Prime
Kiungo asubiri mamilioni Simba
SIMBA inaelezwa kuwa imeachana na aliyekuwa kiungo wake Alassane Kante na sasa inatakiwa kumlipa zaidi ya milioni 90 ili kuachana naye jumla.
Tangu mwanzoni mwa msimu huu, vyanzo vya ndani kutoka kwenye timu hiyo vilisema kuwa Kante anaweza kuuzwa muda wowote, lakini usajili wa Kelvin Nashon na Ibra Jabaar vikaongeza tetesi hizo ambapo mara kwa mara viongozi wa timu hiyo walikuwa wanasema kuwa taarifa kuhusu kiungo huyo zitatolewa.
Awali kabla dirisha la usajili halijafungwa ilielezwa kuwa Kante alikuwa akiwindwa na timu kadhaa kubwa Afrika, lakini hadi usajili unafungwa Agosti 15, 2026, kiungo huyo rais wa Senegal alikuwa hajamalizana na timu yoyote hali iliyowalazimisha Simba kumuondoa kwenye mfumo kwa kuwa angebaki wangevunja kanuni ambayo inawataka kuwa na wachezaji 13 wa kigeni.
Chanzo kutoka kwa mtu wa karibu na mchezaji huyo, kilisema kwa sasa Kante hana timu baada ya Simba kusitisha mkataba wake na sasa anachosubiri nchini ni kulipwa fedha hizo kulingana na makubaliano ambayo yapo ili aondoke na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.
“Simba haikuwa na mpango wa kuendelea na Kante ingawa mikakati yao ilikuwa ni kumtafutia timu ya kumuuza jumla, iliposhindikana kwa wakati wakataka kumtoa kwa mkopo, lakini mchezaji hakuwa tayari kwa hilo, ametaka wamalizane ili aendelee na maisha mengine,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Baada ya mchezaji kujua timu haina projekti naye, anataka amalizane na uongozi kwa amani kama alivyojiunga na timu hiyo kwa amani, anachokitamani ni kuona apate chalenji nyingine mpya hasa katika timu ambayo itakuwa na programu naye kwa ajili ya kuendeleza kipaji chake.”
Chanzo hicho kiliendelea kusema: “Baada ya kupitia vipengele vya mkataba wake kwa upande wa mchezaji atatakiwa alipwe zaidi ya Sh90 milioni, kwa sasa ametolewa kabisa katika mipango ya timu, anaendelea na mambo mengine akisubiria haki yake.”
Simba ilimsajili Kante Julai 23, 2025 kwa mkataba wa miaka miwili chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fadlu Davis akitokea CA Bizertin ya Tunisia. Ametumika msimu mmoja pekee, kisha mkataba wake ukasitishwa kwa makubaliano ya pande mbili.
ATAJWA MOROCCO
Agosti 2, 2026, siku chache kabla ya Simba kuthibitisha kutoendelea na Kante kutokana na kutomtambulisha katika tamasha la Simba Day lililofanyika Agosti 8, 2026, taarifa kutoka Tunisia zilibainisha kwamba, Kocha wa Raja Casablanca, Nasreddine Nabi alikuwa akiangalia uwezekano wa kumsajili kiungo huyo ili kuimarisha kikosi chake kuelekea mashindano ya msimu wa 2026-2027 ikiwemo ushiriki wao wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Raja Casablanca iliyomaliza msimu wa 2025-2026 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tunisia maarufu Botola Pro, ikiwa nyuma kwa pointi tatu dhidi ya mabingwa MAS Fes, kwa mujibu wa jarida la Morocco, LeSiteInfo, klabu hiyo imevutiwa na uwezo wa mchezaji huyo na inaamini anaweza kuongeza nguvu katika safu yao ya kiungo.
Kiungo huyo alikuwa mchezaji muhimu kwenye eneo la kiungo la Simba msimu uliopita akiisaidia kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB pamoja na Kombe la Muungano.