Simba yaipasua Azam, Steve Barker aendeleza rekodi yake
Muktasari:
- Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, umeacha gumzo baada ya matukio mawili yalioonekana yangeweza kuwa penalti, lakini mwamuzi Herry Sasii alipoenda kujiridhisha katika Teknolojia ya FVS, akasema hamna kitu.
SIMBA leo Septemba 16, 2026 imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika pambano la Mzizima Dabi lililopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, huku kocha Msauzi, Steve Barker rekodi yake ya kutopoteza mechi ya Ligi Kuu Bara ikizidi kuwa hai.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, umeacha gumzo baada ya matukio mawili yalioonekana yangeweza kuwa penalti, lakini mwamuzi Herry Sasii alipoenda kujiridhisha katika Teknolojia ya FVS, akasema hamna kitu.
Kipindi cha kwanza kilimalizika bila ya bao, huku Simba ikitawala zaidi umiliki wa mpira kwa asilimia 56 dhidi ya 44 za Azam. Simba pia ilionekana kuwa na mpira mwingi zaidi katika ujenzi wa mashambulizi.
Kwa upande wa pasi, Simba ilipiga pasi 224, kati ya hizo 177 zilifanikiwa, wakati Azam ilipiga pasi 202 na kukamilisha 136. Takwimu hizo zilionyesha timu zote zikijaribu kutawala mchezo kwa kutumia mipira ya chini.
Licha ya umiliki huo, Simba ilishindwa kutengeneza hatari kubwa langoni mwa Azam katika kipindi cha kwanza, kwani ilipiga mashuti mawili ambayo yote hayakulenga lango, huku Azam ikiwa na shuti moja lililolenga lango.
Sintofahamu ya kwanza ilitokea dakika ya 30, wakati Paschal Msindo alipoukokota mpira na kuingia kwenye eneo la Simba, kabla ya Rushine De Reuck na Ismail Toure kumzuia. Baada ya tukio hilo kuangaliwa kupitia FVS, mwamuzi Sasii hakutoa penalti.
Dakika tatu baadaye Simba nayo ilidai penalti baada ya Rushine kugongana na Himid Mao ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, Sasii aliamua kuendelea na mchezo, akiona tukio hilo halikustahili penalti, hivyo matukio yote mawili yakabaki kuwa gumzo.
Mchezo huo pia ulikuwa na vita ya nguvu katikati ya uwanja, huku Mao akiwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakifanya kazi kubwa ya kuzuia mashambulizi ya Simba. Katika kipindi cha kwanza, Mao alifanya faulo tano dhidi ya Rushine, Elie Mpanzu na Libasse Gueye.
Kipindi cha pili Simba ilirudi ikiwa na kasi zaidi na dakika ya 52, Mao alifanya faulo nyingine dhidi ya Gueye, safari hii mwamuzi Sasii akamuonyesha kadi ya njano. Hapo ndipo Simba ilipoanza kuongeza presha kuelekea lango la Azam.
Dakika ya 58, presha hiyo ilizaa matunda baada ya beki wa Azam, Nathan Idumba Fasika, kujifunga kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Nathaniel Chilambo wa Simba, na kuwapa Wekundu wa Msimbazi uongozi wa 1-0.
Azam ilifanya mabadiliko dakika ya 62, Kipre Junior alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Idd Seleman 'Nado', lakini kabla haijapata nafasi ya kurejea mchezoni, Simba ikaendelea kulisakama lango lake.
Dakika ya 67, Clatous Chama akaongeza bao la pili kwa Simba baada ya Libasse Gueye kufanya kazi kubwa ya kuingia na mpira eneo la hatari, wakati Msindo akiwa kwenye harakati za kuokoa, akajikuta anampasia mfungaji, bao lililoongeza pengo hadi kuwa 2-0 na kuifanya Azam kuwa na kazi kubwa ya kusaka mrejesho katika dakika zilizobaki.
Ushindi huo kwa Simba umeifanya kuifukuzia Yanga kwa ukaribu zaidi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, zote zikiwa na pointi 18 kufuatia kushinda mechi sita walizocheza kila mmoja. Tofauti yao ni mabao, Yanga ikifunga 16 na Simba 11, huku kila moja ikiruhusu mawili.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Steve Barker, huo ulikuwa ni mchezo wa 31 wa Ligi Kuu Bara tangu atue kikosini hapo Desemba 19, 2025 ambapo hajapoteza hata mmoja, akishinda 24 na sare saba. Tangu Desemba 7, 2025 Simba ilipofungwa 2-0 na Azam katika ligi, haijapoteza tena na jana ililipa kisasi.
Kituo kinachofuata ni Kariakoo Dabi ambapo watani hao wa jadi walioanza msimu kwa ushindi wa asilimia 100, wanakutana kuamua nani mbabe.