Michael Carrick: Man United tumepotea njia
Muktasari:
- Carrick alionekana kuguswa kihisia wakati akitoa hotuba ya dakika tano na sekunde 36 mwanzoni mwa mkutano wake na waandishi wa habari, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuheshimu nembo ya Manchester United.
MANCHESTER, ENGLAND: MENEJA wa Manchester United, Michael Carrick, amekiri wazi kuwa timu yake imepoteza mwelekeo baada ya matokeo mabaya ya hivi karibuni, huku akiahidi kuirejesha klabu hiyo kwenye misingi na utambulisho wake wa kihistoria.
Carrick alionekana kuguswa kihisia wakati akitoa hotuba ya dakika tano na sekunde 36 mwanzoni mwa mkutano wake na waandishi wa habari, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuheshimu nembo ya Manchester United.
Kauli hiyo imekuja wakati presha ikizidi kumwandama kocha huyo, kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo ambayo imeshinda mechi mbili pekee kati ya 11 ilizocheza msimu huu, huku ikiwa imeshindwa kupata ushindi katika mechi saba mfululizo.
Huo ni mwendelezo mbaya zaidi wa kutopata ushindi kwa United tangu Desemba 2015, hali inayozua maswali kuhusu mustakabali wa Carrick kwenye benchi la ufundi la miamba hiyo ya England.
Presha kwa Carrick iliongezeka zaidi baada ya United kukubali kichapo cha aibu cha mabao 4-1 dhidi ya Como Jumatano, matokeo yaliyofichua matatizo ya timu hiyo ndani na nje ya uwanja.
Kana kwamba kipigo hicho hakikutosha, kiungo na nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes, ameongeza moto baada ya kuzikosoa mbinu ya Carrick katika mahojiano yaliyofanyika baada ya mchezo huo.
Hali hiyo imezidisha mjadala kuhusu uwezo wa Carrick kuiongoza United kurejea kwenye kiwango kinachotarajiwa na mashabiki wake.
Hata hivyo, Carrick hakuitwa kwenye kituo cha mazoezi cha Carrington Alhamisi kwa sababu siku hiyo ilikuwa mapumziko yaliyopangwa kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Uongozi wa United ulithibitisha kuwa kocha huyo ataendelea kusimamia timu katika mchezo ujao dhidi ya Bournemouth, ukieleza kuwa mambo yataendelea kama kawaida.
Pamoja na kauli hiyo, hatua hiyo imechukuliwa na wengi kama nafasi ya mwisho kwa Carrick kujinusuru, huku majina kadhaa ya makocha yakitajwa kuwa yanaweza kuchukua nafasi yake.
Miongoni mwa makocha wanaohusishwa na nafasi hiyo ni Antonio Conte, Eddie Howe na Julian Nagelsmann, ambao wanatajwa kuridhi nafasi hiyo.
Pia, kocha Fabian Hurzeler anatajwa kuwa mmoja wa wagombea wenye uwezo mkubwa wa kuinoa United kutoka ndani ya Ligi Kuu England, ingawa klabu hiyo italazimika kulipa fidia kubwa ili kumpata.
TUMEPOTEZA NJIA
Akizungumza na waandishi wa habari, Carrick hakuficha kukerwa na kiwango kilichoonyeshwa na kikosi chake, akisema matokeo ya hivi karibuni hayaendani na matarajio ya klabu hiyo.
“Kwa sasa hatujafanya vizuri vya kutosha. Hilo liko wazi na tumepitia kipindi ambacho hatukijivunii hata kidogo,” amesema Carrick.
Ameongeza kuwa kipigo dhidi ya Como kilikuwa usiku mbaya kwa klabu hiyo kwa sababu mbalimbali, huku akikiri kuwa kilimuumiza binafsi kuona timu yake ikicheza kwa namna hiyo.
“Jumatano ulikuwa usiku mbaya. Ulikuwa usiku mbaya kwa sababu nyingi na uliumiza sana. Iliniumiza kuona timu yetu ikicheza vile na kuona namna mchezo ulivyoenda.
“Kama nilivyosema baada ya mchezo, haikubaliki Manchester United kucheza na kuonekana katika hali ile,” amesema.
Carrick ameeleza kuwa mashabiki ni sehemu muhimu sana ya klabu hiyo, akisema anafahamu maumivu yao baada ya kutumia muda na fedha kusafiri kuishangilia timu, lakini wakajikuta wakiondoka wakiwa wamevunjika moyo.
