Mreno abwaga manyanga Ghana
Muktasari:
- Shirikisho la Soka Ghana (GFA) limethibitisha Alhamisi kuwa limekubaliana na Queiroz kuvunja mkataba kwa makubaliano ya pande zote, ikiwa ni takribani mwezi mmoja tu tangu kocha huyo raia wa Ureno alipoteuliwa tena kuiongoza timu hiyo.
ACCRA, GHANA: KOCHA Carlos Queiroz amebwaga manyanga kuinoa timu ya taifa ya Ghana 'Black Stars', baada ya kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Gambia kuzidisha hali ngumu ndani ya timu hiyo.
Shirikisho la Soka Ghana (GFA) limethibitisha Alhamisi kuwa limekubaliana na Queiroz kuvunja mkataba kwa makubaliano ya pande zote, ikiwa ni takribani mwezi mmoja tu tangu kocha huyo raia wa Ureno alipoteuliwa tena kuiongoza timu hiyo.
Katika taarifa yake ya kuagana iliyochapishwa kwenye tovuti ya GFA, Queiroz amesema uamuzi huo haukuwa rahisi, lakini pande zote zilikubaliana kuwa mazingira yaliyokuwepo yalifanya kuvunja uhusiano wao wa kikazi kuwa uamuzi unaofaa zaidi.
Amesema maslahi ya Ghana, Black Stars na soka la nchi hiyo yalipaswa kuwa mbele ya kila kitu.
Queiroz ameongeza kuwa mazingira muhimu ya kuendelea na kazi hayakuwa yamekamilika kikamilifu, huku matokeo ya hivi karibuni yakichangia uamuzi wa kumaliza safari yake.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Ghana kupoteza nyumbani kwa mabao 4-2 dhidi ya Gambia katika mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON, licha ya Black Stars kuanza kwa kasi na kuongoza mabao 2-0.
Ernest Nuamah na Felix Afena-Gyan waliipa Ghana matumaini ya ushindi baada ya kuifungia mabao mawili, lakini Gambia iligeuza mchezo na kufunga mabao manne mfululizo kwenye Uwanja wa Accra Sports.
Kabla ya kipigo hicho, Ghana ilikuwa pia imepoteza kwa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Ivory Coast, hivyo kubaki mkiani mwa Kundi C bila pointi baada ya mechi mbili.
Queiroz anaondoka akiwa na rekodi ya ushindi mmoja, sare mbili na vipigo vinne katika michezo saba aliyosimamia, huku timu yake ikifunga mabao matano na kufungwa 10.
Kuondoka kwake kunafunga safari yake yenye misukosuko ya miezi mitano tangu aliporejea Ghana Aprili, alipowekwa kwenye mkataba wa miezi minne uliolenga kuipeleka timu hiyo kwenye Kombe la Dunia 2026.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 73 aliiongoza Ghana kufika hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010, baada ya kuifunga Panama na kutoka sare dhidi ya England.
Hata hivyo, Ghana ilitolewa na Colombia kwa kufungwa bao 1-0 katika hatua ya 32 bora.
Mkataba wake wa awali ulimalizika baada ya mashindano hayo, lakini GFA iliamua kumrejesha tena kwenye nafasi hiyo Septemba 2.
Kuondoka kwa Queiroz kunailazimisha GFA kuanza tena mchakato wa kutafuta kocha na suluhisho la kurejesha utulivu katika kipindi ambacho Black Stars inapitia wakati mgumu.
Ghana kwa sasa iko nyuma kwa pointi sita dhidi ya Ivory Coast na Gambia baada ya michezo miwili.
Kwa kuwa ni timu mbili pekee za juu kutoka kila kundi lenye timu nne zitakazofuzu, Black Stars tayari imejiweka kwenye mazingira magumu katika harakati za kuzuia kukosa AFCON kwa mara ya pili mfululizo.