Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga, Simba, Singida BS safari inaanzia hapa Kimataifa

Muktasari:

  • Katika upande mwingine wa Kombe la Shirikisho Afrika, KMKM ya Zanzibar nayo ina kazi kubwa ya kufanya, huku Singida Black Stars ikipitishwa sehemu yenye changamoto kidogo wakati Azam ikipata nafuu kwa kuanzia hatua ya pili, hata hivyo bado ina mtihani wa kuvuka kulingana na mpinzani wa baadaye.

DROO ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026-2027 iliyochezeshwaleo Alhamisi, Agosti 6, 2026, imezipa njia ya mteremko Yanga na Simba kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu huu, huku upande wa KVZ kutoka Zanzibar, hali ikionekana kuwa mbaya kwao, hivyo inahitaji maombi kutoboa.

Katika upande mwingine wa Kombe la Shirikisho Afrika, KMKM ya Zanzibar nayo ina kazi kubwa ya kufanya, huku Singida Black Stars ikipitishwa sehemu yenye changamoto kidogo wakati Azam ikipata nafuu kwa kuanzia hatua ya pili, hata hivyo bado ina mtihani wa kuvuka kulingana na mpinzani wa baadaye.


LIGI YA MABINGWA

Simba imepangwa kucheza na Mighty Wanderers ya Malawi katika raundi ya awali, hali inayokifanya kikosi hicho cha kocha Steve Barker kuanzia kampeni yake ugenini nchini Malawi.

Ikifanikiwa kuruka kiunzi hicho cha Wamalawi, katika raundi ya pili na ya mwisho kabla ya makundi, Simba itakutana na mshindi baina ya 15 Agosto ya Guinea Ikweta au Fomboni ya Comoros.

Timu hizo zote ambazo zipo kwenye njia ya Simba, hazijawahi kunusa angalau hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga chini ya Kocha Manqoba Mngqithi, yenyewe imepangwa kukutana na Gaborone United ya Botswana ambayo inanolewa na kocha raia wa Ireland Kaskazini, Sean Connor.

Gaborone United msimu uliopita ilikutana na Simba katika hatua hiyo na ilitolewa kwa kichapo cha mabao 2-1 katika mechi mbili baina ya timu hizo.

Ikifanikiwa kupenya hapo, Yanga itakutana na timu itakayoshinda baina ya CFFA ya Madagascar na Lijabatho ya Lesotho ambapo itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani.

Simba na Yanga zitaanzia mashindano hayo kwa kucheza ugenini na zitamalizia raundi hiyo ya kwanza ya awali katika viwanja vya nyumbani.

KVZ ya Zanzibar imepangwa kuanzia ugenini dhidi ya mabingwa wa Libya, Swehly.

Kama KVZ itasonga mbele, itakutana na Esperance ya Tunisia katika raundi ya pili ambapo itaanzia nyumbani na kumalizia ugenini.


KOMBE LA SHIRIKISHO

Singida Black Stars ya Tanzania Bara na KMKM ya Zanzibar, zinaanzia raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2026-2027.

Katika droo ya hatua mbili za awali za Kombe la Shirikisho Afrika iliyofanyika jana Alhamisi katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jijini Cairo, Misri, ilihusisha jumla ya klabu 56 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.

Katika droo hiyo, Singida Black Stars itaanza kampeni yake kwa kucheza dhidi ya Al Ghazala Wau ya Sudan Kusini katika raundi ya kwanza, huku KMKM ikipewa kibarua kigumu cha kuivaa Al Ahly Tripoli ya Libya.

Kwa upande wa Azam FC, ambayo ni miongoni mwa klabu nane zilizopewa nafasi ya kupita moja kwa moja hadi raundi ya pili, itakutana na mshindi wa mchezo kati ya Zed FC ya Misri na Telecom FC ya Djibouti.

Iwapo Singida Black Stars itafanikiwa kuitoa Al Ghazala Wau, katika raundi ya pili itakutana na mshindi kati ya Al Ahly Madani ya Sudan na Tusker FC ya Kenya.

Nayo KMKM ikifanikiwa kuiondoa Al Ahly Tripoli, itamenyana katika raundi ya pili na mshindi wa mchezo kati ya Al Hilal Al Sahel ya Sudan na Welwalo Adigrat ya Ethiopia.

Klabu nane zilizopewa nafasi ya kuanzia raundi ya pili kutokana na viwango vya CAF ni Al Ahly (Misri), Azam FC (Tanzania), USM Alger na CR Belouizdad (Algeria), Raja Casablanca na AS FAR (Morocco), Maniema Union (DR Congo) pamoja na Kaizer Chiefs (Afrika Kusini).


SEPTEMBA KUAMUA

Katika ratiba ya michuano hiyo yote, mechi za mkondo wa kwanza za raundi ya awali zitachezwa kati ya Septemba 4 hadi 6, 2026, huku marudiano ikipangwa kufanyika Septemba 11 hadi 13, 2026.

Raundi ya pili itaanza kwa mechi za mkondo wa kwanza zitakazochezwa kati ya Oktoba 16 hadi 18, 2026, kabla ya marudiano kufanyika Oktoba 23 hadi 25, 2026.

Baada ya hatua hizo, washindi watafuzu hatua ya makundi ambayo itaanza mwishoni mwa Novemba 2026, huku fainali ya mashindano hayo ikitarajiwa kuchezwa katika kipindi cha Mei 9 hadi 31, 2027, ingawa CAF bado haijatangaza tarehe rasmi ya mchezo wa mwisho.

Hata hivyo wakati kitita kikiongezekana kwenye bingwa wa Shirikisho hadi Bilioni 10, kule Ligi ya Mabingwa sasa mshindi atachukua bilioni 16, kazi ipo.