Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usajili MLS unaoshtua kwa mishahara minono

MLS Pict

Muktasari:

  • Lionel Messi sasa ana washindani wa karibu zaidi katika orodha ya wachezaji wanaolipwa zaidi katika Ligi Kuu Marekani, kutokana na kuwasili kwa washambuliaji wengine wawili wa zamani wa Barcelona, lakini nahodha huyo wa Inter Miami bado anaongoza kwa tofauti kubwa katika orodha hiyo, akiwa na malipo ya uhakika ya Dola 28.3 milioni kwa mwaka.

MIAMI, MAREKANI: Je, timu zilitumia kiasi gani kulipa mishahara ya wachezaji ili kupata pointi moja katika msimu wa kawaida wa Ligi Kuu Marekani (MLS) 2026? Taarifa mpya za mishahara ya wachezaji zinatoa mwanga kuhusu matumizi ya klabu mbalimbali.

Lionel Messi sasa ana washindani wa karibu zaidi katika orodha ya wachezaji wanaolipwa zaidi katika Ligi Kuu Marekani, kutokana na kuwasili kwa washambuliaji wengine wawili wa zamani wa Barcelona, lakini nahodha huyo wa Inter Miami bado anaongoza kwa tofauti kubwa katika orodha hiyo, akiwa na malipo ya uhakika ya Dola 28.3 milioni kwa mwaka.

Robert Lewandowski wa Chicago Fire na Antoine Griezmann wa Orlando City wameingia katika orodha hiyo wakiwa nafasi ya pili na ya tatu kwa mishahara mikubwa zaidi. Wakati huohuo, Breel Embolo wa Atlanta United, ambaye pia alijiunga na timu hiyo katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi, anashika nafasi ya tano akikunja Dola 10.8 milioni.

Mshambuliaji wa Los Angeles, Son Heung-min, ambaye yupo katika msimu wake wa pili, anashika nafasi ya nne akilipwa Dola 11.2 milioni.

Lakini, Casemiro, aliyejiunga na Messi mjini Miami baada ya kumaliza mkataba wake na Manchester United ndiye mchezaji wa nne anayelipwa zaidi katika timu hiyo ambayo ni Dola 3.54 milioni.

Hali hiyo imekuja baada ya Miami kutangaza usajili wake kama mchezaji asiye chini ya kundi la wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa maalumu, jambo lililowashangaza baadhi ya watu. Sababu ni kwamba Mbrazili huyo alijiunga na timu hiyo kwa uhamisho wa Bosman, badala ya mkopo wenye kipengele cha kununuliwa kama ilivyokuwa kwa Rodrigo De Paul msimu uliopita wa kiangazi ili kuifanya Miami iendelee kuzingatia kanuni za ligi.

ML 01

Lakini, Chama cha Wachezaji wa MLS kinaonyesha kuwa Casemiro analipwa mshahara wa msingi wa Dola 896,004 kwa mwezi. Takwimu zote hizo za mishahara zimetolewa katika ripoti ya Chama cha Wachezaji wa MLS, ambayo hutolewa mara mbili kila mwaka. Toleo la hivi karibuni lilitolewa saa chache kabla ya kuanza kwa hatua ya mtoano ya ligi hiyo iliyoanza juzi, Alhamisi.

Ingawa takwimu hizo hazijumuishi ada za uhamisho na hivyo haziwezi kuonyesha picha kamili ya uwekezaji wa kila timu katika kikosi chake, zinatoa mwanga muhimu kuhusu kiasi ambacho kila klabu inatumia kulipa mishahara ya wachezaji wake.

Kati ya klabu 30 zinazoshiriki MLS, timuu 13 zina mchezaji mpya anayeongoza kwa kulipwa mshahara mkubwa zaidi baada ya dirisha lenye shughuli nyingi za usajili kufuatia Kombe la Dunia 2026.

Wachezaji wawili, Anders Dreyer wa San Diego anayelipwa Dola 3.6 milioni, na Mateusz Bogusz wa Houston anayepokea Dola 2.5 milioni  wamepanda na kuwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika timu zao baada ya kuondoka kwa wenzao waliokuwa na mishahara mikubwa zaidi.

Lozano alimzidi Riqui Puig, ambaye alikuwa ameumia, baada ya kujiunga na LA Galaxy kwa mkopo akitokea San Diego.

ML 02

Lewandowski, Griezmann na Embolo nao wameingia katika kundi hilo la wachezaji wanaolipwa zaidi katika klabu zao. Kwa upande wa Charlotte, ilimbadilisha Wilfried Zaha na Allan Saint-Maximin, ambaye analipwa Dola 7.2 milioni karibu mara tatu ya mshahara wa nyota huyo wa zamani wa Crystal Palace.

