AFCON PAMOJA 2027: Wenyeji, Misri wasuasua, vigogo wagawa dozi
Muktasari:
- Katika michezo ya raundi ya kwanza ya kusaka tiketi za fainali hizo ambazo wenyeji wamepangwa katika makundi mbalimbali walishuhudia tanzania ikipokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Guinea- Bissau, huku Uganda na Kenya wakilazimishwa sare ya bao 1-1 na Tunisia na Eritrea. Zimbabwe ikifanya maajabu baada ya kupindua meza na kuifunga Sierra Leone 3-2 ikiwa imetoka nyuma kwa mabao mawili.
DAR ES SALAAM: WENYEJI wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) PAMOJA 2027, Tanzania, Kenya na Uganda wameanza vibaya kampeni hiyo, huku vigogo Morocco, Ivory Coast, Algeria, Nigeria na Cameroon wakianza kwa ushindi.
Katika michezo ya raundi ya kwanza ya kusaka tiketi za fainali hizo ambazo wenyeji wamepangwa katika makundi mbalimbali walishuhudia tanzania ikipokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Guinea- Bissau, huku Uganda na Kenya wakilazimishwa sare ya bao 1-1 na Tunisia na Eritrea. Zimbabwe ikifanya maajabu baada ya kupindua meza na kuifunga Sierra Leone 3-2 ikiwa imetoka nyuma kwa mabao mawili.
Kwa upande mwingine, mabingwa wa kihistoria Misri na Senegal hazikuanza kampeni zao kwa ushindi, baada ya Misri kulazimishwa suluhu nyumbani na Angola, huku Senegal ikitoka sare ya 1-1 na Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa ushindani wakiwa chini ya kocha wake mpya Patrick Vieira.
Rwanda na Mali zilianza kwa ushindi wa mabao matatu, huku Mauritania, Namibia, Sudan, Togo, Gambia, Malawi, Niger na DR Congo pia zikikusanya pointi zote tatu.
KUNDI A: Morocco na Niger zaanza kwa kasi
Morocco na Niger zilianza kwa ushindi na kujiweka kileleni mwa Kundi A.
Morocco iliifunga Gabon 2-0, Noussair Mazraoui akifungua bao dakika ya 36 kabla ya Soufiane Rahimi kufunga la pili dakika sita kabla ya mchezo kumalizika.
Niger yenyewe ilinusurika presha ya Lesotho na kushinda 2-1. Daniel Sosah alifunga dakika ya 38 kabla ya Oumar Sako kuongeza la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Lesotho ilipata bao la matumaini kupitia penalti ya Sera Motebang dakika ya 85, lakini Niger ililinda ushindi wake.
Matokeo: Morocco 2-0 Gabon; Niger 2-1 Lesotho.
KUNDI B: Malawi yaongoza, Misri yasimama
Malawi imeanza ikiwa kileleni mwa Kundi B baada ya kuifunga Sudan Kusini 2-1, wakati Misri na Angola zilishindwa kupata bao Cairo.
Babatunde Adepoju aliipa Malawi uongozi dakika ya 20 kabla Stephen Joseph Dhata kusawazisha dakika tatu baada ya mapumziko.
Lloyd Njaliwa aliifungia Malawi bao la ushindi dakika ya 64.
Misri ilidhani imepata bao kupitia Mostafa Zico dakika ya 21, lakini mwamuzi alilikataa kwa sababu ya kuotea.
Hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao jingine, hivyo Angola ikaondoka Cairo na pointi moja muhimu.
Matokeo: Malawi 2-1 Sudan Kusini; Misri 0-0 Angola.
KUNDI C: Ivory Coast na Gambia zaanza kwa ushindi
Ivory Coast ilianza vizuri katika kipindi cha pili cha kocha Herve Renard baada ya kuifunga Ghana 2-0 mjini Bouake.
Malick Yalcouye, mmoja wa wachezaji wapya nane kwenye kikosi cha Renard, alifungua bao dakika ya 44 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Franck Kessie.
Kessie mwenyewe alifunga kwa penalti dakika ya 58 na kuipa Ivory Coast ushindi.
Gambia nayo ilianza kwa pointi tatu baada ya kuifunga Somalia 2-1.
Ebrima Colley alifunga penalti dakika ya 18 kabla Bilal Njie kusawazisha dakika ya 72. Mshambuliaji aliyeingia akitokea benchi, Muhammed Badamosi, aliipa Gambia bao la ushindi dakika 11 baadaye.
Matokeo: Ivory Coast 2-0 Ghana; Gambia 2-1 Somalia.
KUNDI D: Afrika Kusini yaua, Kenya yashikwa
Afrika Kusini ilianza kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Guinea katika mchezo wa kwanza wa Pitso Mosimane tangu arejee kuiongoza timu hiyo.
