Wakenya waitibulia Simba ikisherehekea miaka 90
Muktasari:
- Bao la dakika ya 90+1, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, Elvis Rupia, limetosha kupeleka kilio kwa Simba iliyokuwa inasherehekea miaka 90, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936.
KLABU ya Simba imeshindwa kutamba mbele ya mashabiki wa kikosi hicho waliojitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, baada ya leo Agosti 8, 2026 kufungwa bao 1-0 dhidi ya Kenya Police FC ya Kenya, katika mechi kali ya kimataifa ya kirafiki.
Bao la dakika ya 90+1, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, Elvis Rupia, limetosha kupeleka kilio kwa Simba iliyokuwa inasherehekea miaka 90, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936.
Katika mechi hiyo ya kuadhimisha miaka 90 ya Simba tangu ilipoanzishwa mwaka 1936, ilishuhudiwa kikosi hicho kikishindwa kutamba, licha ya kucheza soka safi na kuvutia mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo.
Simba imecheza mechi hiyo ya kirafiki katika kilele cha Simba Day, ikiwa ni la 18 tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo mwaka 2009, chini ya Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Hassan Dalali na aliyekuwa katibu wake mkuu, Mwina Kaduguda.
Katika mechi hiyo, Simba ilitawala kwa kiasi kikubwa, ingawa ilishindwa kutumia vyema nafasi ilizotengeneza, hususani za kipindi cha kwanza, huku kwa upande wa wapinzani wao wakicheza kwa tahadhari ya kujilinda na kushambulia zaidi kwa kushtukiza.
Kenya Police ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu ya Kenya kwa msimu wa 2024-2025, licha ya kucheza kwa tahadhari ya kujilinda, kipindi cha pili ilitengeneza nafasi mbalimbali za kufunga na kutumia vyema mwishoni.
Katika mechi ya leo, Kocha wa Simba, Steve Barker alianza kikosi cha kwanza na mchezaji mmoja mpya ambaye ni kiungo, Ibraheem Jabaar, huku wengine wakiwa ni wale wale waliokuwepo msimu wa 2025-2026.
Kuanza na mchezaji mmoja pekee mpya, inaonyesha bado Barker anahitaji kuwaingiza kikosini taratibu, hasa ikizingatiwa mechi ijayo ni dhidi ya Yanga, katika Ngao ya Jamii, jambo lililomfanya kuendelea kuwaamini waliokuwepo tangu msimu wa 2025-2026.
Hii ni mechi ya 18, kwa Simba kucheza katika tamasha la Simba Day, tangu lilipoanzishwa mwaka 2009, ambapo kati ya hizo imeshinda 11, ikitoka sare mbili na kupoteza tano.
Kituo kinachofuata kwa Simba kwa sasa ni katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga, itakayopigwa Jumatano ya Agosti 12, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mechi hiyo kali na ya kusisimua ya 'Kariakoo Derby', inazikutanisha timu hizo ambapo kwa Yanga ni bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, huku kwa upande wa watani zao Simba ikitwaa taji la CRDB msimu huo.