazitaruhusiwa kucheza nyumbani kwenye muda mmoja na siku moja kwa sababu za kiusalama. Kitu kama hicho pia kitatumika kwenye mechi za Manchester United na Manchester City, lakini jambo hilo halina shida kwenye mechi za timu za London, ambako kuna idadi kubwa ya klabu.
Maombi ya binafsi ya timu pia yanazingatiwa hasa ikizingatiwa kwamba kama timu zitacheza kwenye uwanja mmoja. Kwa mfano, Oktoba 11, Old Trafford itahusika kwenye mashindano ya Super League Grand Final, hivyo, Man United itakuwa imeomba kucheza ugenini katika wikiendi hiyo.
Baada ya mazingatia ya mambo hayo, kuna sheria tatu muhimu zinazingatiwa kwenye upangaji wa ratiba ya Ligi Kuu England, ambapo kwanza, muda utakaotumika kucheza mechi tano za kwanza, ambapo timu italazimika kucheza mechi mbili nyumbani na tatu ugenini au kinyume chake. Pili, klabu haitaruhusiwa kuanza au kumaliza msimu kwa kucheza mechi mbili nyumbani au mbili ugenini. Katika msimu wa 2023/24, Luton Town ilianza msimu kwa kucheza mechi mbili mfululizo ugenini, kutokana na uwanja wao wa Kenilworth Road ulikuwa bado kwenye maboresho wakati ratiba ya Ligi Kuu England inaanza.
Tatu, katika kipindi cha kuelekea ratiba za Boxing Day na Mwaka Mpya, timu haitaruhusiwa kucheza nyumbani au ugenini mara mbili. Baada ya mambo yote hayo kuzingatiwa, klabu zitawekwa ili kutambua zitaanza msimu kwa kucheza nyumbani au ugenini. Kutoka na hilo, ratiba ya awali ya mechi zote 380 za Ligi Kuu England itawekwa hadharani Jumatano hii, ili kuzifanya timu kutambua zitaanza na nani na ligi katika msimu wa 2025-26.