Prime
Aziz KI anatumika hivi Yanga
UKIANGALIA picha za siku ya kwanza ya mazoezi ya Yanga, wakati Stephanie Aziz KI alipoanza kujifua na timu hiyo kwa mara ya kwanza akiwa pamoja na mshambuliaji Peter Shalulile, utaona pacha nzuri ambayo kocha wa timu hiyo, Manqoba Mngqithi anaitengeneza ndani ya dakika tisini.
Aziz KI ndiye mchezaji wa mwisho kuingia kwenye kikosi cha Yanga, akichukua nafasi ya Allan Okello, aliyeondoka klabuni hapo na kujiunga na AS FAR Rabat ya Morocco, inayotajwa kutumia Dola 1.2 milioni (Sh3.1 bilioni) kumnunua. Juzi, alifanya mazoezi na timu hiyo kwa muda wa saa 1:30 sawa na dakika 90 na kuonyesha mabadiliko makubwa.
Kiungo huyo raia wa Burkina Faso alifanya mazoezi kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga na Yanga akitokea Ittihad ya Libya. Hii ni mara ya pili kwake kurejea klabuni hapo.
Katika mazoezi hayo, kocha wa Yanga alionekana muda mwingi akimpa Aziz KI majukumu ya kuchezesha safu ya ushambuliaji kwa kupiga pasi nyingi za katikati, huku akimtumia zaidi Shalulile kupokea mipira nyuma ya mabeki na kuingia ndani ya boksi kufunga.
Kwenye mazoezi hayo ambayo yalihudhuriwa na Mwanaspoti, kocha huyo alikuwa akimtaka Aziz KI apige pasi haraka, huku akimweleza Shalulile kuwa anatakiwa kuondoka kwa kasi kabla mpira haujatoka mguuni kwa kiungo huyo, ambaye aliwahi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa kufunga mabao 21 msimu wa 2023/2024.
Hata hivyo, jicho la Mwanaspoti limegundua kocha wa Yanga ameshapata mchezaji ambaye timu inaweza kucheza ikimtegemea, kwani mara nyingi amekuwa akiwaelekeza wachezaji wengine kumpasia Aziz KI mipira mingi zaidi.
Kocha wa mipira ya kutengwa, Kagisho Dikgacoi, pia alionekana kumfuatilia kwa karibu kwa kuwa kiungo huyo ana uwezo wa juu wa kupiga mipira ya kutengwa kuliko wachezaji wote kwenye ligi.
Baada ya kumaliza majukumu yake na Shalulile, ambayo yalionekana kukamilika kwa kiwango kikubwa, makocha wa timu hiyo walimbadilishia Aziz KI pacha. Sasa alitakiwa kumpasia mipira mingi kiungo wa pembeni, Housseine Zakouani, ambaye pia walionekana kuelewana vyema huku mara kwa mara wakipongezana.
Aziz KI alionekana kuwa mchangamfu wakati wote wa mazoezi, akibadilishana mawazo na wachezaji wapya huku pia akitaniana na wale aliowakuta klabuni hapo kabla ya kuondoka na kujiunga na Wydad Athletic msimu mmoja uliopita.
Hesabu za Yanga za kumrudisha Aziz KI, mbali na ubora wake wa kufunga, kubwa zaidi ni namna anavyoweza kuwafanya washambuliaji wa kati kupata huduma nzuri na kufunga kwa njia tofauti za utengenezaji wa mashambulizi, tofauti na jinsi timu hiyo ilivyoanza msimu huu.
Katika mechi mbili za mashindano ambazo Yanga imezicheza, imewatumia washambuliaji Shalulile na Toure wakianza pamoja na wakati mwingine kupishana katika michezo dhidi ya Simba kwenye Ngao ya Jamii na Ligi dhidi ya Namungo.
Ndani ya mechi hizo, washambuliaji hao wamepata pasi nne pekee za mashambulizi kutoka katikati ya uwanja. Kati ya hizo, Toure amepata mipira miwili na Shalulile miwili, lakini wote wameshindwa kuzitumia vyema nafasi hizo.
Kuonyesha jinsi usajili wa Aziz KI, ambaye anacheza zaidi katikati, utakavyokuwa na faida kwa Yanga, katika michezo miwili iliyopita washambuliaji hao wamepata mipira 13 ya krosi. Kati ya hiyo, sita iliwafikia; Shalulile akipata minne na Toure miwili.
Huu unaweza kuwa usajili muhimu zaidi kwa Yanga msimu huu kutokana na ubora alionao Aziz KI, ambaye pamoja na uwezo wa kufunga, ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao.
WASIKIE MAKOCHA
Akizungumzia ujio wa Aziz KI, kocha wa Yanga, Manqoba amesema anamjua kiungo huyo na kwamba ataongeza kitu kutokana na ubunifu wake wa kupiga pasi za mwisho kwenda katika robo ya mwisho ya eneo la wapinzani.
“Namjua Aziz KI, si mchezaji mpya kwangu wala hapa Yanga. Tunahitaji kuwa na watu wabunifu kutoka pembeni, lakini pia kutoka eneo la katikati. Unatakiwa kuwaweka wapinzani kwenye presha wakati wote ili kuangalia wapi watafanya kosa,” amesema kocha huyo.
Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, akizungumzia kurejea kwa Aziz KI amesema Yanga imezidi kuimarisha kikosi chake, ambapo sasa ni wazi washambuliaji wa timu hiyo watakuwa na nafasi kubwa ya kufunga kwa kutumia ubunifu wa raia huyo wa Burkina Faso.
“Yanga kumrudisha Aziz KI, nadhani hii si taarifa nzuri kwa timu pinzani. Kwenye timu ambayo ina mshambuliaji mjuzi wa kutumia nafasi kama Shalulile, halafu unamuongeza Aziz KI, hizi ni hesabu za kutengeneza mabao zaidi. Sasa washambuliaji wa timu hiyo kazi yao ni kuhakikisha wanafunga zaidi,” amesema Robertinho.