Musiala afichua tatizo la afya yake
Muktasari:
- Musiala, mwenye umri wa miaka 23, alianguka wakati Bayern ikishinda mchezo wa kirafiki dhidi ya FC Heidenheim Jumanne, siku tatu tu baada ya kukumbwa na hali kama hiyo katika mchezo dhidi ya RB Leipzig.
MUNICH, UJERUMANI: KIUNGO wa Bayern Munich, Jamal Musiala amefichua kuwa amegundulika kuwa na tatizo linalosababisha mshtuko wa muda mfupi wa kutokuwepo fahamu “absence seizures”, baada ya kuanguka mara mbili ndani ya siku nne.
Musiala, mwenye umri wa miaka 23, alianguka wakati Bayern ikishinda mchezo wa kirafiki dhidi ya FC Heidenheim Jumanne, siku tatu tu baada ya kukumbwa na hali kama hiyo katika mchezo dhidi ya RB Leipzig.
Katika matukio yote mawili, Musiala alipata nafuu na kuondolewa uwanjani, lakini hali hiyo ilizua hofu kuhusu afya yake.
Baada ya mchezo huo, kiongozi wa Bayern, Max Eberl, alisema klabu ilikuwa “inafahamu hali yake” na kwamba mchezaji huyo angezungumza kuhusu kilichotokea.
Musiala sasa amevunja ukimya kupitia taarifa ndefu aliyoitoa, akieleza kuwa amegundulika kuwa na mshtuko wa muda mfupi wa kutokuwepo fahamu unaosababishwa na hitilafu ya muda katika mfumo wa fahamu.
Hata hivyo, nyota huyo aliwatuliza mashabiki akisema anaendelea vizuri na kwamba hali hiyo ni ya muda na inaweza kutibiwa kwa urahisi.
“Jambo la kwanza kabisa, niko vizuri! Ninashukuru sana kwa ujumbe na sapoti zenu. Ninaelewa kuwa wengi wenu mna wasiwasi, hivyo ningependa kuwaondolea hofu na kueleza kinachoendelea.
“Nimegundulika kuwa na absence seizures za muda mfupi ambazo zinasababishwa na hitilafu ya mfumo wa fahamu. Hali hiyo inaweza kusababisha matukio kama yale yaliyotokea dhidi ya Leipzig na sasa Heidenheim.
“Ninaelewa kuwa kwa mtazamo wa kwanza yanaweza kuonekana ya kutisha, lakini kwangu kwa sasa ni sehemu ya maisha yangu ya kila siku. Ninapata matibabu bora na nina matumaini makubwa,” alisema Musiala.
Musiala aliongeza kuwa Bayern pamoja na familia na marafiki zake wameendelea kuwa karibu naye katika kipindi hicho, huku akisisitiza kuwa hakuna hatari nyingine za kiafya zinazomkabili.
Alisema amekuwa akishauriana kwa karibu na wataalamu wa afya na kwamba, baada ya kupata ruhusa kutoka kwa madaktari bingwa wa mfumo wa fahamu, ameamua kuendelea na maisha yake ya kawaida pamoja na kufanya kile anachokipenda zaidi, ambacho ni kucheza soka.
“Kinachonisaidia zaidi katika safari hii ni kuendelea kutafuta ushindi na mataji pamoja na timu yangu na kupata sapoti yenu kubwa.
“Naomba sasa mnielewe vizuri zaidi. Wakati huo huo, naomba muelewe kwamba ningependa suala hili libaki kati yangu, watu wangu wa karibu, klabu na wataalamu wa afya,” aliongeza.
HALI HIYO IKOJE?
Absence seizures kwa kawaida ni matukio mafupi yanayoweza kudumu kati ya sekunde tano na 15, yakisababishwa na hitilafu ya muda katika shughuli za umeme za ubongo.
Mtu anayekumbwa na hali hiyo anaweza kwa muda mfupi kupoteza mwelekeo, usawaziko au hata kuanguka.
Hata hivyo, hali hiyo inaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa na kwa kawaida haihusiani na dalili kama kutetemeka kwa nguvu au misuli kukakamaa, ambazo huonekana zaidi katika aina nyingine za mshtuko.