Ime Okon na Samukele Kabini waliifungia Bafana Bafana, huku Seydouba Cisse akiisawazishia Guinea.
Kabini alifunga bao la ushindi dakika ya 77, likiwa bao lake la kwanza katika timu ya taifa.
Nairobi, Kenya ilihitaji bao la Ryan Ogam dakika ya 87 kuokoa sare ya 1-1 dhidi ya Eritrea, baada ya Nahom Girmai Netabay kuipa Eritrea uongozi.
Afrika Kusini inaongoza kundi kwa pointi tatu, Kenya na Eritrea zikiwa na pointi moja kila moja, huku Guinea ikiwa haina pointi.
Kenya tayari imefuzu moja kwa moja kama mwenyeji wa mashindano, hivyo timu iliyomaliza juu kati ya Afrika Kusini, Guinea na Eritrea itaungana na Kenya kwenye AFCON PAMOJA 2027.
Matokeo:Afrika Kusini 2-1 Guinea; Kenya 1-1 Eritrea
KUNDI E: Zimbabwe yafanya 'comeback' kubwa
Zimbabwe ilifanya moja ya mabadiliko makubwa zaidi katika raundi ya kwanza baada ya kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuifunga Sierra Leone 3-2.
Alie Conteh na Sallieu Tarawallie waliipa Sierra Leone uongozi kabla Marshall Munetsi kupunguza bao dakika ya 72.
Tawanda Chirewa alisawazisha dakika nne baadaye kabla Munetsi kukamilisha mabadiliko hayo dakika ya 88 kwa bao lake la pili.
DR Congo nayo ilianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Equatorial Guinea, mabao yakifungwa na Chancel Mbemba na Yoane Wissa.
Matokeo: DR Congo 2-0 Equatorial Guinea; Sierra Leone 2-3 Zimbabwe.
KUNDI F: Mauritania yaanza kwa ushindi
Mauritania imeanza kampeni kwa kuifunga Jamhuri ya Afrika ya Kati mabao 3-1.
Aboubakary Koita alifungua bao kwa penalti kabla Goduine Koyalipou kusawazisha.
Dawda Camara aliirudisha Mauritania mbele kabla Mamadou Diallo kufunga bao la tatu.
Burkina Faso na Benin zilitoka sare ya 1-1.
Lassina Traore aliipa Burkina Faso uongozi kwa penalti dakika ya 20, lakini Aiyegun Tosin alisawazisha kwa penalti dakika ya 68.
KUNDI G: Cameroon na Namibia zaanza kwa ushindi
Cameroon iliifunga Comoros 3-1 na kuanza vizuri kampeni yake.
David Ningo alifungua bao kabla Bryan Mbeumo kuongeza la pili muda mfupi baada ya mapumziko.
Warmed Omari aliifungia Comoros bao la kufutia machozi, lakini Danny Namaso alifunga dakika ya 81 na kuhitimisha matumaini ya wapinzani.
Namibia iliifunga Congo 1-0 mjini Gaborone kupitia bao la kichwa la Bethuel Muzeu dakika mbili baada ya mapumziko.
Matokeo: Cameroon 3-1 Comoros; Namibia 1-0 Congo.
KUNDI H: Sare kila upande
Hakuna timu iliyopata ushindi katika Kundi H baada ya mechi zote mbili za kwanza kumalizika kwa sare.
Uganda, ambayo tayari imefuzu kama mwenyeji, ilitoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Tunisia.
Adem Arous aliipa Tunisia bao dakika ya 12 kabla Rogers Mato kuisawazishia Uganda dakika ya 68.
Libya nayo ilitoka nyuma kwa mabao mawili na kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Botswana.
Tumisang Orebonye aliifungia Botswana mabao mawili kabla Maruwan Alhibeeshi kupunguza pengo na Ezoo El Mariamy kusawazisha kwa penalti katika muda wa nyongeza.
Matokeo: Tunisia 1-1 Uganda; Libya 2-2 Botswana.
KUNDI I: Algeria na Togo zaanza kwa ushindi
Algeria ilimpa kocha mpya Brahim Hamdani mwanzo mzuri baada ya kuifunga Zambia 3-1.
Jaouen Hadjam alifungua bao baada ya dakika mbili tu, lakini Fashion Sakala aliisawazishia Zambia dakika ya 57.
Ibrahim Maza aliirudisha Algeria mbele dakika 10 baadaye kabla Anis Hadj Moussa, aliyeingia akitokea benchi, kufunga la tatu dakika ya 74.
Togo nayo ilianza kwa ushindi baada ya kuifunga Burundi 1-0 kupitia bao la Dermane Karim dakika ya 17.
Matokeo: Algeria 3-1 Zambia; Togo 1-0 Burundi.