Wachezaji wengine wanaolipwa mishahara mikubwa baada ya kujiunga na klabu hizo wakitokea nje ya MLS ni Brais Méndez wa Columbus anayepokea Dola 5.2 milioni; Andre Luiz wa Kansas City Dola 3.3 milioni; na Kai Wagner wa Philadelphia Dola 1.6 milioni.

Washambuliaji wawili waliohamishwa kutoka klabu moja kwenda nyingine ndani ya ligi hiyo katikati ya msimu walitia saini mikataba mipya iliyowafanya kuwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika timu zao mpya. Wachezaji hao ni Rafael Navarro wa St. Louis, anayepokea Dola 4.95 milioni na Dejan Joveljic wa Seattle anayelipwa Dola 3.7 milioni.


USAJILI MPYA ULIOFELI ZAIDI

Mchezaji aliyejitokeza zaidi kwa kushindwa kuendana na matarajio miongoni mwa wachezaji wapya wanaolipwa mishahara mikubwa ni Alexis Sanchez. Gwiji huyo wa Chile mwenye umri wa miaka 37 alijiunga na CF Montreal katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi akacheza mechi 15 za ligi akiwa na Quebec, lakini alishindwa kufunga bao wala kutoa pasi iliyozaa bao.

Malipo yake ya uhakika ya Dola 2.97 milioni yanachukua asilimia 24.6 ya jumla ya fedha zinazotumiwa na timu hiyo kulipa mishahara ya wachezaji. Kuwasili kwa Griezmann kunamaanisha kuwa Messi siyo mchezaji anayechukua sehemu kubwa zaidi ya bajeti ya mishahara ya klabu yake kama ilivyokuwa awali.

Orlando imetenga sehemu kubwa kidogo ya bajeti yake kwa ajili ya kumlipa Mfaransa huyo, asilimia 49.5, ikilinganishwa na asilimia 47.7 ambayo Miami inatumia kumlipa Muargentina huyo.

Lewandowski naye anakaribia takwimu hizo, akichukua asilimia 47.3 ya bajeti yote ya Chicago inayotumika kulipa mishahara ya wachezaji.

Muhimu kuzingatia ni kwamba mkataba wa Messi una vipengele vingine vya malipo ya ziada. Vipengele hivyo vinahusisha sehemu ya mapato yatokanayo na usajili wa huduma za Apple TV, mauzo ya bidhaa kupitia Adidas na Fanatics, pamoja na uwezekano wa kupata hisa za umiliki katika klabu ya Miami baada ya kustaafu kwake.


ML 03

MISHAHARA MINGINE MIPYA

Miongoni mwa wachezaji wengine walioingia katika orodha ya mishahara mipya ni kiungo mshambuliaji wa zamani wa Middlesbrough, Morgan Whittaker, aliyejiunga na Colorado na kulipwa Dola 2 milioni, kiungo wa zamani wa Watford na Everton, Abdoulaye Doucoure anayekipiga Charlotte anayelipwa Dola 1 milioni, beki wa kushoto wa zamani wa Man United, Tyrell Malacia aliyetua Cincinnati anapokea Dola 1.04 milioni na kiungo mshambuliaji wa zamani wa NYCFC, Santi Rodríguez ambaye sasa yupo Columbus anayekunja Dola 3.9 milioni.

Vilevile kuna mshambuliaji wa Afrika Kusini, Lyle Foster, aliyejiunga na Houston anayepokea Dola 1.8 milioni, huku mshambuliaji wa zamani wa Celtic, Kyogo Furuhashi, wa LA Galaxy, akilipwa Dola 1.1 milioni. Wengine ni winga wa Tunisia, Elias Saad anayekipiga Nashville anayepokea Dola 1.7 milioni; winga wa zamani wa Leeds United, Jack Harrison, wa New England anayelipwa Dola 3.65 milioni; na winga wa Ivory Coast, Benie Traoré anayeichezea NYCFC anayepokea Dola 2.5 milioni.

Pia yupo mshambuliaji wa zamani wa Uholanzi, Vincent Janssen, aliyejiunga na Portland analipwa Dola 1.75 milioni, winga wa Tunisia, Elias Achouri aliyepo San Diego anapokea Dola 2.6 milioni, huku kipa wa Scotland, Angus Gunn aliyepo San Jose akilipwa Dola 1.6 milioni, Damion Downs aliyejiunga na St. Louis kwa mkopo akitokea Southampton anapokea Dola 1.6 milioni.