Mvua yatibua ratiba La Liga
Muktasari:
- Timu hizo zilitarajiwa kukutana kwenye Uwanja wa Ciutat de València katika mchezo wa raundi ya sita, lakini mvua kubwa iliyonyesha jijini Valencia ilifanya uwanja huo kujaa maji na kushindikana kutumika.
VALENCIA, HISPANIA: MVUA kubwa iliyonyesha jana Septemba 16, 2026 muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo wa Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga kati ya Levante na Athletic Bilbao, ilifanya mtanange huo kuahirishwa.
Timu hizo zilitarajiwa kukutana kwenye Uwanja wa Ciutat de València katika mchezo wa raundi ya sita, lakini mvua kubwa iliyonyesha jijini Valencia ilifanya uwanja huo kujaa maji na kushindikana kutumika.
Wachezaji wa timu hizo walitoka uwanjani kwa ajili ya maandalizi ya mwisho, lakini hali ilibadilika haraka baada ya mvua kunyesha kwa nguvu, huku sehemu kubwa ya uwanja ikifunikwa na maji.
Hali hiyo ilisababisha mpira kushindwa kuzunguka vizuri wakati wa maandalizi, jambo lililofanya waamuzi, La Liga na maofisa husika kufanya ukaguzi wa uwanja.
Baada ya ukaguzi huo, iliamuliwa mchezo huo usichezwe kwa kuwa uwanja haukuwa katika hali inayoruhusu mchezo wa soka kufanyika.
Taarifa ya Athletic Bilbao ilisema La Liga itatangaza tarehe na muda mpya wa mchezo baada ya Levante na Athletic kufikia makubaliano kuhusu ratiba hiyo.
Levante iliingia katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa La Liga baada ya michezo mitano, huku Athletic Bilbao ikiwa nafasi ya tisa. Levante ilikuwa imeshinda mchezo mmoja pekee msimu huu, wakati Athletic ilikuwa imeshinda miwili kati ya michezo yake mitatu iliyopita.
Kuahirishwa kwa mchezo huo kulitokea wakati Valencia ikiwa chini ya tahadhari ya mvua kubwa, huku mamlaka ya hali ya hewa nchini Hispania, AEMET, ikiwa imetoa tahadhari kutokana na uwezekano wa mvua kubwa na dhoruba katika eneo hilo.
Athletic baada ya mchezo huo kuahirishwa, itashuka dimbani Jumamosi kucheza dhidi ya Deportivo Alavés kwenye Uwanja wa San Mamés, huku Levante ikiifuata Villarreal pale Estadio de la Cerámica, Jumapili hii.