Mmesikia? PSG inasubiri kumbeba bure Vinicius Jr
Muktasari:
- PSG inaamini itafanikiwa kupata saini ya Vini Jr kwa uhamisho wa bure kabisa wakati itakapofika mwaka 2027.
MABINGWA wa soka wa Ufaransa na Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris St-Germain wameripotiwa kutengeneza mchakato madhubuti kabisa wa kuhakikisha wananasa saini ya supastaa wa Kibrazili, Vinicius Jr, anayekipiga kwenye kikosi cha Real Madrid.
PSG inaamini itafanikiwa kupata saini ya Vini Jr kwa uhamisho wa bure kabisa wakati itakapofika mwaka 2027.
Ripoti zinafichua wazi, Vini Jr atakuwa mchezaji huru itakapofika 2027, wakati ambapo mkataba wake huko Los Blancos utakuwa umefika tamati. Bado hakuna mazungumzo ya kuhusu dili jipya na kama Real Madrid itashindwa kumuuza Vini Jr mwakani, basi matajiri yao wa Ufaransa wamelenga kumvuta kwenye kikosi chao huko Parc des Princes kwa uhamisho wa bure kabisa 2027. Hilo likitokea litakuwa kama kulipa kisasi kwa PSG baada ya kumshuhudia supastaa wao, Kylian Mbappe aliponaswa bure na Real Madrid.
Karim Adeyemi
MSHAMBULIAJI wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi anaripotiwa kuziingiza kwenye vita kali timu za Ligi Kuu England zinazopambana kuwania huduma yake.
Manchester United ilitajwa kuhitaji saini yake, lakini sasa mambo yamedaiwa kubadilika kutokana na kuwapo kwa timu nyingine kwenye Ligi Kuu England inayomhitaji mchezaji huyo na imesimama mstari wa mbele wa kuhakikisha inamsajili mwakani.
Serge Gnabry
LIVERPOOL imeripotiwa kuwa na mpango wa kumsajili winga wa Bayern Munich, Serge Gnabry mapema 2026. Gnabry amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Bayern Munich ambacho kimekuwa na ubora mkubwa kwa msimu huu wa 2025-26, lakini sasa Liverpool inahitaji saini yake na itajaribu kupambana kumsajili. Winga huyo alicheza kwa dakika 59, Jumamosi iliyopita wakati Bayern ilipoangusha pointi dhidi ya Union Berlin kwenye Bundesliga.
Manuel Akanji
BEKI wa kati wa Manchester City, Manuel Akanji, aliyetolewa kwa mkopo kwenye dirisha lililopita anapiga hesabu za kuachana na timu hiyo jumla ili kujiunga na Inter Milan. Akanji alijiunga na Man City akitokea Borussia Dortmund mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 15 milioni na kuisaidia timu hiyo kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, sasa yupo Serie A kwa mkopo. Inter itafanikiwa kunasa jumla saini yake kwa ada ya Pauni 13.3 milioni.
Michael Olise
WINGA wa Bayern Munich, Michael Olise ameripotiwa kuzivutia klabu za Liverpool, Arsenal na Manchester United ambazo zinapambana kuwania huduma yake wakati dirisha la uhamisho wa majira ya baridi huko Ulaya litakapofunguliwa. Liverpool inamtazama Olise kama mchezaji mwafaka wa kwenda kurithi buti za Mohamed Salah huko Anfield, lakini saini yake haitakuwa rahisi kwao kutokana na timu nyingi nazo kumtaka.
James Trafford
NEWCASTLE imeripotiwa kupambana kuwania saini ya kipa wa Manchester City, James Trafford, ikimhitaji kwenye dirisha la Januari mwakani. Kipa huyo mwenye umri wa miaka 23, amefungua milango ya kuondoka Etihad kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza, huku Newcastle ikimpa uhakika wa kwenda kupata namba kikosini wakati atakapojiunga nayo.
Joao Gomes
MANCHESTER United imeripotiwa kuwa na mpango wa kuvamia kwenye kikosi cha Wolves ili kunyakua huduma ya kiungo Joao Gomes. Kocha wa Man United, Ruben Amorim anataka kufanya maboresho makubwa kwenye safu ya kiungo ya timu yake baada ya dirisha lililopita la majira ya kiangazi kutumiza zaidi ya Pauni 200 milioni kwenye kusajili mastraika.
Etta Eyong
ARSENAL imeripotiwa kuingia kwenye vita kali na klabu za Real Madrid na Barcelona katika mchakamchaka wa kumsajili staa wa Levante, Etta Eyong. Staa huyo mwenye umri wa miaka 22 alianza msimu akiwa na Villarreal kabla ya kuhamia jumla Levante kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Eyong amefunga mabao 6 na kuasisti tatu.