Doumbia apewa maujanja mapya Simba
Muktasari:
- Doumbia alijiunga na Simba akitokea AS Korofina ya Mali akiwa na rekodi nzuri ya ufungaji, baada ya kufunga mabao 17 kwenye ligi ya Mali msimu uliopita na kumaliza akiwa mfungaji bora.
MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Doumbia, ameendelea kuibua mijadala, ishu ya namna bora ya kutumika ndani ya mfumo wa timu hiyo ikichukua nafasi, huku mchambuzi wa soka, Godlisten Muro, akieleza kuwa changamoto kubwa si uwezo wa mshambuliaji huyo, bali ni namna anavyohusiana na mfumo wa sasa wa Simba.
Doumbia alijiunga na Simba akitokea AS Korofina ya Mali akiwa na rekodi nzuri ya ufungaji, baada ya kufunga mabao 17 kwenye ligi ya Mali msimu uliopita na kumaliza akiwa mfungaji bora.
Hata hivyo, katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, hajafanikiwa kufunga wala kuasisti, hali iliyoongeza presha juu yake.
Muro ameeleza kuwa, tatizo la Doumbia linaweza kutazamwa zaidi katika mfumo, akilinganisha namna mshambuliaji huyo anavyocheza kuendana na wachezaji wengine wa Simba katika eneo la juu.
“Ukiwaona Libasse (Gueye) na (Anicet ) Oura, unaona flow ya timu, unaona umeme unavyotiririka. Akishacheza Doumbia, anaweza kuilazimisha timu itoke kwenye system moja kwenda kwenye system nyingine,” amesema Muro.
Kwa mujibu wa Muro, Simba inaonekana kujengwa zaidi katika kutumia pasi za haraka, mwendo na kasi za wachezaji wa mbele, hivyo mshambuliaji anayepaswa kucheza ndani ya mfumo huo anatakiwa kuwa sehemu ya ushirikiano badala ya kusubiri tu mpira wa mwisho.
“Timu ambayo ina watu wanaokimbia eneo la juu inahitaji kuwa na watu ambao wanaweza kukamilisha ile circuit (mzunguko) ya mashambulizi kwa pamoja. Ndiyo maana ukimwona Libasse, Oura na (Elie) Mpanzu, wanaweza kukimbia na kuhusiana kwa sababu wanaelewana kimfumo,” amesema.
DOUMBIA AINGIE KWENYE MFUMO
Muro amesema suluhisho si Simba kubadilisha mfumo mzima ili kumfaa Doumbia, bali mshambuliaji huyo anatakiwa kujifunza namna ya kuingia katika mfumo ambao tayari unafanya kazi.
“Ni ngumu sana timu kupambana kuingia kwenye mfumo wa mchezaji. Ni mchezaji kukaa kwenye mfumo wa timu,” amesema.
SI MSHAMBULIAJI MBAYA
Muro anasisitiza kuwa, kutofunga kwa Doumbia hakumaanishi uwezo wake umepungua.
“Inaweza isiwe mbaya kwake na inaweza isiwe mbaya kwa Simba. Kinachoweza kuwa tatizo ni kutokulingana kwa namna ya uchezaji. Anaweza kuwa mchezaji mzuri, lakini akawa anatoka nje ya matarajio ya kimfumo,” amesema.