Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania na kitendawili bwawa la Olimpiki

OLIMPIKI Pict

Muktasari:

  • Pamoja na hatua zilizopigwa katika michezo mbalimbali, kuogelea bado hakujanufaika na uwekezaji wa miundombinu unaoweza kuwapa wanamichezo mazingira yanayolingana na yale wanayokutana nayo katika mashindano ya kimataifa, yakiwamo Michezo ya Olimpiki na Mashindano ya Dunia.

ZAIDI ya miaka 60 tangu kupata Uhuru, Tanzania bado haina bwawa la umma la kuogelea lenye urefu wa mita 50 linalokidhi viwango vya kimataifa kwa ajili ya mafunzo na mashindano makubwa, hali inayowalazimu wanamichezo kutafuta mazingira bora ya maandalizi nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Pamoja na hatua zilizopigwa katika michezo mbalimbali, kuogelea bado hakujanufaika na uwekezaji wa miundombinu unaoweza kuwapa wanamichezo mazingira yanayolingana na yale wanayokutana nayo katika mashindano ya kimataifa, yakiwamo Michezo ya Olimpiki na Mashindano ya Dunia.

Tanzania ina mabwawa katika hoteli, shule, vyuo na taasisi mbalimbali, lakini mengi yana urefu wa mita 25 au chini ya hapo. Hivyo, changamoto si idadi ya mabwawa yaliyopo pekee, bali uwezo wake wa kutumika kwa mafunzo ya kitaalamu na mashindano ya kiwango cha juu.

Tofauti kati ya bwawa la mita 25 na mita 50 ina umuhimu mkubwa katika maandalizi. Katika bwawa fupi, waogeleaji hupata nafasi ya kugeuka katikati na kujisukuma ukutani, tofauti na bwawa la mita 50, ambako wanahitaji kudumisha kasi, nguvu na mbinu zao kwa umbali mrefu zaidi bila kugeuka.

OLIMPI 05

Hali hiyo inahitaji mazoezi ya kutosha katika mazingira yanayofanana na mashindano wanayotarajia kushiriki.

Kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la Kimataifa la Michezo ya Majini ‘World Aquatics’, bwawa la mita 50 kwa mashindano makubwa ya kimataifa linahitaji upana wa angalau mita 25 na kina cha chini cha mita 2.5.

Pia linahitaji vifaa vya kuanzia mashindano, mifumo ya kielektroniki ya kupima muda, sehemu za kuguswa na waogeleaji wanapomaliza mizunguko, pamoja na miundombinu mingine ya kiufundi na usalama.


OLIMPI 04

JUKUMU LA SERIKALI, WAJIBU WA KISHERIA

Kutokuwapo kwa bwawa hilo si changamoto inayopaswa kuachiwa waogeleaji na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) pekee. Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya michezo kupitia sera, uwekezaji wa miundombinu na rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya sekta hiyo.

Jukumu hilo linaonekana katika Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa, Sura ya 49, Toleo la Marejeo la mwaka 2023. Kifungu cha 4(1)(a) kinataja majukumu ya Baraza la Michezo la Taifa katika kuendeleza, kukuza na kusimamia michezo kwa kushirikiana na vyama vya michezo, ikiwamo kuwezesha mafunzo, ruzuku, maeneo ya michezo na upatikanaji wa vifaa.

Wajibu huo unaongezewa nguvu na Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ulioanzishwa kupitia kifungu cha 6A cha sheria hiyo. Kifungu cha 6A(2)(b) kinataja kuwezesha ujenzi na matengenezo ya miundombinu na vifaa vya michezo, huku kifungu cha 6A(2)(d) kikihusu utambuzi na ukuzaji wa vipaji, na kifungu cha 6A(2)(f) kikieleza kuhusu kuwezesha mafunzo ya wanamichezo.

Kwa msingi huo, ujenzi wa bwawa la mita 50 unapaswa kuangaliwa kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kukuza michezo nchini, badala ya kuwa ombi la wadau wa kuogelea pekee.

Hata hivyo, licha ya uwepo wa sheria na taasisi zinazohusika, wadau wameendelea kueleza umuhimu wa miundombinu hiyo bila kuona matokeo ya kudumu.


OLIMPI 01

SHUHUDA YA RUSHAKA

Athari za kukosekana kwa bwawa la mita 50 zinaonekana katika uzoefu wa waogeleaji waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika mashindano makubwa duniani.

Khalid Rushaka, aliyewakilisha Tanzania katika Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008, anasema mara yake ya kwanza kuogelea katika bwawa la mita 50 ilikuwa mwaka 2007 kwenye Mashindano ya Dunia yaliyofanyika Melbourne, Australia, licha ya kuwa tayari alikuwa na uzoefu wa miaka mitano katika mchezo huo. Rushaka alianza kuogelea mwaka 2002 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako alijifunza na kujenga uwezo wa kushindana katika bwawa lenye urefu wa mita 33/yadi 50. Hata hivyo, mashindano aliyokuwa akishiriki kabla ya hapo yalifanyika katika mabwawa ya mita 25.

Anasema tofauti ya mabwawa hayo ilimfanya atambue umuhimu wa kufanya mazoezi katika mazingira yanayofanana na mashindano ya kimataifa.

“Niliposhiriki Mashindano ya Dunia mwaka 2007, nilitambua ni kwa kiasi gani nilihitaji kufanya mazoezi zaidi katika bwawa la mita 50 ili kuzoea mazingira ya mashindano ya kiwango hicho,” anasema.

