Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TRA United, Yanga mechi ya mtego Ligi Kuu

ARUSHA Pict

Muktasari:

  • Simba inaongoza msimamo ikiwa na pointi 24 huku Yanga ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 18. Tofauti hiyo inaifanya mechi ya leo kuwa muhimu kwa mabingwa hao watetezi, ambao wanahitaji pointi tatu ili kuendelea kuwasogelea wapinzani wao wa jadi kileleni.

YANGA inahitaji ushindi leo, Jumamosi, dhidi ya TRA United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha ili kupunguza pengo la pointi sita dhidi ya vinara Simba, lakini mbele yake kuna kikwazo cha timu ambayo imewahi kuvuruga mipango ya Wananchi katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Simba inaongoza msimamo ikiwa na pointi 24 huku Yanga ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 18. Tofauti hiyo inaifanya mechi ya leo kuwa muhimu kwa mabingwa hao watetezi, ambao wanahitaji pointi tatu ili kuendelea kuwasogelea wapinzani wao wa jadi kileleni.

Ushindi dhidi ya TRA utaifikisha Yanga pointi 21 na kupunguza tofauti dhidi ya Simba hadi pointi tatu, ikiwa vinara hao hawataongeza pointi. Hata hivyo, ili kufanikisha hilo, Wananchi wanapaswa kuhakikisha wanatumia nafasi wanazopata na kuepuka makosa yanayoweza kuwagharimu, hasa baada ya kupoteza mchezo wao uliopita.

ARU 01

Sasa mchezo dhidi ya TRA unakuwa nafasi ya kurejea kwenye ushindi na kurejesha imani kwa mashabiki, huku wakijua kuwa kupoteza pointi nyingine kunaweza kufanya kazi ya kuifukuzia Simba kuwa ngumu zaidi.

Kwa upande wa TRA United, matokeo ya mechi tano za mwisho za ligi yanaonyesha mwendelezo usioridhisha. Timu hiyo imeshinda mchezo mmoja, imetoka sare mbili na kupoteza miwili, ikifunga mabao manne na kuruhusu manne.

Pamoja na tofauti ya nafasi na pointi, TRA ina kumbukumbu ya ushindi dhidi ya Yanga inayoweza kuipa imani. Novemba 7, 2024, TRA iliishangaza Yanga kwa kuifunga mabao 3-1 katika mchezo wa ligi.

YANG 02

Kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amekiri kuwa timu yake haikuwa na mchezo mzuri dhidi ya Simba na kwamba makosa yao wenyewe ndiyo yaliyowagharimu.

 Amesema wachezaji wake wana wajibu wa kurekebisha hali hiyo huku akisisitiza umuhimu wa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa timu sapoti katika mchezo wa leo.

“Hatukuwa na mchezo mzuri dhidi ya Simba, siwezi kusema vinginevyo. Tuliadhibiwa kutokana na makosa yetu wenyewe na tuna wajibu wa kurejea. Ili tufanye hivyo, tunahitaji mashabiki wetu waje kwa wingi kutuunga mkono. Hatutawakatisha tamaa,” amesema Mngqithi.

Kocha huyo ameongeza kuwa timu yake bado ina uwezo wa kufanya vizuri licha ya kupoteza dabi, akieleza kuwa katika soka kuna kushinda na kushindwa.

Alisisitiza kuwa yeye, benchi la ufundi na wachezaji wanapaswa kuendelea kutoa kiwango bora katika kila mchezo. Kwa Yanga, sasa muhimu ni kugeuza dhamira hiyo kuwa matokeo, hasa ikizingatiwa kuwa inahitaji pointi tatu ili kupunguza tofauti ya pointi  dhidi ya Simba.

Kwa upande wa TRA United, kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ amekiri kuwa mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na aina ya mpinzani wanayekutana naye, lakini akasisitiza kuwa kikosi chake kimejiandaa kufanya vizuri.

“Haitakuwa mechi nyepesi kutokana na aina ya timu ambayo tunaenda kukutana nayo. Sisi kama TRA tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Morocco ambaye aliwahi kuinoa Taifa Stars.

ARU 02

Mechi nyingine za Ligi Kuu zinazotarajiwa kuchezwa leo, JKT Tanzania watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, kuwakaribisha Kagera Sugar iliyozaliwa upya chini ya kocha Cedrick Kaze.

Namungo FC ikiwa nyumbani Ruangwa, Lindi, kocha Juma Mgunda atakuwa na kibarua kizito dhidi ya klabu yake ya utoto Coastal Union.

Mgunda msimu huu amekuwa na rekodi nzuri nyumbani akishinda mechi mbili mfululizo alizocheza Uwanja wa Majaliwa hivyo kasi hiyo anategemea kuiendeleza leo dhidi ya Coastal Union inayoshika nafasi 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.