Rooney amtaka nyota Arsenal atue Man United
Muktasari:
- Rooney alitoa kauli hiyo katika kipindi cha kwanza cha podcast yake mpya ya Stick to United, anayoiendesha pamoja na Mark Goldbridge, baada ya United kufungwa mabao 4-2 na AC Milan katika mchezo wao wa mwisho wa maandalizi ya msimu mpya.
MANCHESTER, ENGLAND GWIJI wa Manchester United, Wayne Rooney amependekeza Manchester United imsajili chipukizi wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly, akiamini anaweza kuwa suluhisho katika nafasi ya beki wa kushoto na pia kiungo wa kati.
Rooney alitoa kauli hiyo katika kipindi cha kwanza cha podcast yake mpya ya Stick to United, anayoiendesha pamoja na Mark Goldbridge, baada ya United kufungwa mabao 4-2 na AC Milan katika mchezo wao wa mwisho wa maandalizi ya msimu mpya.
Rooney alisema nimesikia kwamba anaweza kupatikana kwa kiasi kisicho kikubwa cha fedha. Kwangu mimi, huo ni uamuzi rahisi kabisa.
“Ukipata mchezaji anayeweza kucheza beki wa kushoto na pia kiungo wa kati, akiwa bado kijana na mwenye maisha marefu mbele yake, sioni sababu ya kutomleta,” alisema Rooney.
Hata hivyo, Rooney anaamini usajili wa Lewis-Skelly hautamaliza tatizo jingine la United katika eneo la kiungo, ambako ameitaka timu hiyo kuongeza nguvu na uimara wa mwili.
“Ningependa kuona nguvu zaidi katikati ya uwanja. Tunahitaji kiungo mkubwa wa box-to-box ambaye anaweza kuvunja mashambulizi, kwenda mbele na mpira, kuona pasi na kuwa na nguvu katikati ya uwanja.
“Ukiwaangalia Youri Tielemans, Kobbie Mainoo na Andrey Santos, wote ni wachezaji wadogo kimwili na hakuna mwenye kasi kubwa miongoni mwao,” aliongeza.
Ingawa hakumtaja moja kwa moja kama chaguo la kwanza, Rooney alimtaja kiungo wa Aston Villa, Amadou Onana, kama mchezaji mwenye aina ya sifa ambazo Manchester United inahitaji.
Katika hatua nyingine, Rooney amemtaja beki Luke Shaw kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao klabu hiyo haipaswi kumtegemea kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu England.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Milan, Goldbridge alimlaumu Shaw kwa kuruhusu mabao yote manne.
“Nilifikiri Luke Shaw alihusika kwenye mabao yote manne. Tulicheza vibaya na sidhani kama anaweza kucheza mechi mbili kwa wiki,” alisema Goldbridge.
Rooney alikubaliana naye kwa kiasi, akisema Shaw hakuwa na mchezo mzuri, licha ya kuwa na msimu mzuri uliopita.
“Nilifikiri alikuwa na msimu mzuri uliopita, lakini hakufanya vizuri dhidi ya AC Milan. Kwa hiyo, sidhani kama unaweza kumtegemea Luke Shaw kuwa katika kiwango kilekile kwa msimu mzima,” alisema Rooney.
Carrick naye ataka usajili
Kauli za Rooney zimekuja wakati Carrick mwenyewe akihitaji klabu kuongeza wachezaji kabla ya dirisha la usajili kufungwa Septemba 1.
Carrick alisema wiki iliyopita kuwa United bado inahitaji kuongeza nguvu katika kikosi ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kushindania mafanikio msimu huu.
“Tunataka zaidi, tunahitaji zaidi na tunaendelea kutafuta namna ya kufanya hivyo. Najua fedha ni fedha, hilo nalielewa.
“Tunapaswa kusukuma kila kitu tunachohusika nacho, huku tukitambua uhalisia wa historia ya hivi karibuni kwa kipindi fulani.
“Kwa sasa tunapaswa kutumia tulichonacho vizuri, lakini lazima tusukume kila mpaka tunaoweza ili tuweze kushinda tena. Hilo ndilo changamoto,” alisema Carrick.