Nani anamtaka Alvarez Barca?
Muktasari:
- Kumsajili Rodri bila shaka ilikuwa hatua kubwa, lakini simulizi kubwa kwa Barcelona katika dirisha la usajili la majira ya joto lilikuwa ni harakati zao zisizokoma za kumsajili Julian Alvarez, ambapo mshambuliaji huyo wa Atletico Madrid alionekana kuwa mrithi kwenda kuchukua nafasi ya Robert Lewandowski, na yeye mwenyewe alikuwa tayari kukabiliana na changamoto hiyo mpya.
BARCELONA, HISPANIA; BARCELONA imekuwa ikifunga mabao mengi tangu Hansi Flick alipowasili 2024, na licha ya kukosa usajili wa mshambuliaji mpya katika dirisha la usajili la majira ya joto, hali hiyo imeendelea msimu huu.
Kumsajili Rodri bila shaka ilikuwa hatua kubwa, lakini simulizi kubwa kwa Barcelona katika dirisha la usajili la majira ya joto lilikuwa ni harakati zao zisizokoma za kumsajili Julian Alvarez, ambapo mshambuliaji huyo wa Atletico Madrid alionekana kuwa mrithi kwenda kuchukua nafasi ya Robert Lewandowski, na yeye mwenyewe alikuwa tayari kukabiliana na changamoto hiyo mpya.
Hata hivyo, Atletico walikuwa wakali katika msimamo wakidai Alvarez haendi popote na hasa kwa mpinzani wao katika Ligi Kuu Hispania (La Liga). Ungefikiri hilo lingekuwa tatizo kwa Barca, lakini ukweli ni kwamba, licha ya kumkosa straika waliyemlenga wamekuwa wakifanya vizuri sana mbele ya lango la timu pinzani.
TANO TANO ZIPO NYINGI
Barcelona imefunga mabao matano katika mechi nne kati ya sita katika mashindano yote msimu huu, ikiwa na jumla ya mabao 26. Wamefunga 21 katika mechi tano za La Liga, angalau saba zaidi ya timu nyingine yoyote ikiwa na maana kwamba wametupia mara nyingi nyavuni kuliko timu nyingine yoyote katika ligi tano kubwa za Ulaya.
Ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Elche ulifuatiwa na ushindi wa kawaida zaidi wa 2-0 dhidi ya Athletic Club. Tangu hapo, wameifunga Rayo Vallecano 5-2, Valencia 5-0 na Levante 4-2. Wastani wa Barcelona wa kufunga mabao 4.2 kwa kila mchezo wa ligi ni mkubwa zaidi kuliko wa timu yoyote katika ligi tano kubwa za Ulaya msimu huu wakiwa mbele ya Freiburg ya Ujerumani yenye 3.3, huku pia wakifunga matano katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu dhidi ya Feyenoord (5-1).
Kwa hiyo, baada ya kushindwa kumsajili Alvarez, Barcelona wamewezaje kufunga mabao mengi kiasi hicho? Timu hiyo ilimsajili Gabriel Jesus kutoka Arsenal, lakini alionekana zaidi kama mbadala wa Ferran Torres; mchezaji wa kikosi badala ya mshambuliaji wa kuanza, hivyo Flick amebadilika katika wiki za mwanzo za msimu wa 2026-27.
Raphinha hakuwahi kucheza kama mshambuliaji msimu uliopita, lakini ametumia asilimia 90 ya muda wake msimu huu akiongoza safu ya ushambuliaji. Na amekuwa akifanya hivyo vizuri. Mchezaji huyo wa zamani wa Leeds United kwa ujumla amekuwa akicheza pembeni pamoja na Lamine Yamal na Anthony Gordon, na watatu hao wamekuwa na matokeo mazuri hadi sasa.
Raphinha tayari ana mabao manane msimu huu, huku Yamal akiwa na saba. Gordon bado hajafunga tangu alipohamia kutoka Newcastle United katika majira ya joto, lakini ametoa asisti nne za mabao katika La Liga, ambazo ni nyingi zaidi kwa pamoja kuliko mchezaji yeyote katika ligi tano kubwa za Ulaya sawa na Paulo Dybala wa Roma.
Fermin Lopez ameongeza mabao manne, huku mchezaji mpya Karim Adeyemi akiwa na matatu. Jesus alifungua akaunti yake ya mabao katika ushindi mkubwa dhidi ya Feyenoord wiki iliyopita. Hata hivyo, hilo halipaswi kuwa jambo la kushangaza. Barca siyo wageni katika kufunga . Walifunga mabao 95 katika ligi msimu uliopita, ikiwa ni idadi ya pili kwa wingi miongoni mwa timu zote katika ligi tano kubwa za Ulaya, nyuma ya Bayern Munich (122).
Hilo limekuwa jambo la kawaida tangu Flick alipochukua timu 2024, ambapo Barcelona imefunga mabao 344 katika mechi 123 chini ya uongozi wake, ikiwa na wastani wa mabao 2.8 kwa kila mchezo. Hata hivyo, uwezo wa kufunga haujatokana tu na kutengeneza nafasi nyingi. Real Madrid (104) wamepiga mashuti mengi zaidi katika La Liga msimu huu kuliko Barcelona (96).
Lakini, kikosi cha Flick ni hatari sana katika kumalizia nafasi. Kiwango cha kubadili mashuti kuwa mabao cha asilimia 21.9 msimu huu ni cha pili kwa ukubwa miongoni mwa timu zote katika ligi tano kubwa za Ulaya, nyuma ya Elversberg ambao ni wageni katika Bundesliga (26.7% – mabao manane kutokana na mashuti 30).
