Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HUSSEIN AZENGA; Bodaboda anayepigania ndoto za kuwa Mwakinyo

AZENGA Pict

Muktasari:

  • Azenga, mzaliwa wa Morogoro, aliamua kuhamia Dar es Salaam kutafuta maisha, lakini kabla ya kujikita kwenye masumbwi alikuwa akifanya shughuli mbalimbali za kujikimu.

MIONGONI mwa mabondia wanaochipukia kwenye ngumi ni Hussein Azenga kutoka Chorila Boxing, ambaye maisha yake yamejaa simulizi ya kupambana na mazingira huku akitafuta nafasi ya kutimiza ndoto zake katika mchezo huo.

Azenga, mzaliwa wa Morogoro, aliamua kuhamia Dar es Salaam kutafuta maisha, lakini kabla ya kujikita kwenye masumbwi alikuwa akifanya shughuli mbalimbali za kujikimu.

“Nilifika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 2017. Nilikuwa nafanya kazi  katika soko la  Mabibo na baada ya kukaa kwa mwaka mmoja nikarudi nyumbani kwa sababu sikuwa naelewa mambo yalikuwa magumu. Baadaye nilirudi tena Dar es Salaam na kuanza maisha ya kujitegemea.”

AZE 01

TWAHA KIDUKU

Bondia huyo baada ya kurejea tena Dar mwaka 2022 akaingia kwenye ngumi na bondia ambaye alikuwa akimfuatilia kwa wakati huo ni Twaha Kiduku kutokana na ubora wake ulingoni.

Alivutiwa zaidi na namna mashabiki walivyokuwa wakishangilia na kuonyesha mapenzi kwa bondia huyo, jambo lililomfanya naye atamani siku moja awe sehemu ya mchezo huo na kuwafanya watu wamkubali kupitia uwezo wake

“Nilikuwa nikimuona kaka yangu Twaha kwenye TV sasa zile vaibu za mashabiki na namna wanavyomkubali nikaaanza na mimi kuupenda mchezo huo na kuona naweza kuwa moja ya bondia mkubwa Afrika,” anasema Azenga


BODABODA

Bondia huyo anasema ngumi pekee hazitoshi kuendesha maisha yake hivyo mbali na mazoezi ya ngumi anafanya kazi ya kuendesha bodaboda ili kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

Azenge anasema ana familia inayomtegemea, akiwa na mke pamoja na mtoto mmoja, hivyo muda mwingine maisha yanamlazimisha kuvaa kofia mbili kwa wakati mmoja; moja ya bondia na nyingine ya dereva bodaboda.

“Nikiamka nafanya kazi ya bodaboda kwa sababu lazima niishi na niihudumie familia yangu. Lakini muda wa mazoezi ukifika naifunga bodaboda yangu na kwenda gym. Lazima nipambane pande zote mbili.”

Maisha hayo ndiyo yanayomfanya Azenga kuamini kuwa safari yake ya mafanikio haitegemei ngumi pekee bali mapambano ya kila siku ili mkono uende kinywani.

Azenga anasema ana kiwango cha nyota 1.5, baada ya kushuka kutoka mbili kutokana na kutopigana kwa muda mrefu. Pambano lake la mwisho alicheza mwezi Januari dhidi ya Juma Saidi  jambo ambalo limeathiri kushuka kwa kiwango chake.

“Nilikuwa na nyota mbili lakini kwa sababu sijapigana kwa muda mrefu tangu Januari, sasa niko kwenye nyota moja na nusu. Natamani nipate pambano ili nirudi kwenye kiwango changu,” anasema bondia huyo.

AZE 04

PAMBANO BAGAMOYO

Miongoni mwa mapambano ambayo ameyaweka kwenye kumbukumbu yake ni lile dhidi ya Adam Lazaro lililofanyika Bagamoyo.

Azenga anakumbuka pambano hilo kwa sababu alipewa taarifa muda mfupi kabla ya siku ya pambano, hali iliyomlazimisha kutumia bodaboda kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo kwa ajili ya kupima uzito na baadaye kurejea tena kwa pambano.

Pamoja na maandalizi mafupi na safari hiyo, aliingia ulingoni na kuonyesha uwezo wake, akifanikiwa kushinda kwa KO katika raundi ya nne, wakati pambano hilo lilipangwa kuwa la raundi nane.

“Hilo ni moja ya mapambano ambayo sitalisahau. Nilipewa taarifa siku tatu kabla. Nilikwenda Bagamoyo kwa bodaboda kupima uzito, nikarudi na baadaye nikapambana. Pamoja na changamoto zote nilishinda kwa KO raundi ya nne,” anasema Azenga na kuongeza

“Pambano langu la mwisho nilipigana na Juma Saidi na nilifanikiwa kumaliza kwa KO raundi ya pili. Sasa ninachohitaji ni kupata mapambano zaidi ili niendelee kupanda.”

AZE 03

WADHAMINI CHANGAMOTO

Kama ilivyo kwa mabondia wengi wanaochipukia, Azenga anaona ukosefu wa wadhamini ni moja ya changamoto kubwa zinazowakabili.

Kwa mtazamo wake, bondia anahitaji mtu au kampuni inayoweza kumsaidia katika maandalizi, usafiri, mazoezi na mahitaji mengine ili aweze kujiandaa vizuri bila kulazimika kugawanya muda wake kati ya michezo na shughuli za kujikimu.

“Changamoto kubwa ni kupata mtu wa kushika mkono. Bondia anahitaji mdhamini ukiwa na mtu anayekuamini, unaweza kujiandaa vizuri na kupigana mara nyingi zaidi na kwa kiwango kikubwa.”

Azenga anaongeza kuwa kuna wakati mwingine matokeo ya bondia yanatokana na sapoti iliyopo nyuma yake akitolea mfano kuna baadhi ya mabondia ambao unashangaa ameshindaje ikiwa pambano linaonekana wazi.

“Kwenye ngumi kuna mikono mirefu. Wakati mwingine bondia akiwa na watu wenye nguvu nyuma yake anaweza kupata nafasi ambayo mwingine hana sisi ambao hatuna wadhamini tunahitaji kusaidiwa ili tupate nafasi sawa.”


NDOTO ZAKE

Pamoja na changamoto hizo Azenga anasema matumaini yake ndani ya miaka 10 ni kuwa bondia anayeshikilia mikanda mbalimbali ya Afrika na kufuata nyayo za mabondia waliomtangulia

Miongoni mwa majina anayoyataja ni Twaha Kiduku, Hassan Mwakinyo na Mfaume Mfaume, ambao kwake ni mifano ya mabondia walioweza kujenga majina yao ndani na nje ya Tanzania.

“Ndani ya miaka 10 ijayo nataka nifike mbali. Nataka kufuata nyayo za mabondia kama Twaha Kiduku, Mwakinyo na Mfaume Mfaume. Ndoto yangu ni kuiwakilisha Tanzania kimataifa na watu duniani wanifahamu.”