Katika tukio lake la kwanza dhidi ya Leipzig Jumamosi, Musiala alionekana kuchanganyikiwa na kushindwa kusimama vizuri.
Alionekana akitanua mikono yake huku akiyumba na kushuka kuelekea chini, kabla ya wachezaji wenzake, Ismael Saibari na Joshua Kimmich, kuwahi kumshika na kumzuia asidondoke uwanjani.
WACHEZAJI WALIOANGUKA UWANJANI
Matukio ya wachezaji kuanguka ghafla uwanjani kutokana na matatizo ya kiafya yamewahi kutokea katika soka la kiwango cha juu, huku baadhi yakihitaji huduma za dharura za kuokoa maisha.
Hali hiyo imewahi kuwakumba mastaa kadhaa, wakiwamo Christian Eriksen, Fabrice Muamba na Sergio Aguero.
Christian Eriksen
Kiungo wa Denmark, Christian Eriksen, alianguka ghafla uwanjani baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati wa mchezo wa Euro 2020 dhidi ya Finland.
Eriksen alihitaji huduma ya haraka ya CPR kabla ya kuokolewa na kurejea katika hali nzuri.
Baadaye alirejea kucheza soka la kulipwa akiwa ametumia kifaa maalumu cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo, kinachojulikana kama implantable cardioverter-defibrillator (ICD).
Fabrice Muamba
Kiungo wa zamani wa Bolton Wanderers, Fabrice Muamba, alipata mshtuko mkubwa wa moyo wakati wa mchezo wa FA Cup mwaka 2012 dhidi ya Tottenham Hotspur.
Moyo wake ulisimama kwa muda wa dakika 78 kabla ya madaktari na wahudumu wa afya kufanikiwa kumrejesha.
Tukio hilo lilitikisa dunia ya soka na hatimaye Muamba alilazimika kustaafu soka akiwa bado kijana.
Sergio Aguero
Mshambuliaji wa zamani wa Argentina na Manchester City, Sergio Aguero alipata maumivu makali ya kifua na matatizo ya kupumua wakati akiichezea Barcelona mwaka 2021.
Baada ya kufanyiwa vipimo, aligundulika kuwa na tatizo la mpangilio wa mapigo ya moyo, hali iliyomlazimisha kutangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 33.
Nabil Bentaleb
Kiungo wa Algeria, Nabil Bentaleb, pia aliwahi kukumbwa na dharura ya kiafya mwaka 2024 iliyohusisha moyo.
Tukio hilo lilimlazimu kulazwa hospitalini kwa ajili ya matibabu na uangalizi wa karibu kabla ya kuendelea na safari yake ya kurejea katika shughuli za kawaida.
Musiala ni tofauti
Hata hivyo, hali iliyompata Jamal Musiala ni tofauti na matukio hayo yaliyohusisha moyo.
Musiala ameelezwa kuwa na absence seizures za muda mfupi zinazotokana na hitilafu ya mfumo wa fahamu, badala ya mshtuko wa moyo.
Pamoja na tofauti hizo, matukio ya ghafla ya kiafya kwa wachezaji wa soka yanaendelea kuonyesha umuhimu wa huduma za haraka za kitabibu na ufuatiliaji wa afya za wanamichezo, kutokana na mahitaji makubwa ya kimwili wanayokabiliana nayo katika mchezo huo.
KUELEWA ABSENCE SEIZURES
Absence seizures ni nini?
Ni hali ya kupoteza fahamu kwa muda mfupi na ghafla, inayosababishwa na hitilafu ya muda katika mfumo wa fahamu wa ubongo. Mtu anaweza kuonekana kama amepoteza mwelekeo au ufahamu kwa sekunde chache kabla ya kurejea katika hali yake ya kawaida.
Hudhibitiwaje?
Tofauti na aina za mshtuko zinazoweza kusababisha mwili kutetemeka au misuli kukakamaa, absence seizures kwa kawaida huwa za muda mfupi na mtu huweza kurejea katika hali yake ya kawaida haraka.
Kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu na kupata ruhusa kutoka kwa wataalamu wa afya, hali hiyo inaweza kudhibitiwa huku wakiendelea na shughuli zao za kawaida, ikiwemo michezo.