UBORA SI MCHEZO
Kiwango hicho cha ubadilishaji nafasi kuwa mabao kinatokana na ukweli kwamba wanatengeneza nafasi zenye ubora wa juu. Jumla yao ya mabao yanayotarajiwa (xG) 16.7 katika La Liga ndiyo kubwa zaidi kwa tofauti ya 3.7 (wakiwa mbele ya Madrid wenye 13.0), huku wastani wao wa mabao yanayotarajiwa (xG) 3.35 kwa kila mchezo ukiwa mkubwa zaidi katika ligi tano kubwa za Ulaya (wakiwa mbele ya Bayern wenye 2.94).
Barca wanapata wastani wa xG 0.19 kwa kila shuti katika La Liga msimu huu, huku hakuna timu inayopata wastani mkubwa zaidi katika ligi tano kubwa za Ulaya. Mabao 17 kati yao ya La Liga yametokana na pasi za mabao, ambayo ni angalau saba zaidi ya timu nyingine yoyote. Bila shaka, lazima izingatiwe kwamba jambo dogo kama mpira wa krosi kugusa mchezaji kidogo linaweza kusababisha pasi ya mwisho isihesabiwe rasmi kuwa asisti, lakini ukweli kwamba mabao 17 kati ya 21 yamepatokana na pasi murua unaashiria kuwa mabao ya Barcelona kwa ujumla yametokana na mashambulizi yaliyo safi na yaliyokusudiwa, na siyo kutegemea mpira kubahatisha kurudi kwao au kugonga mchezaji mwingine.
Kwa kuwa wana safu ya mbele inayobadilika na kucheza kwa uhuru, siyo jambo la kushangaza kwamba mara nyingi wanajaribu kupeleka mpira nyuma ya safu za ulinzi. Barcelona wamejaribu pasi 37 za kupenyeza mpira nyuma ya safu ya ulinzi katika La Liga msimu huu (12 zimefanikiwa); hiyo ni zaidi ya mara mbili ya timu nyingine yoyote isipokuwa Racing Santander (19). Pasi ya kupenyeza mpira ndiyo inayopita kwenye safu ya ulinzi ya wapinzani, kwa kawaida ikisababisha hali ya mchezaji mmoja kukabiliana na kipa.
Pengine siyo jambo la kushangaza kwamba, ukiondoa penalti mbili, hakuna hata moja ya mabao yao yaliyotokana na mipira ya adhabu. Jumla yao ya mabao 19 yaliyofungwa katika mchezo wa kawaida ni angalau manane zaidi ya mpinzani wao yeyote katika La Liga.
Yamal anaupiga zaidi akiwa ametoka kushinda Kombe la Dunia 2026 akiwa tayari ametengeneza nafasi 18 za kufunga katika mchezo wa kawaida, nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote katika ligi tano kubwa za Ulaya, na zaidi ya mara mbili ya nafasi zilizotengenezwa na mchezaji mwenzake yeyote. Hata hivyo, bado hajatoa pasi yake ya kwanza ya bao, jambo ambalo ni la kushangaza ukizingatia idadi ya mabao ambayo Barca imefunga.
Raphinha kwa upande wake amekuwa katika kiwango bora sana katika nafasi yake mpya ya mshambuliaji wa kati, ambapo kwenye mechi sita msimu huu amefunga mabao manane kutokana na mashuti 18 akiwa na kiwango cha kubadili mashuti kuwa mabao cha asilimia 44.4. Hii inajumuisha penalti, lakini hata ukiondoa penalti hiyo, bado kiwango hicho kinakuwa asilimia 41.2.
Wachezaji kama Gordon na Dani Olmo bado hawajaanza kufunga msimu huu, hivyo kama kuna chochote, inaonekana kuna uwezekano wa Barcelona kufunga mabao zaidi hasa ikiwa wachezaji wenzake Yamal wataanza kutumia nafasi anazowatengenezea. Bila shaka, huu ni mwanzo mdogo wa msimu, lakini kwa kasi yao ya sasa ya kufunga, Barca wanaelekea kufunga mabao 160 katika La Liga msimu huu.
Ni kweli, hilo litakuwa jambo kubwa kuweza kufikiwa. Rekodi ya mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa La Liga inashikiliwa na Real Madrid, waliowahi kufunga 121 msimu wa 2011-12, lakini kila mara mabingwa wa La Liga wanapocheza, wanaonekana kuwa na uwezo wa kufunga mabao mengi.
Katika mashindano yote msimu uliopita, Barcelona walifunga mabao 144 katika mechi 57. Ikiwa watacheza idadi hiyo hiyo ya mechi msimu huu, watakuwa kwenye mwelekeo wa kufikisha 247. Huenda tusiweke dau lolote juu ya hilo, lakini unaweza kufikiria jambo hilo? Jana waliwakaribisha Racing Santander, kabla ya kusafiri kwenda Sevilla mwishoni mwa wiki kuelekea mapumziko ya mechi za kimataifa. Je, wanaweza hata kufikisha mabao 30 ya La Liga kabla ya mapumziko ya kwanza ya mechi za kimataifa za msimu? Huenda tukasikia tena kuhusu juhudi mpya za Wakatalunya kumnasa Alvarez mwezi Januari, lakini kwa hali ilivyo sasa, Barca wanaonyesha wanaridhika kabisa na kile walichonacho tayari.