Miaka 10: Man United yavunja rekodi ya usajili
Muktasari:
- Takwimu za Transfermarkt kuanzia msimu wa 2016/17 zinaonyesha United imetumia takribani pauni1.77 bilioni kununua wachezaji, huku ikipata karibu pauni518 milioni pekee kutokana na mauzo. Hivyo, matumizi yake halisi yanafikia takribani pauni1.25 bilioni.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeibuka kuwa klabu iliyotumia fedha nyingi zaidi kwa usajili kuliko mapato iliyopata kupitia mauzo ya wachezaji katika muongo mmoja uliopita, licha ya Chelsea kutumia karibu pauni bilioni moja zaidi katika kununua wachezaji.
Takwimu za Transfermarkt kuanzia msimu wa 2016/17 zinaonyesha United imetumia takribani pauni1.77 bilioni kununua wachezaji, huku ikipata karibu pauni518 milioni pekee kutokana na mauzo. Hivyo, matumizi yake halisi yanafikia takribani pauni1.25 bilioni.
Chelsea ndiyo iliyotumia fedha nyingi zaidi kwa ujumla katika kipindi hicho, ikitumia karibu pauni2.67 bilioni kununua wachezaji. Hata hivyo, klabu hiyo imeingiza takribani pauni1.83 bilioni kutokana na mauzo, hivyo matumizi yake halisi yanakuwa karibu pauni836 milioni.
Kwa upande wa matumizi halisi, Manchester City inashika nafasi ya pili ikiwa imetumia takribani pauni 1.10bilioni, ikifuatiwa na Arsenal kwa pauni1.09 bilioni na Tottenham Hotspur kwa pauni942 milioni.
Tofauti ya shughuli za usajili kati ya Chelsea na United pia inaonekana katika idadi ya wachezaji. Chelsea imesajili wachezaji 83 na kuuza 125, wakati United imesajili 48 na kuuza 48 katika kipindi hicho.
Usajili wa rekodi wa United katika kipindi hicho ulikuwa Paul Pogba, aliyerejea kutoka Juventus mwaka 2016 kwa pauni89 milioni, kiasi kilichokuwa rekodi ya dunia wakati huo. Miaka sita baadaye, Pogba aliondoka United bila klabu hiyo kupata ada ya uhamisho.
United pia imetumia fedha nyingi kumsajili Antony, Harry Maguire, Romelu Lukaku na Jadon Sancho, huku baadhi ya usajili huo ukishindwa kuendana na thamani kubwa iliyolipwa.
Chelsea nayo imekuwa ikifanya biashara kubwa katika dirisha la usajili. Miongoni mwa usajili wake ghali zaidi ni Moises Caicedo, aliyesajiliwa kwa pauni115 milioni, kabla ya rekodi hiyo kuvunjwa Julai mwaka huu baada ya klabu hiyo kumsajili Morgan Rogers kutoka Aston Villa kwa pauni117 milioni.
Mauzo makubwa ya Chelsea pia yameisaidia kupunguza matumizi yake halisi. Mfano mwingine ni Enzo Fernandez, ambaye Chelsea ilimsajili kwa fedha nyingi lakini baadaye akauzwa kwa pauni125 milioni.
Kwa Arsenal, usajili ghali zaidi katika kipindi hicho bado ni Declan Rice, aliyenunuliwa kutoka West Ham United kwa pauni105 milioni mwaka 2023.
Liverpool ilivunja rekodi ya Uingereza msimu uliopita kwa kumsajili Alexander Isak kwa pauni milioni 125, kabla ya kukaribia kiwango hicho tena msimu huu kwa kumsajili Bradley Barcola kutoka Paris Saint-Germain kwa ada ya awali ya pauni 107milioni.
Nje ya England, Paris Saint-Germain ndiyo iliyotumia fedha nyingi zaidi katika kipindi hicho, huku ikishikilia pia rekodi ya dunia ya usajili baada ya kumsajili Neymar kutoka Barcelona kwa pauni200 milioni mwaka 2017.
Barcelona inashika nafasi ya tisa katika matumizi ya jumla, licha ya kutumia pauni142 milioni kumnunua Philippe Coutinho. Real Madrid kwa upande mwingine, inashika nafasi ya 14 baada ya kuvunja rekodi yake ya usajili kwa kumnunua Yan Diomande kwa pauni115 milioni.
Bayern Munich haipo katika 15 bora, huku Newcastle United ikiwa klabu nyingine ya Ligi Kuu England iliyopo ndani ya 10 bora, ikinufaika pia na mapato makubwa kutokana na mauzo ya Isak na Tonali katika miaka ya karibuni.
Matumizi makubwa yanaendelea kuongezeka katika Ligi Kuu England, huku klabu zake zikitumia rekodi ya pauni3.46 bilioni katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi pekee.