MLS nani atatwaa ubingwa Marekani 2026?
Muktasari:
- Kwa kuzingatia takwimu, Nashville SC ilikuwa timu iliyofanya vizuri zaidi katika msimu wa kawaida wa MLS, ikikusanya pointi 77 katika mechi 34. Ilikuwa na pointi 13 zaidi ya Vancouver Whitecaps iliyomaliza nafasi ya pili kwa pointi 64.
MIAMI, MAREKANI: NANI atatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Marekani (MLS) mwaka 2026? Ligi hiyo imeingia hatua ya mtoano, ambapo timu 16 zinachuana kuwania taji la Kombe la MLS. Baada ya hatua ya mchujo wa awali (Wild Card), FC Cincinnati na Real Salt Lake zilifanikiwa kufuzu na kuungana na timu nyingine 14 katika hatua ya 16 bora.
Timu hizo zitashiriki raundi ya kwanza inayochezwa kwa mfumo wa mechi tatu, huku kila moja ikilenga kusonga mbele hadi nusu fainali za kanda. Washindi wa hatua hiyo watakutana katika fainali za kanda, kabla ya mabingwa wa Kanda ya Mashariki na Kanda ya Magharibi kukutana katika fainali ya Kombe la MLS 2026, itakayochezwa Desemba 18. Twende pamoja!
NANI ATATWAA UBINGWA 2026?
Kwa kuzingatia takwimu, Nashville SC ilikuwa timu iliyofanya vizuri zaidi katika msimu wa kawaida wa MLS, ikikusanya pointi 77 katika mechi 34. Ilikuwa na pointi 13 zaidi ya Vancouver Whitecaps iliyomaliza nafasi ya pili kwa pointi 64.
Katika msimu huo, Nashville iliweka rekodi ya kukusanya pointi nyingi zaidi katika historia ya msimu wa kawaida wa MLS, pamoja na pengo kubwa zaidi la pointi kati ya timu iliyomaliza nafasi ya kwanza na ya pili.
Timu hiyo ilipoteza mechi tatu pekee, ikitwaa ubingwa wa Kanda ya Mashariki na tuzo ya mashabiki bora 2026. Idadi hiyo ya vipigo ni ndogo kuliko iliyowahi kurekodiwa na timu yoyote katika historia ya msimu wa kawaida wa MLS.
Timu ya mwisho kutwaa ubingwa wa msimu wa kawaida na baadaye kushinda Kombe la MLS ilikuwa Los Angeles FC mwaka 2022. Hata hivyo, inaweza kuwa jambo la kushangaza kuona kuwa Nashville siyo timu inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa Kombe la MLS 2026. Kwa mujibu wa utabiri wa kompyuta maalumu ya Opta, ina nafasi ya asilimia 18.0, chini ya Vancouver Whitecaps yenye asilimia 22.6.
UTABIRI WA KOMBE LA MLS 2026
Vancouver Whitecaps ilifungwa na Inter Miami katika fainali ya Kombe la MLS msimu uliopita. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa timu hiyo kufika fainali ya mashindano hayo, na sasa inalenga kuwa timu ya pili kutoka Canada kutwaa taji hilo, baada ya Toronto FC kufanya hivyo mwaka 2017.
Pia, Vancouver itakuwa na matumaini ya kufuata mfano wa Toronto, ambayo ilifungwa katika fainali ya MLS mwaka 2016 na Seattle Sounders, kabla ya kutwaa ubingwa mwaka uliofuata kwa kuifunga timu hiyo hiyo mwaka 2017.
Brian White ndiye mchezaji anayetarajiwa kuwa tishio kubwa kwa wapinzani wa Vancouver. Alifunga mabao 20 katika msimu wa kawaida wa 2026, idadi kubwa zaidi kuwahi kufunga katika msimu mmoja wa maisha yake ya soka. Huo pia ulikuwa msimu wake wa nne mfululizo akifunga mabao 15 au zaidi.
White amefunga mabao 15 au zaidi katika kila mmoja wa misimu minne iliyopita ya kawaida ya MLS. Alifunga mabao 15 mwaka 2023, 16 mwaka 2024, 18 mwaka 2025 na 20 mwaka 2026.
Mshambuliaji huyo aliisaidia Vancouver kufanya vizuri zaidi katika historia yake ya kushiriki MLS, kwa kutwaa ubingwa wa Kanda ya Magharibi kwa kukusanya pointi 64 na kushinda mechi 19. Takwimu hizo zilivunja rekodi zake za awali zilizowekwa mwaka 2025, ambapo ilikusanya pointi 63 na kushinda mechi 18.
Moja ya sababu zinazofanya Vancouver kupewa nafasi kubwa zaidi ya Nashville ni takwimu za msingi za msimu wa kawaida, zinazoashiria kuwa nafasi ya kwanza ya Nashville huenda isionyeshe kikamilifu kiwango chake halisi.
POINTI TARAJIWA MLS 2026
Jumla ya pointi tarajiwa za Nashville ilikuwa 54.3, ambazo zingeiweka katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa msimu wa kawaida wa MLS. Tofauti kati ya pointi halisi ilizokusanya na zile zilizotarajiwa ilikuwa 22.7, ikiwa kubwa zaidi kwa mbali kuliko timu nyingine yoyote katika mashindano hayo.
Kwa upande wa Vancouver, takwimu zake za msingi zilikuwa karibu sawa na matokeo halisi ya msimu. Timu hiyo ilikusanya pointi 64, huku pointi zake tarajiwa zikiwa 66.6. Tofauti hiyo inaonesha namna Nashville ilivyofanya vizuri zaidi ya matarajio katika pande zote mbili za uwanja mwaka 2026. Nashville ilifunga mabao 14 zaidi ya yale ambayo mfumo wa xG ulikadiria ilipaswa kufunga. Ilifunga mabao 71, wakati xG yake ilikuwa 57.0. Upande wa pili wa uwanja, iliruhusu mabao 17 pungufu ya yale yaliyotarajiwa kufungwa dhidi yake. Iliruhusu mabao 25, wakati xG ya wapinzani wake ilikuwa 42.5.
Itakuwa jambo la kuvutia kuona kama kiwango hicho cha kufanya vizuri zaidi ya matarajio kitaendelea katika mechi za mtoano.
Inter Miami inalenga kuwa timu ya kwanza kutwaa Kombe la MLS kwa misimu miwili mfululizo tangu LA Galaxy ilipofanya hivyo mwaka 2012.
Inter Miami iliifunga Vancouver kwa mabao 3-1 katika fainali ya mwaka 2025 na itakuwa na imani ya kutwaa tena ubingwa, mradi Lionel Messi awe fiti kushiriki mechi za mtoano. Mshambuliaji huyo raia wa Argentina yuko katika msimu wake wa nne akiwa na Inter Miami tangu alipojiunga na klabu hiyo Julai 2023. Takwimu zake katika mashindano hayo zinavutia sana.
Katika mechi 93 alizocheza za msimu wa kawaida na mtoano, Messi amefunga mabao 83 na kutoa asisti 49, hivyo kuhusika moja kwa moja katika mabao 132. Tangu alipoanza kuitumikia Inter Miami, hakuna mchezaji mwingine aliyehusika katika mabao mengi zaidi ya Denis Bouanga, aliyefikisha 102. Katika msimu wa kawaida wa MLS 2026, Messi alifunga mabao 26 na kutoa asisti 13. Hakuna mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi au kutoa asisti nyingi zaidi ya hizo katika ligi hiyo msimu huo.
Messi alikuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha MLS (Golden Boot) kwa misimu miwili mfululizo, na sasa anawania kuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka (MVP) mara tatu.