MRBEAST: YouTube ni dunia yake
Muktasari:
- Katika mtandao wa YouTube, MrBeast ambaye jina lake halisi ni Jimmy Donaldson, ndiye Ronaldo na Messi wa huko na mbali ya mafanikio ya namba nyingi za watazamaji pia ana mafanikio ya utajiri ambao kwa kiasi kikubwa ameupata kupitia mtandao huo. Leo tumekusogezea hapa.
FLORIDA, MAREKANI: KATIKA moja ya mahojiano ya Cristiano Ronaldo alipokuwa akielezea kilichomsukuma hadi kufungua chaneli yake ya YouTube ni watoto wake walimwambia hata kama akiwa na chaneli hatoweza kumpita Mrbeast na kwa sababu hiyo staa huyu alimtafuta Beast na kuamua kutengeneza naye video mara baada ya kufungua chaneli yake.
Katika mtandao wa YouTube, MrBeast ambaye jina lake halisi ni Jimmy Donaldson, ndiye Ronaldo na Messi wa huko na mbali ya mafanikio ya namba nyingi za watazamaji pia ana mafanikio ya utajiri ambao kwa kiasi kikubwa ameupata kupitia mtandao huo. Leo tumekusogezea hapa.
ANAPIGAJE PESA
Chanzo chake kikuu cha mapato ni YouTube ambako ana chaneli zaidi ya tatu na ile kubwa zaidi ina subscribers zaidi ya milioni 200.
Kupitia chaneli zote kwa mwezi staa huyu anapata zaidi ya Dola 50 milioni.
Pia ana udhamini wa kampuni mbalimbali anazofanya nazo kazi kama balozi na kwa kila video kampuni hizo ambazo ni Honey, Shopify, Amazon na NordVPN humlipa takriban Dola 1 milioni.
Mrbeast pia ana duka lake la mtandaoni ambalo huuza mashati, hoodies, kofia na bidhaa nyingine na kwa mwaka linakadiriwa kumpa mapato ya takriban Dola 30 milioni.
Nyota huyu pia anamiliki kampuni yake ya MrBeast Burger iliyoanzishwa mwaka 2020 ambayo ilikuwa na matawi sehemu mbalimbali duniani.
Ndani ya muda mchache tangu kuanzishwa kwake iliingiza faida ya takriban Dola 100 milioni.
Ana kampuni ya Feastables ambayo inafanya vizuri sana kwa sasa ikiwa inatengeneza bidhaa mbalimbali za kutafuna (bites) kama vile chocolate zinazouzwa kwenye maduka kama Walmart na kwenye mtandao.
Maduka yanayouza bidhaa hizi yapo sehemu mbalimbali duniani.
Kijumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 500 milioni.
Ndani ya mwaka mmoja staa huyu anakadiriwa kupata kati ya Dola 500 hadi 700 milioni.
NYUMBA
Tofauti na mastaa wengine matajiri, MrBeast hapendi sana masuala ya kununua majumba ya kifahari.
Mwaka 2023 alinunua nyumba ya kawaida North Carolina kwa Dola 320,000.
Alinunua pia nyumba tano zilizo karibu na nyumba yake ili kuwaweka marafiki na wafanyakazi wake karibu. Nyumba hizo kwa pamoja zinakadiriwa kugharimu Dola 2 milioni.
Ameamua kuishi maisha ya kawaida ili kuwekeza zaidi kwenye kusaidia wengine na kukuza biashara zake.
MSAADA WAKE KWA JAMII
MrBeast amejijengea jina la utofauti kutokana na moyo wake wa kusaidia jamii. Miongoni mwa misaada maarufu:
Kupandikiza lensi za macho kwa watu zaidi ya 1,000 waliokuwa hawaoni vizuri.
Kugawa nyumba, magari na fedha taslimu kwenye video zake.
Kulipia ada ya shule kwa mamia ya wanafunzi.
Kupanda miti milioni 20 kupitia mradi wa TeamTrees.
Kusafisha bahari na mito kupitia TeamSeas.
Ingawa si mpenda magari wa kifahari sana, MrBeast amewahi kumiliki au kutumia magari haya:
Tesla Model 3 Dola 40,000
Lamborghini Huracán Dola 200,000
BMW i8 Dola 140,000
Toyota Corolla Dola 20,000
MAHUSIANO NA BATA
MrBeast sio mtu wa bata kabisa na hapendelei kutumia vitu vya kifahari. Aliwahi kuwa kwenye uhusiano na Maddy Spidell, mwanamitindo na mshawishi wa mitandao ya kijamii. Walianza kuonekana pamoja mwaka 2019 kabla ya baadae kuachana.
Kwa sasa yupo katika uhusiano na mrembo kutoka Afrika Kusini, Thea Booysen ambaye wamekuwa pamoja tangu mwaka 2022 na mwaka 2024 alimvalisha pete ya uchumba.