Sababu ratiba ya Ligi Kuu kupanguliwa
Muktasari:
- Uamuzi huo umefanyika baada ya Bodi kutathmini ratiba ya mashindano ya kimataifa yanayozikabili klabu hizo pamoja na mahitaji ya kiuendeshaji katika kuhakikisha ligi inaendelea bila migongano ya ratiba.
BODI ya Ligi Kuu Tanzania imefanya mabadiliko katika ratiba ya Ligi Kuu Bara msimu huu, hatua ambayo imehusisha michezo ya vigogo Simba na Yanga huku ikisisitiza kuwa mabadiliko hayo hayataathiri tarehe ya mwisho ya ligi.
Uamuzi huo umefanyika baada ya Bodi kutathmini ratiba ya mashindano ya kimataifa yanayozikabili klabu hizo pamoja na mahitaji ya kiuendeshaji katika kuhakikisha ligi inaendelea bila migongano ya ratiba.
Kaimu Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Yahya Abushehe, alisema maboresho hayo hayamaanishi kuwa msimu utamalizika tofauti na ilivyopangwa, bali ni mpangilio wa michezo unaolenga kukidhi mahitaji ya kalenda ya mashindano.
“Bodi imefanya maboresho ya ratiba ya michezo hiyo kwa kuzingatia sababu za kiuendeshaji na mahitaji ya kalenda ya mashindano. Uamuzi huo umefanywa na Bodi baada ya kutathmini mazingira yote ya uendeshaji wa ligi,” alisema Abushehe.
Aliongeza kuwa: “Licha ya mabadiliko hayo, tarehe ya kufungwa kwa Ligi Kuu msimu huu itaendelea kuwa ileile iliyowekwa kwenye ratiba, hivyo hakuna kitakachobadilika.” Mabadiliko ya ratiba hiyo imegusa mechi ya Yanga dhidi ya Geita Gold ambayo awali ilipangwa kuchezwa Septemba 8, 2026, lakini sasa itakuwa Septemba 15, 2026.
Hatua hii imechukuliwa ili kuwapa muda wa kutosha wa kujiandaa na kusafiri kurejea nchini baada ya kucheza na Gaborone United huko Botswana, Septemba 5, 2026, kisha kurudiana nao Septemba 12, 2026.
Simba pia mechi yake ya Septemba 9, 2026 dhidi ya Azam imesogezwa mbele hadi Septemba 16, 2026, kupisha mchezo wao wa ugenini dhidi ya Mighty Wanderers nchini Malawi unaotarajiwa kupigwa Septemba 6, 2026 na marudiano yake Septemba 13, 2026.
Mabadiliko ya ratiba si jambo jipya katika Ligi Kuu Bara, hasa pale zinapokuwepo kalenda za mashindano ya kimataifa, timu za taifa au mashindano ya ndani. Msimu uliopita, Dabi ya Kariakoo ilipitia mabadiliko ya ratiba.
Mchezo wa kwanza kati ya Yanga na Simba uliokuwa umepangwa Desemba 13, 2025 ulibadilishwa na baadaye ukachezwa Machi 1, 2026, huku mchezo wa pili nao ukapangwa baadaye.
Msimu huo pia TPLB iliwahi kubadilisha ratiba ya mchezo wa Mbeya City dhidi ya Simba kutoka Juni 18 hadi Juni 17, 2026, huku muda nao ukibadilishwa kutoka saa 10:00 jioni hadi saa 8:00 mchana kwa sababu za kiuendeshaji.