Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mazoezi, udhibiti vyakula ndo mpango mzima  

Muktasari:

  • Mitandaoni, wengine wanajadili mbinu za kukabiliana na uzito kwa wachezaji kwa kutumia dawa, kama vile kujiuliza: Je, ni salama kiafya kwa wachezaji wa soka la kulipwa?

KATIKA michezo ya awali ya ligi mbalimbali duniani, ikiwamo ligi ya hapa nyumbani ya NBC na zile za kimataifa, ikiwamo EPL, La Liga na Bundesliga, tayari imeshuhudiwa baadhi ya washambuliaji wakionekana kama vile ni wazito.

Mitandaoni, wengine wanajadili mbinu za kukabiliana na uzito kwa wachezaji kwa kutumia dawa, kama vile kujiuliza: Je, ni salama kiafya kwa wachezaji wa soka la kulipwa?

Pamoja na kufanya mambo mbalimbali, kufanikiwa kupunguza uzito wa mwili kunatokana na mazoezi na udhibiti wa vyakula, ambao ndiyo mpango mzima wa kukabiliana na ukibonge. Lakini nilikutana na swali linalohusu dawa za kupunguza uzito au unene, ambazo nyingi zinatangazwa sana mitandaoni.

Bahati mbaya, Fifa ilipiga marufuku dawa za kupunguza uzito, kwani baadhi zinafanana kiutendaji na zile za kuongeza nguvu mchezoni.

Mtakumbuka mchezaji wa zamani wa Arsenal, Kolo Toure, aliwahi kupimwa na kukutwa anatumia dawa za kuongeza nguvu mchezoni zilizopigwa marufuku.

Baadaye alipunguziwa adhabu baada ya kubainika kuwa alitumia dawa hizo kwa bahati mbaya, kwani alimwona mke wake akitumia dawa za kupunguza uzito na naye akaamua kuzitumia. Hivyo, hapa tunapata picha kuwa dawa za kupunguza uzito au za kuongeza nguvu si njia sahihi ya kukabiliana na uzito uliokithiri, bali imebaki mazoezi na udhibiti wa vyakula ndiyo mpango mzima.

Wachezaji, hasa wanasoka vijana, ni kawaida kujikuta wakitumia dawa za kudhibiti uzito wa mwili, hasa kutokana na zama hizi ambazo ni za utandawazi. Wengine wanajikuta wanatumia dawa hizo, ambazo nyingi zina madhara, kwa bahati mbaya au kukosa ufahamu wa kutosha juu ya matumizi ya dawa hizo. Leo nitawapa ufahamu kuhusu dawa za kupunguza uzito uliokithiri au unene.


ZIFAHAMU DAWA ZA KUPUNGUZA UZITO

Ni kweli upunguzaji wa uzito wa mwili kwa kutumia dawa ni moja ya matibabu ambayo yanawachanganya wanajamii. Hii ni kutokana na uwepo wa taarifa nyingi za mitandaoni na uwepo wa matabibu wa kienyeji wanaotangaza dawa zao za kupunguza uzito wa mwili.

Kisayansi, njia salama ya kukabiliana na unene ni mazoezi mepesi na ulaji sahihi wa vyakula kwa kuzingatia kanuni za afya. Njia hii, hasa kwa mazoezi ya kila siku, ndiyo inakubalika kama nyenzo inayokabili unene ukilinganisha na dawa za kupunguza unene.

Katika huduma za afya, hakuna dawa iliyoidhinishwa na ipo ndani ya miongozo ya matibabu ya kitaifa na kimataifa, ikiwamo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ambayo ni salama kupunguza uzito wa mwili.

Zaidi, miongozo mingi inasisitiza unene uliokithiri au uzito mkubwa huweza kudhibitiwa kwa mazoezi na vyakula.

Bado, taasisi nyingi za chakula na dawa duniani zinazitilia shaka usalama wa dawa za kupunguza uzito, ndiyo maana hazipo katika miongozo ya matibabu.

Vipo vidonge ambavyo vimekuwa vikitumiwa mara kwa mara duniani katika nchi zilizoendelea kukabiliana na uzito wa mwili, ni pamoja na Orlistat, Belviq, Contrave, Sexenda, Phentermine na Qsymia.

Baadhi ya dawa hizo zinafanya kazi mwilini ikiwamo kuzuia unyonywaji wa mafuta na sukari katika mfumo wa chakula, nyingine huchochea homoni inayoitaarifu ubongo kuwa tumbo limejaa chakula na kukunyima hamu ya kula chakula.

Mtu anayeruhusiwa kuandika dawa za kupunguza uzito wa mwili ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani (physician) pekee. Hii ni kutokana na ukweli kwamba dawa hizo zina madhara makubwa, ikiwamo kusababisha shambulizi la ghafla la moyo.

Hutoa dawa hizo kwa watu ambao uwiano wa uzito wa mwili na urefu wa mwili (Body Mass Index) ni zaidi ya 30 au pengine ni 27, huku tayari ameanza kupata madhara ya unene, ikiwamo kuugua kisukari cha aina ya pili.

Vilevile, inapoonekana kuwa mbinu ya vyakula na mazoezi mepesi imeshindikana.

Si kila mtu anaweza tu kutumia dawa hizo, ni lazima wataalamu wa afya wamfanyie uchunguzi wa kina kuona kwamba mwili wake utaweza kukabiliana na madhara yatokanayo na dawa hizo.

Madhara ya dawa za kupunguza unene wa mwili ni pamoja na kupata maumivu ya tumbo, kupata choo chenye mafuta, kuumwa kichwa, kupata kichefuchefu, kizunguzungu, sukari ya mwili kuwa chini, mapigo ya moyo kudunda bila mpangilio na kukosa usingizi.

Ieleweke kuwa kutumia dawa hizi kiholela bila kumwona daktari ni sawa na kuyaweka maisha yako hatarini. Si salama kwa afya yako kutumia dawa za kupunguza unene.

Mbadala sahihi wa dawa hizi ni mazoezi mepesi ya mara kwa mara, ikiwamo kutembea umbali wa kilomita mbili kila siku kwa siku tano za wiki, kuruka kamba, kuendesha baiskeli, kuogelea, kucheza muziki uliochangamka na kufanya shughuli za kuushughulisha mwili.

Ukiacha wachezaji ambao hufanya mazoezi kila siku, kwa watu wa kawaida wanatakiwa angalau kufanya mazoezi mepesi kwa dakika 30-60 kwa siku, kwa siku tano za wiki.

Ni vizuri wachezaji na watu wa kawaida kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na kuepuka kutumia dawa zozote kiholela.

Mbadala sahihi wa kukabiliana na uzito wa mwili ni mazoezi mepesi na udhibiti wa vyakula vinavyonenepesha, ikiwamo wanga, sukari na mafuta.