KUNDI J: Sudan yaongoza, Senegal yashikiliwa
Sudan imeanza kileleni mwa Kundi J baada ya kuifunga Ethiopia 1-0 kupitia bao la Mohamed Eisa dakika ya 86.
Senegal, chini ya kocha mpya Patrick Vieira, ilishindwa kupata ushindi katika mchezo wake wa kwanza wa ushindani.
Nicolas Jackson aliipa Senegal uongozi dhidi ya Msumbiji dakika ya 32, lakini Geny Catamo akasawazisha katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza.
Hakuna timu iliyofunga bao la pili kipindi cha pili, hivyo Sudan ikaongoza ikiwa na pointi tatu.
Matokeo: Sudan 1-0 Ethiopia; Msumbiji 1-1 Senegal.
KUNDI K: Rwanda na Mali zaanza kwa mabao matatu
Rwanda na Mali zote zilianza kampeni kwa ushindi wa mabao 3-1.
Rwanda iliifunga Liberia baada ya kuonesha kiwango kizuri kipindi cha kwanza.
Abeddy Biramahire alifunga dakika ya pili kabla Mickels Leroy Jacques kuongeza la pili.
Sylvanus Nimely aliipa Liberia bao la matumaini, lakini Mickels Joy Lance alifunga kwa penalti na kuirejeshea Rwanda tofauti ya mabao mawili kabla ya mapumziko.
Mali iliifunga Cape Verde 3-1.
Martial Tia alifungua bao dakika ya tano kabla Lopes Cabral kusawazisha.
Nene Dorgeles alifunga mabao mawili, moja kila kipindi, na kuipa Mali pointi zote tatu.
Matokeo: Rwanda 3-1 Liberia; Mali 3-1 Cape Verde.
KUNDI L: Guinea-Bissau yaanza kwa kishindo
Guinea-Bissau ilipata moja ya ushindi mkubwa wa ugenini katika raundi ya kwanza baada ya kuifunga Tanzania 2-0.
Franculino Dju alifungua bao dakika ya 33 kabla Mama Balde kuongeza la pili dakika ya 58.
Ushindi huo una umuhimu zaidi kwa sababu Tanzania tayari imefuzu kama mwenyeji wa mashindano, hivyo Guinea-Bissau, Nigeria na Madagascar zinachuana kwa nafasi ya juu miongoni mwa timu ambazo si wenyeji.
Nigeria nayo ilikusanya pointi tatu baada ya kuifunga Madagascar 2-1 kwa kugeuza matokeo.
Ehsan Kari aliipa Madagascar uongozi dakika ya 16 kabla George Ilenikhena kusawazisha katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza.
Moses Usor, aliyeingia akitokea benchi, alifunga bao la ushindi dakika ya 65.
Guinea-Bissau inaongoza kundi kwa tofauti ya mabao mbele ya Nigeria.
Matokeo: Tanzania 0-2 Guinea-Bissau; Nigeria 2-1 Madagascar.
Raundi ya pili imeanza, huku timu zilizopoteza pointi katika mechi za kwanza zikipata nafasi ya kurekebisha matokeo na zile zilizoanza kwa ushindi zikilenga kuendeleza mwenendo huo katika mbio za kufuzu AFCON PAMOJA 2027.
RATIBA KESHO, JUMATATU
Equatorial Guinea vs Sierra Leone (saa 1:00 usiku)
Zimbabwe vs DR Congo(saa 1:00 usiku)
Jamhuri Afrika Kati vs Burkina Faso (saa 1:00 usiku)
Botswana vs Tunisia(saa 10:00 jioni)
KESHOKUTWA, JUMANNE
Madagascar vs Tanzania (saa 10:00 jioni)
Uganda vs Libya (saa 1:00 usiku)
Gabon vs Niger (saa 10:00 jioni) Lesotho vs Morocco (saa 10:00 jioni)
Sudan Kusini vs Misri (saa 10:00 jioni)
Ghana vs Gambia(saa 1:00 usiku); Somalia vs Ivory Coast (saa 10:00 jioni)
Benin vs Mauritania (saa 10:00 jioni)
Comoros vs Namibia (saa 8:00 mchana)
Congo vs Cameroon (saa 10:00 jioni)
Cape Verde vs Rwanda (saa 1:00 usiku)
Liberia vs Mali (saa 10:00 jioni)
Guinea-Bissau vs Nigeria (saa 1:00 usiku)
Zambia vs Togo (saa 1:00 usiku); Burundi vs Algeria (saa 10:00 jioni)
Msumbiji vs Sudan (saa 10:00 jioni; Ethiopia vs Senegal (saa 4:00 jioni)
JUMATANO
Eritrea vs Afrika Kusini (saa 1:00 usiku)
ALHAMISI
Guinea vs Kenya (saa 1:00 jioni)