Mike Maignan bado anasakwa Stamford Bridge
Muktasari:
- Chelsea inataka kurudi kwa staa huyo kutokana na kiwango kibovu ambacho kipa wao Mhispania Robert Sanchez mwenye umri wa miaka 27 amekionyesha tangu kuanza kwa msimu huu hususani katika mechi dhidi ya Manchester United.
KIPA wa AC Milan na timu ya taifa ya na Ufaransa, Mike Maignan mwenye umri wa miaka 30 anaweza kuingia tena katika ajenda ya usajili ya Chelsea dirisha lijalo la majira ya baridi.
Chelsea inataka kurudi kwa staa huyo kutokana na kiwango kibovu ambacho kipa wao Mhispania Robert Sanchez mwenye umri wa miaka 27 amekionyesha tangu kuanza kwa msimu huu hususani katika mechi dhidi ya Manchester United.
Mkataba wa sasa wa Maignan unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na ifikapo Januari atakuwa huru kusaini mkataba wa awali.
Mabosi wa Chelsea, wanaamini watampata Maignan kwa kiasi kidogo cha pesa kwani kipa huyo amegoma kusaini mkataba mpya na Milan, hivyo ni lazima watamuuza ili kuepuka kuona akiondoka bure. Katika msimu uliopita, kocha Enzo Maresca aliweka wazi kwamba havutiwi na kiwango ambacho kipa huyo amekionyesha lakini bado aliendelea kumwamini kusimama katika milingoti mitatu.
Mbali ya Maignan, Chelsea inadaiwa kumtazama pia kipa mwingine wa Brentford, Mark Flekken kama chaguo mbadala.
Joao Palhinha
TOTTENHAM Hotspur inataka kuubadilisha mkataba wa mkopo wa kiungo wa Ureno, Joao Palhinha mwenye umri wa miaka 30 kutoka Bayern Munich kuwa wa kudumu ifikapo Januari mwakani. Ikiwa Palhinha atasaini mkataba wa moja kwa moja Fulham pia itakuwa na fungu katika pesa za ada ya uhamisho. Mkataba wa Palhinha na Bayern unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi nane za michuano yote.
Dayot Upamecano
BEKI kisiki wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Dayot Upamecano mwenye umri wa miaka 26 anatamani kujiunga na Real Madrid pindi mkataba wake utakapoisha mwisho wa msimu huu. Dayot anahitajika na timu nyingi kutokana na hali ya mkataba wake. Bayern imekuwa ikipambana kumsainisha mkataba mpya lakini hadi sasa amekataa.
Adam Wharton
CRYSTAL Palace inatarajiwa kukataa ofa yoyote itakayowasilisha katika dirisha lijalo la majira baridi ili kumsajili kiungo wake wa kimataifa wa England, Adam Wharton, 21, licha ya vigogo barani Ulaya ikiwamo Liverpool na Real Madrid kuonyesha nia ya kumsajili. Wharton ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Palace lakini anataka changamoto mpya.
Gleison Bremer
LIVERPOOL, Manchester United na Chelsea zote zinamfuatilia kwa karibu beki wa Juventus na timu ya taifa ya Brazil, Gleison Bremer mwenye umri wa miaka 28. Timu zote hizi ikiwamo pia na Paris Saint Germain zinapanga kuanza kuwasilisha ofa Januari mwakani ili kuboresha zaidi safu zao za ulinzi. Mkataba wa sasa wa Bremer unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Msimu uliopita alicheza mechi nne za michuano yote.
Ruben Vargas
WINGA wa Sevilla, Ruben Vargas mwenye umri wa miaka 27 bado anafuatiliwa na Tottenham Hotspur inayotaka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya baridi mwakani. Kocha wa Spurs, Thomas Frank anaamini timu yake bado inahitaji kurekebisha eneo lao la ushambuliaji hususani pembeni.
Mkataba wa sasa wa Vargas unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Sergio Reguilon
EVERTON inafikiria kumsajili beki wa pembeni wa zamani wa Tottenham Hotspur na Real Madrid, Sergio Reguilon mwenye umri wa miaka 28 ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Spurs kumalizika mwisho wa msimu uliopita.
Mbali ya Everton, saini ya staa huyu ambaye anaweza akasajiliwa muda wowote kutokana na kuwa kwake huru anawindwa pia na Aston Villa.
Carlos Baleba
KOCHA wa Brighton, Fabian Hurzeler amemshauri kiungo Carlos Baleba aendelee kubaki hadi mwisho wa msimu huu licha ya tetesi zinazozidi kwamba Manchester United inataka kumsajili katika dirisha hili. Mashetani wekundu wanavutiwa sana na kiungo huyo wa kimataifa wa Cameroon mwenye umri wa miaka 21, kutokana na kiwango ambacho anaendelea kukionyesha. Fundi huyu anaonekana kuwa mbadala sahihi wa Casemiro ambaye kuna asilimia nyingi akaondoka mwisho wa msimu.