Mshahara wa Sancho wazitibua Napoli, Juventus

Muktasari:
- Taarifa zinaeleza Sancho ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Chelsea anataka kulipwa mshahara wa Pauni 250,000 kwa wiki kiasi ambacho timu zote zimeweka wazi kuwa haziwezi kumlipa.
NAPOLI na Juventus zipo tayari kuilipa Manchester United Pauni 25 milioni kwa ajili ya kumsajili winga wa timu hiyo na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho, lakini changamoto kubwa imekuwa ni mahitaji binafsi ya mchezaji.
Taarifa zinaeleza Sancho ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Chelsea anataka kulipwa mshahara wa Pauni 250,000 kwa wiki kiasi ambacho timu zote zimeweka wazi kuwa haziwezi kumlipa.
Man United inatamani sana kumuuza mchezaji huyo ili kupata pesa itakazotumia kufanya usajili katika dirisha hili kwa sababu bajeti yake hairuhusu kunyofoa sehemu zingine.
Mkataba wa sasa wa Sancho unatarajiwa kumalizika 2027. Awali ilidaiwa huenda angesaini kusalia Chelsea ambako alicheza kwa mkopo.
Eberechi Eze
ARSENAL imepanga kuingia kwenye vita dhidi ya majirani zake wa Jiji la London, Tottenham Hotspur kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Eberechi Eze, 26, katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi. Taarifa zinaeleza Palace ipo tayari kumwachia staa huyu lakini inahitaji kiasi kisichopungua pauni 68 milioni kama ada yake ya uhamisho.
Cristian Romero
TOTTENHAM Hotspur inahitaji Pauni 60 milioni ada ya uhamisho ili kumuuza beki wa kati raia wa Argentina, Cristian Romero, 27, dirisha hili la majira ya kiangazi. Beki huyo yupo katika rada za Atletico Madrid inayoitaka saini yake, lakini haipo tayari kutoa kiasi hicho cha fedha badala yake inataka kutoa Pauni 30 milioni. Hadi sasa bado mazungumzo yanaendelea baina ya vigogo wa timu zote mbili juu ya dili hilo.
Marc Guehi
WAWAKILISHI wa Liverpool wako London kufanya mazungumzo na Crystal Palace kwa ajili ya kuipata saini ya beki kisiki wa timu ya taifa ya England, Marc Guehi, 24, katika dirisha hili. Guehi ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Palace ambayo ipo tayari kumuacha aende lakini kwa ofa ambayo itakuwa nono. Inaelezwa Mwenyewe anatamani kutua Liverpool.
Joao Pedro
NEWCASTLE United imewasilisha ofa rasmi Brighton ili kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Brazil, Joao Pedro, 23. Pia imewasilisha ofa Burnley ili kumsajili kipa wa timu hiyo raia wa England, James Trafford, 22. Baada ya kuwasilisha ofa hizo hadi sasa bado hakuna majibu rasmi iliyopokea kutoka kwa timu husika.
Illia Zabarnyi
MABOSI wa Bournemouth wapo tayari kumuuza beki wa kati raia wa Ukraine, Illia Zabarnyi katika dirisha hili la majira ya kiangazi ikiwa timu inayomtaka italipa Pauni 59 milioni. Zabarnyi mwenye umri wa miaka 22, amezivutia timu nyingi Ulaya kutokana na mchango mkubwa alioutoa akiwa na Bournemouth msimu uliomalizika na Paris St-Germain (PSG) inadaiwa kuwa imeshaanza hadi mazungumzo kwa ajili ya kumsajili mchezaji huyo.
Warren Zaire-Emery
MABOSI wa Manchester United wametuma wawakilishi kwenda Ufaransa kwa ajili ya kuzungumza na Paris St-Germain ili kumsajili kiungo wa timu hiyo na Ufaransa, Warren Zaire-Emery, 19, katika dirisha hili la majira ya kiangazi.Mchezaji huyo amekuwa akifuatiliwa na Manchester United kwa muda mrefu akiwa na PSG na timu ya taifa.
Maxime Esteve
NURNLEY imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuhitaji kisia kisichopungua Pauni 50 milioni ili kumuuza beki wake wa kati raia wa Ufaransa, Maxime Esteve, 23, ambaye anawindwa sana na Bayern Munich. Inaelezwa kocha wa Bayern Munich, Vincent Kompany ni shabiki mkubwa wa staa huyo ambaye aliwahi kumfundisha akiwa Burnley.