Amesisitiza kuwa jukumu lake kubwa ni kuhakikisha anaiandaa timu inayowakilisha vyema klabu hiyo na kuwafanya mashabiki wajivunie utambulisho wake.
“Jukumu langu ni kuiweka timu uwanjani inayoiwakilisha Manchester United na mashabiki wake, ili waweze kujivunia utambulisho tunaouonyesha.
“Hivi karibuni tumekuwa tukiondoka kwenye misingi hiyo katika baadhi ya michezo, jambo ambalo nalitambua kikamilifu na ninafanya kila linalowezekana kulirekebisha,” amesema.
AKUMBUKA ENZI ZA FERGUSON
Katika hotuba yake, Carrick alirejea misingi iliyojenga mafanikio ya Manchester United kwa miaka mingi, akitaja unyenyekevu, kujituma, kujivunia kufanya kazi kwa bidii na uwezo wa kupambana katika mazingira magumu.
Amesema klabu hiyo imekuwa ikijulikana kwa uwezo wake wa kurejea baada ya kukutana na changamoto, ikiwamo kupata mabao ya dakika za mwisho na kujenga mafanikio ya kudumu.
Carrick pia alitaja baadhi ya watu walioacha alama kubwa katika historia ya United, akiwamo Ryan Giggs, Wayne Rooney, Sir Alex Ferguson, Sir Matt Busby na Sir Bobby Charlton.
Akizungumzia Giggs, mmoja wa wachezaji wakubwa kuwahi kuitumikia klabu hiyo, Carrick amesema mafanikio ya mchezaji mmoja hayapaswi kuwekwa mbele ya maslahi ya Manchester United.
“Manchester United daima imekuwa kubwa kuliko mtu mmoja mmoja na itaendelea kuwa hivyo. Ni kubwa kuliko mimi na ni kubwa kuliko mchezaji yeyote.
“Nilibahatika kuwafahamu baadhi ya wachezaji na kucheza nao. Ryan Giggs, ambaye bila shaka ni mmoja wa wachezaji wakubwa kuwahi kuichezea klabu hii, lakini haikuwa kuhusu Ryan Giggs, ilikuwa kuhusu Manchester United,” amesema.
Pia alimpongeza Rooney kwa kujitoa kwake kwa ajili ya timu, akieleza kuwa hata akiwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo, jambo muhimu zaidi kwake lilikuwa kucheza kwa manufaa ya timu.
Carrick alimwelezea Ferguson kuwa kocha bora zaidi kuwahi kutokea, akisema kipaumbele chake kikuu kilikuwa mafanikio ya Manchester United.
Alirejea pia mchango wa Busby na Charlton katika kuijenga upya klabu hiyo, akisisitiza kuwa historia yake imejengwa juu ya uvumilivu, unyenyekevu na kufanya kazi kwa bidii.
“SINA HAKI YA KUWA HAPA”
Carrick amesisitiza kuwa historia kubwa ya Manchester United haipaswi kuwafanya wachezaji, makocha au viongozi wa klabu hiyo wajione wana haki ya kushinda bila kufanya kazi kwa bidii.
Amesema mafanikio ya zamani ni sehemu ya historia ya klabu hiyo, lakini hayawezi kuwa dhamana ya ushindi katika kila mchezo.
“Sina haki ya kuwa hapa. Kujiona una haki ya kupata mambo fulani hakuwezi kukubalika katika klabu hii. Hatuna haki ya kushinda kwa sababu tu tumewahi kufanya hivyo zamani.
“Tuna historia ya ajabu, lakini hiyo haimaanishi kuwa tunastahili kushinda moja kwa moja. Inahitaji kufanya kazi kwa bidii na kujitoa kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Kocha huyo ameongeza kuwa wachezaji wanapaswa kuwa tayari kujitolea kwa ajili ya klabu na wenzao, hata pale wanapolazimika kufanya mambo magumu yasiyopendeza.
Amesema anataka kuona mashabiki wakirejeshewa furaha, nguvu, shauku na uhusiano mzuri waliokuwa nao na timu katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, ambacho alikitaja kuwa kizuri kwa kiwango kikubwa.
“Tumekuwa na kipindi ambacho tulifanya mambo mengi vizuri, lakini kwa sasa tumepoteza njia kidogo, nikisema ukweli. Hata hivyo, tutairejesha hali hiyo. Nina imani kabisa kwamba tutafanikiwa.
“Ninaheshimu klabu hii na ninaelewa kinachohitajika ili kuifanyia kazi na kushinda. Hilo ni jambo muhimu sana kwangu,” amesisitiza Carrick.