Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morocco yalipa kisasi kwa Afrika Kusini

MOROCCO Pict

Muktasari:

  • Bingwa wa mwaka 2022, Afrika Kusini iliingia WAFCON 2026 ikiwa na heshima kubwa, uzoefu wa mashindano na wachezaji waliocheza mechi kubwa lakini ilishindwa kufurukuta mbele ya wenyeji Morocco.

ROBO fainali ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake ilitamatika baada ya Morocco kulipa kisasi cha mwaka 2022 ikiitandika Afrika Kusini mabao 2-1 na kutinga nusu fainali.

Bingwa wa mwaka 2022, Afrika Kusini iliingia WAFCON 2026 ikiwa na heshima kubwa, uzoefu wa mashindano na wachezaji waliocheza mechi kubwa lakini ilishindwa kufurukuta mbele ya wenyeji Morocco.

Ukiitazama tangu mashindano yanaanza kwa Afrika Kusini tatizo halikuwa uwezo wa Banyana Banyana, bali namna walivyoanza mashindano na kushindwa kutumia nafasi zao katika nyakati muhimu.

MORO 01

Kosa la kwanza lilianza kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Tanzania na walitawala vipindi kadhaa na kupata nafasi nyingi, lakini Twiga Stars wakawashangaza kwa ushindi wa 2-1.

Afrika Kusini ilipiga mashuti 24 dhidi ya 10 ya Tanzania, lakini bado ikaondoka uwanjani bila pointi. Hapo ndipo mambo yalipoanza kuonekana magumu walikuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi, lakini hawakuwa na ukali wa kutosha kuzibadilisha nafasi hizo kuwa matokeo.

Mchezo dhidi ya Ivory Coast ukaonyesha tena udhaifu huo. Afrika Kusini ilijikuta nyuma kwa mabao mawili, lakini uzoefu wao ukawasaidia kurejea na kulazimisha sare ya 2-2.

Ushindi wa 1-0 dhidi ya Burkina Faso uliwafungulia mlango wa robo fainali, lakini Afrika Kusini ilimaliza nafasi ya pili Kundi B, nyuma ya Ivory Coast iliyomaliza na pointi saba. Hii ndiyo iliwakutanisha na Morocco, mshindi wa Kundi A, katika robo fainali.

MORO 02

Kwenye robo fainali, Morocco ilionyesha tofauti kubwa katika jambo moja kutumia nyakati muhimu. Wenyeji walipata bao la kwanza dakika ya 31 kupitia Sakina Ouzraoui, kabla Hanane Aït El Haj kuongeza la pili kwa penalti dakika ya 51.

Banyana ilipata bao la kufufua matumaini kupitia Thembi Kgatlana dakika ya 67, lakini haikuweza kupata bao la pili. Morocco haikuwa bora kila dakika, lakini ilijua muda gani wa kuongeza kasi, kutulia na lini kutumia udhaifu wa mpinzani.

Tofauti nyingine ilikuwa utulivu wa Morocco kwenye eneo la mwisho. Ouzraoui alitumia nafasi yake vizuri, Aït El Haj hakutetereka kwenye penalti, wakati Banyana ilihitaji juhudi kubwa kurejea mchezoni.

MORO 03

Mbali na Morocco, Algeria nayo imetinga hatua ya nusu fainali baada ya kuitandika Ivory Coast mabao 2-1. Mabao ya Ines Khiri na Amira Ould Braham yaliifanya timu hiyo kuandika rekodi ya kutinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza kwenye ushiriki wao.

Akizungumzia ushindi huo mfungaji wa bao la kwanza la Morocco, Ouzraoui amesema ni mafanikio makubwa kwa timu hiyo kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani.

"Pongezi ziende kwa wachezaji wote kama wenyeji wa mashindano kwetu ni kitu kikubwa kutinga nusu fainali na kufuzu kwa mara nyingine tena kucheza Kombe la Dunia kwani ni sehemu kubwa ya kuonyesha uwezo wetu," amesema Ouzraoui na kuongeza;

"Hii ni fursa kubwa kwa sababu kucheza Kombe la Dunia kutatusaidia sisi wachezaji kuonekana kimataifa kwa sababu ni mashindano ya dunia."