Baada ya kurejea kutoka Melbourne, anasema alianza kwenda katika bwawa la Kasarani jijini Nairobi, Kenya, kwa ajili ya kambi za mazoezi pamoja na Kocha John Belela (JB) na Samson Makere, walipokuwa wakijiandaa kwa Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008.

Anasema walilazimika kusafiri na kukaa Kenya ili kupata muda wa kutosha wa kufanya mazoezi katika bwawa lenye urefu sawa na lile walilotarajia kulitumia katika mashindano ya Olimpiki.

Kwa mujibu wa Rushaka, maandalizi ya mashindano makubwa yanahitaji miezi kadhaa ya mazoezi endelevu. Hivyo, kutegemea kambi za nje ya nchi kunawaongezea waogeleaji gharama za usafiri na malazi, huku wakiishi mbali na familia zao.

Anasema Tanzania inahitaji bwawa la mita 50 litakalowapa waogeleaji na makocha nafasi ya kufanya mazoezi mara kwa mara, kupima maendeleo ya wanamichezo na kuandaa mashindano ya ndani yatakayowajengea vijana uzoefu kabla ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.

Ni shauku yake kuwa kizazi kijacho cha waogeleaji wa Tanzania, kinaposhiriki Mashindano ya Dunia au Michezo ya Olimpiki, kiwe kimezoea umbali wa mita 50 kupitia mazoezi na mashindano yaliyofanyika nyumbani, badala ya kuanza kuzoea mazingira hayo kinapofika katika mashindano ya kimataifa.


OLIMPI 03

KAULI YA TSA

Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), David Mwasyoge, anasema kukosekana kwa bwawa la kisasa kunawaongezea waogeleaji gharama za maandalizi ya mashindano ya kimataifa, kwani hulazimika kuondoka nchini mapema kutafuta mazingira yanayofanana na yale ya mashindano.

“Pamoja na World Aquatics kugharimia waogeleaji, TSA kwa kushirikiana na wazazi wanalazimika kutafuta fedha za ziada kwa ajili ya kulipia gharama za mazoezi ya waogeleaji, makocha na viongozi wengine ambazo hazilipwi na shirikisho hilo la kimataifa,” anasema Mwasyoge na kuongeza:

“Ni wazi kuwa timu lazima iwahi kuondoka ili kuzoea miundombinu ya mashindano. Hivyo, TSA na wazazi wanalazimika kulipia gharama za chakula, malazi na mazoezi kwa muda wa ziada ambao haujawekwa kwenye mpango wa World Aquatics.”

“Gharama hizo tungeweza kuziepuka endapo tungekuwa na miundombinu inayotambuliwa na World Aquatics au mashirikisho mengine ya kimataifa. Hii ingemaanisha kuwa waogeleaji wetu wangeondoka kwa wakati uliopangwa na kufika kwa mujibu wa taratibu bila kuingia gharama za ziada,” anasema.

Hali hiyo inaifanya familia kuwa sehemu muhimu ya ufadhili wa maandalizi ya wanamichezo. Wazazi hulazimika kuchangia safari, malazi na mazoezi, jambo linaloweza kuwanyima fursa waogeleaji wenye vipaji wasiokuwa na uwezo wa kifedha au wafadhili.

Vilevile, fedha hizo zingeweza kuelekezwa katika vifaa, lishe na programu za kukuza vipaji nchini.


OLIMPI 02

ZANZIBAR YAKOSA MASHINDANO

Changamoto hiyo inaonekana pia Zanzibar, ambako kukosekana kwa bwawa lenye viwango vinavyohitajika kumeathiri uwezo wa chama cha mchezo huo kuendesha mashindano ya kawaida. Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Zanzibar (Chakuza), Salmin Maulid Uledi, anasema kwa miaka kadhaa sasa hawajaandaa mashindano ya kuogelea yanayokidhi vigezo vya kimataifa kutokana na kukosekana kwa bwawa la mita 50 lenye viwango vya Olimpiki.

Anasema Zanzibar ina vijana wengi wenye vipaji vya kuogelea, lakini wanakosa mazingira yanayowawezesha kuendeleza uwezo wao na kufikia malengo ya kushindana katika ngazi za juu.

Uledi anasema ingawa kuna bwawa la timu ya Wahoo linalomilikiwa na shule, gharama za kulitumia zimekuwa kikwazo kwa chama kuendesha mazoezi na mashindano kwa utaratibu unaohitajika.

“Kwa miaka mingi tulikuwa tunatumia eneo la fukwe la Forodhani kwa ajili ya kufanya mazoezi. Hata hivyo, mazoezi hayo zaidi yalikuwa ya kuwafundisha waogeleaji kuelea majini, kwa sababu hatukuwa na vifaa muhimu kama ‘diving blocks’, ‘touch pads’ na vifaa vingine vya kisasa,” anasema.

Anasema kwa sasa eneo hilo lina meli kubwa zilizoegeshwa kwa shughuli maalumu, hali iliyowalazimu kutafuta maeneo mengine ya mazoezi.

Kutokana na mazingira hayo, anasema: “Kwa sasa hatuna mashindano ya kuogelea yanayofanyika kwa kuzingatia vigezo vya bwawa la mita 50. Badala yake, tumekuwa tukifanya mashindano ya ‘Open Water’, ambayo hutumia bahari na kupima umbali wa waogeleaji.”

Uledi anasema wamekuwa na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo kwa miaka mingi, lakini ukosefu wa fedha umezuia utekelezaji wa mipango yao, huku wakibaki na ahadi za kupata miundombinu hiyo.


ITAENDELEA KESHO